Wednesday, April 16, 2014

KUFANYIKA RAFIKI WA MUNGU

Bwana Yesu Asifiwe mpendwa msomaji wangu, karibu tumalizie somo letu. nina imani Mungu atakufundisha kitu kipya. Karibu.



Yohana 1:12. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio Jina lake”.

Katika mstari huo juu, tunajifunza vitu vikubwa viwili kulingana na somo letu. Moja, kufanyika watoto wa Mungu. Pili, kuliamini Jina la Yesu Kristo au kumuamini Yesu Kristo. Kumbuka somo letu linasema “kuukulia wokovu na neema ya Mungu”, katika somo la kwanza tuliona namna ya kumuamini Mungu (Yehova) na Yesu Kristo. Kupitia imani hiyo ndipo tunapata haki ya wokovu.



Kwa maana hiyo, tunapoamini na kupata wokovu tunafanywa kuwa wana wa Mungu aliye hai (Yehova). 

Kuwa mtoto wa tajiri na kuwa mtoto wa tajiri na wakati huo huo rafiki wa moyoni ni vitu viwili tofauti na kuna faida tofauti. Utanielewa baada ya vifungu vifuatavyo vya Biblia.

Isaya 41:8. “Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu (Mungu)”

Yakobo 2:23.”Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu

Katika mstari wa kwanza tumejifunza kuwa ukimwamini Mungu na Yesu Kristo unafanyika mtoto wa Mungu, lakini katika mistari miwili ya hapo juu tunaona kuwa kuna watu ambao Mungu anawaita rafiki zake.

Hata wewe leo hiii ukiamua kuendelea mbele zaidi na uhusiano wako na Mungu kutoka kuwa mtoto wa Mungu hadi kufikia kuwa rafiki wa Mungu, INAWEZEKANA, hebu tuangalie mstari ufuatao kwa uthibitisho;

Yohana 15:14. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo”.

Kwa hiyo katika mstari huo hapo juu tunaona jinsi Yesu Kristo anavyokiri kuwa kuna watu wanaoweza kuwa rafiki wa Mungu. Lakini ipo gharama katika kuwa rafiki wa Mungu, gharama hiyo ni kutenda kila Mungu analokuamuru kulitenda pasipo kuchagua.

Na, kufanyika rafiki wa dunia ni kufanyika adui wa Mungu. Kutenda kwa kufuatisha namna na mwenendo wa dunia unaopendeza na kuvutia macho ambao ndani yake kuna udhalimu ni kujifanya rafiki na dunia. Na kwa njia hiyo (kuwa rafiki wa dunia) tunajiondolea haki na nafasi ya kuwa rafiki wa Mungu (Yakobo 4:4, Warumi 8:7)

Kuna faida katika kuwa mtoto na rafiki wa Mungu, kumbuka mfano wangu wa kwanza. Ukiwa mtoto na rafiki wa Mungu, Mungu hatakuficha kitu (Yohana 15:15).

Kumbuka, Mungu alipowatuma Malaika kuiharibu miji ya Sodoma na Gomora; wale Malaika walipokelewa na Ibrahimu na Lutu. Lakini Mungu alimfunulia siri hiyo Ibrahimu kwanza, ni kwa sababu Ibrahimu alikuwa rafiki wa Mungu (Mwanzo 18:17).

Katika kumalizia somo letu lenye kichwa “HATUA ZA KUUKULIA WOKOVU NA NEEMA YA MUNGU”, tunamalizia na HATUA YA KUFANYIKA RAFIKI WA MUNGU.

KUDOWNLOAD PDF YA SOMO LOTE, BONYEZA HAPA

KUMPOKEA YESU KRISTO KUWA BWANA NA MWOKOZI WAKO, BONYEZA HAPA

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts