Sunday, November 18, 2012

UPENDO.


   Upendo wa kweli ni kumpenda mtu yule anayekuchukia, siyo kwa sababu ya mali au vitu alivyonavyo bali kwa sababu moyo umeamua kumpenda.

Jambo hilo ni gumu sana kwa wengi wetu, kwani tunawapenda wanaotupenda tu na hata kukawa na msemo unaosema “mpende akupendaye, asiyekupenda achana naye”. Tabia hii imeingia hadi makanisani, upendo wa wapendwa wengi wa siku hizi ni kupendana wao kwa wao tu, kusaidiana wao kwa wao tu na hata kutembeleana ni wao kwa wao tu. Huu siyo upendo aliotufundisha Bwana Wetu Yesu Kristo, ni kosa!

Kama wewe ni mkristo au siyo mkristo na unampenda mtu kwa sababu ana kitu au mali inayokunufaisha kwa namna moja au nyingine, bado hauna upendo. Kwa sababu mtu huyo akiondokewa na hicho kinachokufanya umpende, upendo wako kwake utayeyuka wote.

Upendo ni nini?
 Mathayo 5:44 “lakini Mimi (Yesu Kristo) nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”.

Upendo ni kuwapenda watu wote; rafiki zetu na adui zetu, na kuwaombea pia wapate mema na siyo mabaya.

Wakristo wa siku hizi ili wakuombee basi ni lazima yawe maombi ya kanisa kwa ujumla, au kuwe na jambo zuri umetenda kwa manufaa na faida yao. Ukimpa zawadi ya kitu au pesa, atakuombea Baraka hata kufunga atafunga. Lakini asipopewa kitu, mkristo huyu hana muda wa kukuombea. Huo siyo upendo tulioagizwa na Bwana wetu Yesu Kristo. (Luka 6:27)

Upendo huu ni kuwapenda watu wote kama nafsi zetu; kama vile tunavyojipenda sisi wenyewe ndivyo tuwapende na wenzetu.
Mathayo 19:19 “…mpende jirani yako kama nafsi yako”.
Kama wewe ukilala njaa siyo kwa sababu upo katika maombi ya kufunga, bali kwa sababu umekosa chakula utakavyoumia ndivyo uumie vile vile ukisikia jirani yako amelala njaa pasipo kujali kuwa ni mkristo mwenzako au siyo mkristo, ni rafiki yako au adui yako. Huu ndiyo upendo wa Yesu Kristo, tena ni amri (Marko 12:31).

Nini faida za upendo?
Sadaka pasipo upendo haifai kitu. Ukikosa upendo kwa jirani yako yoyote, sadaka unayoitoa madhabahuni si kitu. Upendo unafaa kuliko sadaka unayoiona ni nono, au inayogusa moyo wako.
Marko 12:33 “…na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia”.

Kutukamilisha. Kama jinsi Baba yetu wa Mbinguni alivyomkamilifu kwa sababu alimtoa Yesu Kristo afe ili kutukomboa kwa sababu anatupenda, na sisi tukiwapenda wenzetu wote tunakamilishwa kama Mungu mwenyewe alivyo mkamilifu.
Mathayo 5:45,48 “ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Pendo litawavuta wasiomjua Mungu, wamjue Mungu. Tukiwapenda wote; wakristo na wasio wakristo, frafiki zetu na adui zetu, tunamtambulisha Mungu wetu mwenye upendo kwa watu wote kwao. Na kwa njia hii ya upendo huu wa dhati, tunawafanya wasiomjua Mungu nao wamjue Mungu kupitia upendo wetu kwao.

Upendo wa namna hii hauji ila kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na endapo umekosa upendo huu siyo kosa kwani unaweza kuupata sasa. Yesu mwenyewe alisema, ombeni lolote mtakalo kwa jina langu na Baba wa mbinguni atawapa. Kama umekosa upendo aliotuagiza Yesu, omba na kwa imani Mungu wetu atakupa.
Yohana 14:13 “Nanyi mkiomba lolote (upendo) kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana”.

Mungu aliyetukuka, mtakatifu awabariki wote.


Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts