Friday, December 7, 2012

NJIA UTAKAYOICHAGUA NDIYO NJIA UTAKAYOPITA.

   Mwanadamu wa kwanza aliumbwa katika ukamilifu; kiroho na kimwili, mtakatifu asiyejua dhambi na mwenye mwili usioonja mauti. Baada ya kuasi agizo la Mungu na kutenda dhambi, akapoteza ukamiliu wa utakatifu, lakini kwa vile Mungu ni pendo, anatupenda wanadamu akatuandalia ukombozi ili atununue kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika Ufalme wa Mwana wa pendo lake, Yesu Kristo.

   Lakini kuupokea ukombozi huo, ni hiyari ya mwanadamu mwenyewe, kwani baada ya kuitambua dhambi mwanadamu huyu alipata utashi wa kutambua wema na uovu (Mwanzo 3:7).
Kumbukumbu la Torati 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimeweka mbele yako uzima na mauti… basi chagua uzima ili uwe hai, wewe na uzao wako”.
Yeremia 21:8 “Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi, tazama naweka mbele yenu njia ya uzima na njia ya mauti”.

   Katika kitabu cha Torati, Mungu anaapa (anazishuhudiza) kwa mbingu na nchi kuwa ametuwekea wanadamu njia mbili mbele yetu, ambazo ni uzima na mauti. Na kwa sababu Mungu ni pendo, anatushauri kuichagua njia ya uzima.

   Na siyo anatushauri tu, pia anatupa na sababu ya kwanini anatushauri kuchagua uzima, anasema ili uwe hai. Kuwa hai ni kupokea uzima wa milele, baada ya hukumu yenye kutisha ya Mungu yenye haki, siku atakapo tuhukumu wanadamu sawa sawa na matendo yetu.
Na katika kitabu cha Yeremia, Mungu anarithibitisha neno lake kuwa ameweka njia mbili mbele yetu; moja ni njia itupayo uzima na nyingine ni njia ya mauti. Ni juu yetu kuamua tunachagua na kuifuata njia ipi.

   Kuchagua njia ya uzima ni lazima kwanza uifahamu hiyo njia, ni ipi na unawezaje kuichagua na kuifuata. Njia ya uzima ni Yesu Kristo, kuchagua njia ya uzima ni kumchagua na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako. Na kuifuata njia ya uzima ni kutimiza na kutenda mapenzi ya neno la Mungu, kufuata na kushika neno la Yesu mwenyewe kwa matendo dhahiri.

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi”.

   Ile njia ya uzima ambayo Mungu aliziapia mbingu na nchi kuwa ameiweka mbele yetu na kutushauri kuichagua na kuifuata hiyo, ndiyo hiyo inafunuliwa katika kitabu cha Yohana Mtakatifu. Yesu mwenyewe anajidhihirisha kuwa yeye ndiye njia, na siyo njia tu, ina uzima ndani yake amboyo kupitia hiyo tunaurithi Ufalme wa Mungu.

   Kuchagua njia ya uzima kunapaswa kuendane na matendo ya uzima, tusikiri kwa maneno ya vinywa vyetu kuwa tunao uzima (tumempokea Yesu Kristo) na wakati huo huo matendo yetu ni kinyume na kukiri kwetu.

Mathayo 3:8 “Basi zaeni matunda yapasayo toba”, matunda ni matendo na toba ni kuupokea uzima, sasa matendo yetu yanapaswa kuenenda kama jinsi tulivyoupokea huo uzima.
Cha kushangaza, Wakristo wengi wa siku hizi wanatenda kinyume na wanavyokiri katika vinywa vyao. Na kusababisha jina la Mungu litukanwe.

Tito 1:16 “Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana”, kukiri kuwa umempokea Yesu Kristo na unahudhuria katika nyumba za ibada lakini matendo yako ni kinyume na kukiri kwako ni sawa na kupoteza muda!

   Kuchagua njia ya uzima na kutoifuata kwa matendo njia hiyo kunamadhara yafuatayo;

Kulitukanisha jina la Yesu; watu wanapoyatazama matendo yetu wanategemea kuona maisha yetu yakiakisi maisha halisi ya Yesu Kristo, na inapokuwa tofauti ndipo jina la Yesu linapotukanwa (2 Petro 2:2).

Kurithi mauti na kuzimu; kutotembea katika njia ya uzima ni kutembea katika njia ya mauti, na kutembea katika njia ya mauti ni kuchagua mauti (Mithali 12:28, 15:24).

Njia utakayopita katika uhai wako ndiyo njia utakayo iendea baada ya kifo, ikiwa umechagua njia ya uzima lakini unapita katika njia ya uovu basi baada ya kifo pia utaiendea njia uliyokuwa ukiipitia. Hapa haijarishi ni dua, swala au maombi mengi kiasi gani utafanyiwa wakati wa mazishi yako.

 Unachochagua kuishi ndicho utakacho tunukiwa.
Mathayo 16:27 “… ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”, kila mmoja wetu atalipwa kwa kadiri ya alivyotenda alipokuwa hai na siyo kwa kadiri ya sala za kumuombea awekwe pema peponi (Yohana 5:28-29).

Kama umechagua njia ya uzima, tembea katika njia ya uzima maisha yako yote kwa uaminifu.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts