Tuesday, February 20, 2018

MPANGO KAZI WA KIBIBLIA WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAISHA

Nakusalimu mpenzi msomaji wangu, Jina la Yesu Kristo lisifiwe.

Leo napenda kuanza na hadithi kwa ufupi sana,
Ninaishi katika jamii ya wafugaji ambao hutegemea malisho ya mifugo yao; ng’ombe, mbuzi na kondoo katika majani yaotayo kondeni na vichakani. Wengi wa wafugaji hawa wanamiliki idadi kubwa ya mifugo, hivyo huwalazimu kutoka na mifugo yao kila siku kwenda kutafuta malisho na maji. Vijana wa kiume wa umri wa kati, huamka mapema asubuhi, hutoa mifugo katika mazizi yao, huiswaga na kuiongoza mifugo hii sehemu yalipo malisho mazuri na maji. Kila ifikapo jioni, hufanya kama walivyofanya asubuhi, huiswaga na kuiongoza mifugo yao kuirudisha mazizini mwao. Wafugaji hawa wanaotembea na mifugo yao kwa lengo la kutafuta malisho na maji huitwa wachungaji.

Wachungaji hawa hukaa nyuma na kuitanguliza mifugo yao mbele kwa lengo la kuweza kuiangalia isitawanyike na kufanya uharibifu wa mazao na mazingira wawapo njiani kuelekea malishoni ama kurudi mazizini. Katika kundi la mifugo isiyopungua hamsini, mifugo iliyotangulia mbele huchoka kutokana na safari ya mwendo mrefu kwenda na kurudi kutafuta malisho, hivyo hupunguza mwendo kasi wa kutembea. Mifugo iliyotangulia mbele ikipunguza mwende kasi wa kutembea, huilazimu mifugo yote inayofuata pamoja na mchungaji kupunguza mwendo kasi. Mara tu mwendo kasi wa kutembea unapopungua mchungaji huichapa mifugo iliyo karibu naye, mifugo ya nyuma, ili iweze kuongeza mwendo pasipo kujali kuwa mifugo iliyo mbele ndiyo inayopunguza mwendo hivyo basi mifugo ya mbele ndiyo ilistahili kuchapwa. 

Mifugo ya nyuma iliyochapwa huanza kukimbia na kuisukuma mifugo ya mbele, ambayo hukumbuka, kumbe tumepunguza mwendo, na kuanza kukimbia pia ili kuongeza mwendo. Mifugo ya mbele inajisahau kutunza mwendo kasi, inaanza kutembea taratibu, ili kukumbushwa kuongeza mwendo kasi, inachapwa mifugo ya nyuma ambayo siyo sababu ya kupungua kwa mwendo kasi. Mara baada ya kuchapwa, huikumbusha mifugo ya mbele kuongeza mwendo kasi, na mara mwendo kasi unaongezeka. Hayo ndiyo maisha ya kila siku ya mifugo inayobaki nyuma katika msafara wa kwenda ama kurudi malishoni. Hupokea kipigo kisicho na sababu. 

Tujifunze nini katika hadithi ya leo? Hadithi ya leo inatufundisha mambo makubwa matatu; 1. Changamoto ni lazima 2. Usilalamikie changamoto 3. Kabiliana na changamoto. 


Changamoto ni lazima
Mpenzi msomaji ninapenda kukujulisha kuwa, katika maisha ili mradi upo hai unaishi, huna budi kukutana na changamoto katika hatua moja ama nyingine ya maisha yako. Ni lazima ukutane na changamoto, kwa kusababisha mwenyewe ama kwa kusababishiwa. Ndiyo, zipo changamoto tunazipitia kwa sababu tu kwa namna moja ama nyingine tumezisababisha wenyewe. Pia zipo changamoto ambazo zinatupata katika maisha kama matokeo ya makosa ya watu wengine. Katika hadithi yetu, ng’ombe waliopo nyuma wanachapwa kwa sababu ya kutembea taratibu lakini wanaosababisha mwendo wa taratibu ni ng’ombe waliopo mbele. Je, changamoto ni nini? Changamoto ni hali yoyote ya kiuchumi, kijamii, kimahusiano ama kielimu inayokuwekea kizuizi cha kusonga mbele na mara zote kizuizi hiki huumiza na huweza kukufanya ukate tamaa na kujiona haustahili. 

Usilalamikie changamoto
Unapokumbwa na changamoto ya aina yoyote ile, usilalamike, kulalamikia changamoto ni sumu kali sana katika maisha. Kumbuka hadithi yetu, ng’ombe wa nyuma wanapochapwa kwa kosa la ng’ombe wa mbele kutembea taratibu, hawamgeukii mchungaji na kuanza kumlaumi kwa kuwachapa kwa kosa lisilo lao. Unaporuhusu kuilalamikia changamoto iliyokukabili kwa sababu imesababishwa na mtu mwingine (unajiona umeonewa, haukustahili), unapoteza uwezo na nguvu za kuitatua. Ukiisha kupoteza uwezo na nguvu za kutatua changamoto inayokukabili, unakuwa si mshindi tenda dhidi ya changamoto hiyo. Hatua inayoufuata ni KUKATA TAMAA. Ukikata tama, unapoteza muelekeo na mustakabali mzima wa maisha yako.

Kabiliana na changamoto inayokukabili
Dawa ya changamoto yoyote ile inapokukabili, ni kukabiliana nayo kwa lengo moja kubwa, kuitatua na kuimaliza kabisa. Katika hadithi yetu tunaona ng’ombe walio nyuma (wasiopungua watatu hadi watano) wanapochapwa hukimbia kusonga mbele kulikabili kundi kubwa la ng’ombe (kuanzia hamsini) waliopo mbele yao na kuwafanya waanze kukimbia ili kuongeza mwendo kama atakavyo mchungaji. Mchungaji ni sawa na maisha, siku zote maisha yanataka mchaka mchaka, wewe ni sawa na ng’ombe aliyeko nyuma, changamoto za maisha ni ng’ombe waliopo mbele. Maisha yanapokupa changamoto, kabiliana nazo ili uzitatue. Jambo la muhimu, usiache changamoto haijamalizika kutatuliwa. Ni kosa kubwa sana.

Mpango kazi wa kutatua changamoto
Sasa tuangalie mpango kazi wa Kibiblia wa kukabiliana na kutatua changamoto. Rejea mistari michache ya Biblia katika kitabu cha Luka 9:10-17. Wafuasi wa Yesu Kristo walipompelekea habari ya kuwaruhusu waondoke wale makutano, walikuwa wanafanya kitu kifuatacho, kuwasilisha changamoto (watu wanaozidi 5000 nyikani pasipo chakula) inayomkabili Yesu pamoja na ufumbuzi wa hiyo changamoto (kuwaruhusu waende vijiji vya jirani kutafuta chakula). Ufumbuzi waliouwasilisha wafuasi wa Yesu haukuwa sahihi, endapo Yesu angewaruhusu makutano wale kwenda vijiji vya jirani majira ya jioni kuelekea usiku wangeumia njiani na wengine wangezimia kwa safari ndefu ya kwenda kutafuta chakula wakiwa na njaa kali.
Katika masimulizi hayo tunajifunza mambo makuu matatu kutoka kwa Yesu Kristo; 1. Utulivu 2. Kushukuru 3. Kukabili na kutatua changamoto.

Utulivu
Yesu Kristo alipopokea changamoto yake hakuifanya kuwa habari ya mjini, masimulizi na malalamiko kwa kila aliyekutana naye. Hili ni kosa ambalo wengi tunalifanya, tunapopatwa na changamoto tuanza kuilalamikia huku tukiifanya ni habari ya mjini kuitangaza katika kila mbao za matangazo tunazokutana nazo. Jifunze kwa Yesu, unapopatwa na changamoto tuliza moyo na akili, endapo utaona huwezi (unahisi kuchanganyikiwa), jipe nafasi ya utulivu huku ukitafari mambo mengine yasiyohusiana kabisa na changamoto inayokukabili. Jaribu kufanya mambo yatakayo kufariji na kukupa furaha kwa wakati huo hadi pale utakapojiona upo tayari kuikabili na kuitatua changamoto iliyopo mbele yako. Kujipa muda ili upate utulivu wa moyo na akili ili kuikabili changamoto yako kunakupa nguvu na uwezo wa kufiriki njia sahihi ya utatuzi ili kuimaliza kabisa changamoto iliyopo mbele yako. Endapo utathubutu kutatua changamoto yoyote katika hali ya hofu na mashaka (pasipo utulivu), matokeo ya utatuzi huo hayatakuwa sahihi wala ya kudumu. 

Kushukuru
Kuna nyakati tunajipata uwezo wetu wa kutatua changamoto zetu ni mdogo kuliko ukubwa wa changamoto, nyakati kama hizi tunapaswa kushukuru Mungu kwa kuachilia changamoto zitupate. Usilaumu, usimlaumu Mungu kamwe kwa changamoto inayokukabili. Hakuna changamoto inayompata mtu kamwe kwa lengo la kumuangamiza, changamoto itakuangamiza endapo tu utanzaa kulaumu, utajiona hufai, utajiona hukustahili na utamua kukata tama. Lengo la changamoto pasipokujali inatupata kwa namna gani, ni kutufundisha na kutuimarisha. Na ndiyo maana kuna misemo mingi sana, kwa mfano msemo mmoja wa Kiswahili unasema, “ukimuona nyani mzee ujue amekwepa mishale mingi sana”, upo msemo mwingine wa Kiingereza usemao, “experience makes perfection”. Unapomshukuru Mungu, unamfanya ashughulikie changamoto yako yeye mwenyewe, ama kwa kukupa njia sahihi au mtu sahihi kwa ufumbuzi wa changamoto hiyo. Kumbuka Biblia haisemi Yesu Kristo alipowashika wale samaki watano na mikate miwili (ni zaidi ya utani kuwa na samaki wawili na mikate mitano kama chakula cha watu wanaozidi elfu tano) mikononi mwake alianza kuombea waongezeke ili watoshe idadi ya watu. La hasha, Yesu Kristo alishukuru, Mungu akaongeza samaki na mikate ili itosheleze idadi ya makutano na kusaza. 

Kukabili na kutatua changamoto
Yesu Kristo aliamuru wafuasi wake wafanye mambo mawili; kuwakalisha chini makutano na kuwagawanya makutano katika makundi ya watu wachache wachache. Kuwakalisha chini makutano maana yake ni kuliweka tatizo au changamoto (makutano) chini ya mamlaka na uwezo wake. Unapoiweka changamoto chini ya mamlaka na imaya yako (kwa njia ya maombi na kushukuru), unaifanya ionekano ndogo kuliko uwezo na nguvu zako, hii itakusaidia katika kuikabili hiyo changamoto pasipo woga. Ziambie changamoto zako, Mungu wako ni mkubwa kuliko zenyewe. Yesu Kristo alipowagawanya makutano katika makundi alikuwa anatatua changamoto kwa hatua. Kamwe huwezi kutatua changamoto yoyote ile pasipo kuimega kidogo kidogo hadi inaisha. Ukilazimisha kutatua changamoto yako kwa mara moja, kuna sehemu kutakudai kutatua badae, hutaweza kuimaliza. Kwa namna nyingine unapopatwa na changamoto angalia palipo rahisi ndipo anza napo hapo. Kwa mfano, mwanafunzi unamaliza kidato cha sita, hujafanya vizuri katika mtihani kuweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu kutimiza ndoto yako ya kupata digrii uipendayo, badala ya kukata tamaa na kukaa nyumbani kuanza tabia hatarishi zinazoweza kuharibu kabisa maisha yako, unaweza kuamua kusoma kwanza diploma ya fani ile uipendayo, baada ya kumaliza hiyo diploma unapata sifa ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu kupata digrii ya ndoto yako.

Mwenyezi Mungu akubariki sana msomaji wangu. Ni maombi yangu kuwa Mungu akuongoze kwa kila changamoto unayopitia ili utoke kwa ushindi. Amina.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts