Saturday, June 8, 2013

KWA NINI YOHANA MBATIZAJI ALIULIZA, “WEWE NDIWE YULE AJAYE, AU TUMTAZAMIE MWINGINE?” MATHAYO 11:3.



Yohana Mbatizaji aliuliza swali hilo kana kwamba hamjui Yesu Kristo na hakuwahi kumuona bali alizisikia habari za ujio wake tu.

Lakini ukisoma maandiko utaona kuwa Yohana mbatizaji alikuwa akimjua Yesu Kristo na aliwahi kukutana naye;

Mathayo 3:11. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 

Mstari huo wa Biblia unatueleza kuwa Yohana Mbatizaji aliutambua ujuo wa Yesu Kristo hata kabla hajaonana na Yesu Kristo mwenyewe.

Mathayo 3:13-14. Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?

Mstari huo wa Biblia unathibitisha kuwa Yohana Mbatizaji aliwahi kukutana na kuongea na Yesu Kristo, na alimtambua kuwa ndiye Masihi wa Mungu kwa sababu alitaka kumzuia asimbatize bali yeye Yohana ndiyo abatizwe na Yesu. Pia sauti ya uthibitisho ilisikika kutoka mbinguni, na mkutano wote waliisikia (Mathayo 3:17).

Sasa iwaje Yohana Mbatizaji alipokuwa gerezani na alipozipata habari za Yesu Kristo na matendo ya miujiza aliyoifanya (alizijua nguvu zake pia, Mathayo 3:11b), aliwatuma wanafunzi wake wakamuulize Yesu Kristo swali hili; “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Mathayo 11:3.

Yohana Mbatizaji aliuliza swali hili kwa sababu; alitegemea Yesu Kristo angeenda kumuona gerezani, na alitegemea kupata kipaumbele kutoka kwa Yesu katika kipindi alichokuwa kizuizini, lakini Yesu Kristo aliwapa kipaumbele wenye dhambi na watoza ushuru (Luka 15:2).

Yesu Kristo alitambua makusudi ya Yohana Mbatizaji kuuliza swali hilo, ndipo alipowajibu wanafunzi wa Yohana Mbatizaji;

(a). “Nendeni mkamueleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.” Mathayo 11:4, 5. 

Hapa Yesu Kristo alikuwa akimthibitishia Yohana Mbatizaji kuwa yeye ndiye.

(b). baada ya wanafunzi wa Yohana Mbatizaji kuondoka Yesu Kristo akaongezea, “Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo. Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi!” (Mathayo 11:16-19). 

Ukiangalia pia Luka 5:30-32. Ikawa mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.

Hapo Yesu Kristo alitaka kutufundisha kuwa anachokipa kipaumbele zaidi ni kile kilichomleta duniani; kuutangaza ufalme wa Mungu na kuziokoa roho zinazopotea dhambini. Ndipo aliposema mfano huu, “ni nani kwenu aliye na kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?”, “Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu”. Luka 15:3-7.

Yesu Kristo anazidi kufafanua kuwa, yeye kuwa karibu na wenye dhambi ni ili aziokoe roho zao. Hawapi kipaumbele zaidi wenye haki, bali wenye dhambi.



Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts