Mathayo 22:37-38 “…Mpende Bwana
Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
Hii ndiyo amri iliyo kuu tena ni ya kwanza.”
Katika Biblia habari hii inaanza baada ya Yesu Kristo
kuulizwa swali la kujaribiwa na mmoja katika Mafarisayo, ambao walikuwa
wanaijua torati kamili ya manabii kwa habari ya sheria na amri zake.
Walimuuliza swali wakimjaribu ili awaambie ni amri ipi iliyokuu katika torati,
na ndipo Bwana Yesu akawapa jibu tofauti na walilolitegemea. Akawaambia, Mpende
Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako
zote. Kibinadamu jibu hili ni kama halina mantiki yoyote na limekaa kimzaha
zaidi, kwani hakuna mtu asiyempenda Mungu wake.
Lakini ukitazama kiundani zaidi, na kama utapata msaada wa
Roho Mtakatifu utagundua kuwa jibu hili linatuhusu na kugusa imani zetu moja
kwa moja na siyo wale Mafarisayo tu. Labda tuangalie na kuchambua maana ya
vipengere vikubwa vitatu katika mstari wa 37 wa kitabu hicho cha injili.
Kwa moyo wako wote. Neno kwa moyo wako wote linamaanisha
kukipa sehemu yote ya moyo wako kitu unachokipenda. Kama umeamua kukipenda kitu
fulani, basi ukipende kwa kumaanisha, usikichanganye na kitu kingine. Wala
usiwe na mbadala wa hicho unachokipenda.
Kwa roho yako yote, ni kuamua kujitoa hata maisha yako kwa
ajili ya hicho unacho kipenda. Kutokuyathamini maisha yako zaidi ya
unachokipenda. Sehemu nyingine neno la Mungu linasema atakaye kunifuata na
ajikane mwenyewe, sasa kumpenda Mungu kwa roho yote ni kujikana nafsi yako.
Kwa akili zako zote, ni kumfanya Mungu achukue sehemu kubwa
ya mawazo yako pasipo kujari sehemu ama wakati uliopo. Kuna watu wakiwa na
wapendwa nao ni wapendwa, wakiwa mbali na wapendwa basin a upendwa wao
wanauvua.
Kuamua kumpenda Mungu kwa moyo wote, na roho yote, na akili
zote, ni kumpenda Mungu pasipo kumchanganya na dhambi, kumpenda Mungu kwa
kujikana nafsi zetu na kumpenda Mungu kwa mawazo yetu.
Kuna watu wanawapenda wanandoa wao zaidi ya kumpenda Mungu,
wanawapa sifa zinazozidi uzuri wa malaika lakini watu hao hao ukiwakuta kwenye
nyumba za ibada wakati wa kipindi cha kumsifu Mungu unawedha ukadhani ni
wagonjwa. Na wapo watu wanaowapenda wanadamu kwa roho zao zote kiasi cha
kuzirai wakipewa taarifa za vifo vyao lakini kumpenda Mungu hakumo ndani yao.
Na wapo watu ambao wanajikana nafsi zao kwa ajili ya watu wengine au mambo
mengine. Watu hawa watakwambia hawana muda wa kuhudhuria nyumba za ibada kwa
kisingizio cha maisha yanabana au shule ngumu lakini ni mabingwa wa kutenga
muda wa kwenda klabu na kumbi mbali mbali za starehe na marafiki lakini muda wa
kuongea na Mungu wao hawana.
Kuna aina ya maisha ambayo ni kusudi la shetani moja kwa
moja, kama kutoa muda wako mwingi katika vipindi vya televisheni, kusoma vitabu
vya hadithi na magazeti, kufanya kazi hadi za “over time”. Lakini linapofika
suala la kujitoa kwa Mungu anaye kupa uhai bure, unajibu uko “busy”, hata
kusoma biblia yako ni hadi jumapili kanisani, na usomaji wenyewe ni ule wa
kufuatisha neno la mhubiri wa siku hiyo.
Hatuna budi kuyatafakari maisha tunayo ishi kuwa ni maisha ya namna ama
aina gani, je tunampa Mungu kipaumbele anachostahili katika maisha yetu ya kila
siku? Mpenzi msomaji, hebu jiulize swali hilo je mfumo wako wa maisha unampa
Mungu kipaumbele anachostahili? Na kama jibu ni ndiyo basi Mungu akuzidishe
zaidi, na ikiwa jibu ni siyo basi Mungu akusaidie ili umpe nafsi yake
anayostahili katika maisha yako.
Kama tunavyo oona katika mstari ule wa 38 wa injili hii,
Yesu aliwajibu wale Mafarisayo kuwa amri hii ndiyo kuu tena ni ya kwanza.
Kuvunja amri kuu ni kutenda kosa kuu.