Wednesday, March 12, 2014

HATUA ZA KUUKULIA WOKOVU NA NEEMA YA MUNGU



 Tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapozaliwa, kuna hatua mbali mbali za ukuaji na majina ya hatua hizo hutofautiana kutoka hatua moja hadi hatua nyingine. Inapotokea mtoto amezaliwa, lakini haongezeki kimo, uzito, ufahamu licha ya kuongezeka kwa idadi ya miaka, hicho ni kiashilia tosha kuwa mtoto huyo ana matatizo ya ukuaji kiafya. Ni lazima wazazi wa mtoto huyo watafute msaada wa kitabibu haraka sana iwezekanavyo.

Katika ulimwengu wa kiroho pia, mtu yoyote anapompokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake, anakuwa amepokea wokovu. Wokovu unalingana na ukuaji wa mwanadamu, ni lazima mtu huyu aukulie wokovu na neema ya Mungu kutoka hatua ya kwanza kabisa hadi kufikia hatua ya mwisho ambayo ni ufufuo wa uzima wa milele.

Katika somo letu hili lenye kichwa, “hatua za kuukulia wokovu na neema ya Mungu”, tutajifunza hatua kuu tatu ambazo mtu aliyeokoka ni lazima azipitie. Ni maombi yangu kwamba, Roho Mtakatifu akufundishe kwa utulivu na undani ili upate kuelewa na kujitambua uko hatua ipi na unatakiwa kwenda hatua ipi, na ufanye nini ili kuifikia hatua iliyopo mbele yako.

Hatua za kuukulia wokovu na neema ya Mungu, nimezigawa katika hatua kuu tatu ambazo zina hatua nyingine ndogo ndogo ndani yake kulingana na vile Roho Mtakatifu alivyonijalia;

Kuamini na kuokoka

Kumjua Mungu, kumjulisha Mungu kwa wengine na Mungu kukujua wewe

Kufanyika rafiki wa Mungu

1. KUAMINI NA KUOKOKA

(a). kuamini
Marko 16:16, aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa
Yohana 3:16, kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu (mwanadamu), hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (wokovu)
Katika mistari miwili hiyo hapo juu, kuna kitu tunajifunza. Kitu hicho ni lazima kuamini ndipo wokovu upatikane. Kwa sababu hiyo huwezi kupata wokovu pasipokumuamini Mungu na Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.

Siyo kila mtu anayemjua Mungu na Yesu Kristo, anamuamini Mungu na Yesu Kristo. Na siyo kila anayemuamini Mungu anamuamini na Yesu Kristo. Na ndiyo sababu siyo wanadamu wote tunaolisikia neno la Mungu tumeokoka.

Kwa sababu hiyo, ni lazima mtu aamini kuwa Mungu yupo, anaishi milele, Yesu Kristo ni mwana wa Mungu (Mathayo 16:16, Luka 1:35), aliyekufa msalabani na kufufuka ili atuokoe (Mathayo 26:28).
Na siyo kuamini tu Mungu yupo, ni lazima ijulikane kuwa Mungu unayemuamini ni Yehova (ndilo Jina lake), tena anaishi milele. Ninasema hivi kwa sababu, hata wanaoabudu sanamu, wanyama au miti mikubwa nao pia wana Imani kuwa hivyo vitu wanavyoviabudu ndiyo miungu yao.

(b). kuokoka
Kuokoka ni kuamini kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kukiri kwa kinywa imani hiyo na kubadilika kutoka kuishi maisha ya dhambi na kuishi maisha matakatifu ya kupendeza Mungu.

Kwa maana hiyo, imani peke yake haitoshi kumpa mtu wokovu, ni lazima aikiri imani hiyo kwa maneno ya kinywa chake pasipo kulazimishwa au kushawishiwa (Warumi 10:9)

Haitakiwi mtu apate wokovu kwa kulazimishwa au kushawishiwa; kwa mfano mtu anaamua kuokoka ili amuoe au aolewe na mtu fulani aliyeokoka. Wengi wa watu wa aina hii hawawezi kuukulia wokovu kwa viwango vinavyostahili, kwa sababu hawakuokoka ili kumpokea Yesu Kristo bali waliokoka ili wampate mtu fulani. Wengi wao wanakuwa na wokovu wa kifafa.

(c). Hatua za kuokoka
(i). kuisikia injili ya Yesu Kristo
Ni lazima uisikie injili ya Yesu Kristo kwanza ili upate kumjua Mungu na Yesu Kristo kisha ujenge Imani itakayo kupelekea kuupata wokovu (1 Petro 1:23, Marko 16:15-16).

(ii). Kuamini
Baada ya kuisikia injili, kinachofuata ni kujenga imani ya ile injili uliyoisikia (Wagalatia 3:26). Na hapa ndipo penye tatizo, kama umeisikia imani potofu basi utakuwa ukiamini na kuabudu watu, vitu, wanyama; vitu visivyo Mungu wa kweli aliye hai. 

Kwa sababu hiyo, kabla ya kuamini ni vema ukachunguza ni Mungu yupi anayehubiriwa hapo, siyo kila mungu anayehubiriwa anastahili kuabudiwa. Ni Mungu mmoja tu ndiye anayestahili kuabudiwa, jina lake Yehova ambaye kupitia Yesu Kristo tunapata wokovu na uzima wa milele.

(iii). Kuokoka
Baada ya kuisikia injili ya Yesu Kristo, unapata Imani ya injili uliyoisikia, hatua inayofuata ni kuokoka kwa kuikiri imani uliyoisikia na kufanyika mwanafunzi wa Yesu Kristo ukiacha njia zote ovu na kufuata njia ya haki kama lisemavyo neno la Mungu (Warumi 10:10).

(d). Imani ni lazima ikue au iongezeke
Baada ya kuamini na kupokea wokovu, hutakiwi kubaki pale pale kama jinsi siku ya kwanza ulipoamini na kuokoka ulivyokuwa. Unatakiwa kuilinda imani na wokovu wako, na imani yako ni lazima ikue au iongezeke, kutoka kiwango hadi kiwango, kutoka chini kupanda juu (2 Korintho 10:15 na 2 Thesalonike 1:3).

Mpendwa msomaji wangu ni imani yangu kuwa kuna kitu kipya Roho Mtakatifu amekufundisha, usikose sehemu ya pili ya somo hili. Mungu akubariki sana, na akubariki zaidi kwa kushiriki na wengine masomo haya. Amina. 

1 comment:

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts