Sunday, September 1, 2019

UTATU MTAKATIFU WA MUNGU (MUNGU BABA, MUNGU MWANA NA ROHO MTAKATIFU)


UTANGULIZI

UTATU MTAKATIFU WA MUNGU (THE HOLY TRINITY OF GOD)

Mungu ni nani?
Mungu ni Roho takatifu aliyekuwapo milele iliyopita, aliyepo sasa na atakayekuwapo milele ijayo (Yohana 4:24, 2 Wakorintho 3:17). Mungu hana mwili wa damu na nyama kama tulivyo viumbe wengine na hana maumbo ya vitu asili visivyo hai kama milima mikubwa. Mara nyingi Mungu alipojidhihirisha kwa wanadamu, alijidhihirisha kwa sauti peke (Mwanzo 3, Isaya 6:8, Kutoka 19:9) na mara chache Mungu alijidhihirisha kwa uwazi kabisa kwa mtumishi wake Musa (Kutoka 33:18-23). Ijapokuwa Musa hakuwahi kuiona sura ya Mungu (alipata kibari cha kukiona kivuli cha Mungu katika maumbo ya moto), kwa sababu Mungu ni Roho yenye utukufu mwingi, hakuna mwanadamu atakayemuona Mungu kwa macho ya damu na nyama akaishi (Kutoka 33:20, Yohana 1:18).

Sifa kuu tatu (3) za Mungu
Omniscient
Neno hili linatokana na neno “omniscience” neno linalomaanisha “ufahamu”. Mungu ni “omniscient”, ikimaanisha ni mwenye ufahamu wa elimu zote. Mungu ni Roho anayejua kila elimu na kamwe hakuna jambo jipya kwake ama analohitaji kujifunza. Ni Mungu anayeujua mwisho wa kitu au jambo (mfano, uhai wa mwanadamu) kabla ya mwanzo wa kitu au jambo husika (Isaya 46:10, Yeremia 10:12). Maarifa na hekima yote ya wanadamu wote wa dunia hii ni sawa na upumbavu tu kwa Mungu (1 Wakorintho 1:25) kwa sababu kiwango chake cha ufahamu ni juu mno.

Omnipotent
Neno “omnipotent” linatokana na neno “omnipotence” linalomaanisha kuwa na nguvu ama uwezo uliovuka mipaka ya vipimo ama akili za kibinadamu. Hivyo basi Mungu ni Roho yenye uwezo usio na mipaka (kizuizi) katika kutenda jambo lolote. Naweza kusema, “Mungu ni nguvu na nguvu ni Mungu”. Soma Biblia yako vifungu vifuatavyo, Kumbukumbu la Torati 3:24, Zaburi 62:11, Ayubu 26:14, Ayubu 9:4, Yeremia 10:12. Hakuna nguvu iliyowahi kuwashinda wanadamu ilimshinda Mungu, kumbuka mfano mdogo tu, gharika/vimbunga vyote (mvua za vimbunga) zinazotokea duniani kote hazijawahi kuzuiliwa na wanadamu zisifanye madhara zaidi ya wanadamu kuzikimbia gharika/vimbunga hivyo. Kwa sababu mvua hizo zina nguvu inayozidi uwezo wa wanadamu na fahamu zao zote. Lakini Mungu (Yesu Kristo) alipokutana na dhoruba ya bahari aliikemea nayo ikatii na kukawa na utulivu mkubwa (Matayo 8:26). Hii inadhihirisha uwezo na nguvu za Mungu namna zilivyo kuu pasipo na mipaka ama ukomo wa utendaji kama wanadamu. 

Omnipresent
Neno hili linatokana na neno “omnipresence” lenye maana ya uwepo katika sehemu zote kwa wakati wote/mmoja (ule ule). Mungu ni Roho iliyopo sehemu zote katika wakati ule ule, yaani wakati huu unaposoma mafundisho haya, Mungu yupo mahali hapo ulipo, yupo mahali alipo muandishi wa somo hili, yupo nchi zote za dunia hii. Hivyo ndivyo Mungu alivyo, Mungu asiye na chanzo au asili wala mwisho (Ufunuo 1:8, Zaburi 139:7-12, Yeremia 23:24). 

Sifa hizo kuu za Mungu aliye hai, ambaye jina lake ni Jehova hakuna mungu mwingine yoyote anayeweza kuwa nazo. Ni ajabu sana kuona baadhi ya watu wanaabudu miungu mfano wa wanyama ama miti mikubwa ama milima mirefu. Ni ajabu zaidi kuona mwanadamu anaabudu hata kinyago alichokitengeneza yeye mwenyewe. Nikusihi mpenzi msomaji wangu, yupo Mungu mmoja tu wa kuabudiwa, anaitwa Yehova na ndiye Mungu ninayemuhubiri kupitia jina la Yesu Kristo aliye hai. 

MUNGU MMOJA, NAFSI TATU (UTATU MTAKATIFU WA MUNGU)
Nafsi ni nini?
Kabla ya kuendelea kumjua Mungu katika nafasi tatu anazochukua yaani nafsi tatu ambazo ni Mungu Baba, Mungu mwana na Roho Mtakatifu, hebu tuangalie nini maana ya nafsi? Kwa lugha ya kigeni, neno nafsi linajulikana kama “soul’ wakati neno roho linajulikana kama “spirit”. Mungu ni Roho na wakati huo huo ni Nafsi tatu ndani ya Roho moja. Tofauti na mwanadamu ambaye ana roho, nafsi na mwili, Mungu hana mwili wa nyama na damu kama hii tuliyonayo sisi wanadamu au viumbe wengine mfano wanyama. 

Nafsi ni hisia au matamanio yanayoongoza matendo au tabia za mwili. Kwa maana nyingine, nafsi ni hisia au matamanio yanayoamua ubinadamu wa mtu. Nafsi za wanadamu zinaishi kwa kufuata matamanio ya vitu vionekanavyo kwa macho hapa duniani. Na ndio sababu mwanadamu anayeishi kwa kufuata tamaa za nafsi yake kamwe hawezi kumpendeza Mungu. Hata hivyo, roho ya mwanadamu inaishi kumpendeza Mungu ikishindana na nafsi. Hadi pale mwanadamu anapopokea neema ya kuongozwa na Roho Mtakatifu ndipo roho yake itaweza kuishinda nafsi na hivyo kuisha maisha ya kumpendeza Mungu. 

Kwa hiyo, matendo ya Mungu yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo yanatufanya tumuone Mungu mmoja ndani ya nafsi tatu. Matendo hayo ndiyo tabia za Mungu. Hebu tuangalie tabia au matendo hayo ya Mungu katika nafsi tatu.

Mungu Baba
Roho ya Mungu inaopochukua tabia ya uumbaji (kuzaliwa jambo jipya kimwili/kimaumbile au kiroho), inachukua nafsi ijulikanayo kama Mungu Baba. Katika uumbaji wa viumbe vyote tunavyoweza kuviona kwa macho yetu na hata vile tusivyoweza kuviona ambavyo vina udogo usioweza kuonekana kwa macho mfano wa vimelea vya bakteria, hapa Mungu anaitwa Mungu Baba (mzazi). Mzazi ni chanzo au asili ya maisha ya ina fulani. Soma Bibli yako katika vifungu vifuatavyo; Mwanzo 1:1, Wakolosai 1:16. Mungu katika nafasi ya uumbaji wa ulimwengu wote na kuwa chanzo ama asili ya aina zote za maisha/uhai anachukua nafsi ya Mungu Baba. Na kwa namna hiyo, muimbaji mmoja (Don Moen) alipompima Mungu katika nafasi hiyo akamuita Jina la “Creator King”, hakika jina hili ni tamu ulimini, nafsini na hata rohoni. 

Mungu Mwana
Kulitokea vipindi viwili vya maangamizo makuu, ambavyo Mungu aliamua kuwaangamiza wanadamu kutokana na kuongezeka kwa maasi katika dunia. Vipindi hivyo ni wakati wa gharika ya Nuhu (Mwanzo 6, Mwanzo 7) na wakati wa Sodoma na Gomora (Mwanzo 19). Licha ya maangamizo hayo, bado wanadamu waliendelea kutenda dhambi. Siyo kwa sababu wanadamu wanapenda sana dhambi, la hasha, ni kwa sababu nafsi ya mwanadamu inavutwa na matamanio ya kuipendeza dunia na siyo Mungu. Kwa sababu hiyo Mungu akaonelea atafute namna ya kutusaidia wanadamu ili tuweze kuushinda ulimwengu (dhambi) na tuishi maisha ya kumpendeza (Mwanzo 9:11). 

Hivyo basi, Mungu akachukua mwili wa udhaifu (mwili wa damu na nyama), akazaliwa na bikira Maria kwa makusudi maalumu ya kuachilia neema ya ukombozi kwa mwanadamu aliyepotea dhambini (Mathayo 1:18-20). Mateso yote aliyoyapitia Yesu Kristo; kukamatwa kama mwizi, kupigwa na kuchapwa mijeredi kama muhalifu, dhihaka za kutemewa mate na kutukanwa, maumivu ya kuubeba msalaba mzito (msalaba unaokadiriwa kuwa na uzito usiopungua kilogram 135) juu ya mwili uliodhohofu na kuchakaa kwa mateso ya usiku kucha na asubuhi yote, maumivu ya misumali iliyoubeba mwili juu ya msalaba na taji ya miiba kichwani….hakika Bwana wetu Yesu Kristo alivumilia sana pasipo kutoa neno la lawama. Mateso hayo yalipaswa tuyachukue kila mmoja wetu ili kulipia thamani ya ukombozi wetu kutoka ufalme wa giza (ufalme wa shetani) na kuandikishwa katika ufalme wa nuru (Ufalme wa Mungu), soma Biblia yako katika kitabu cha Isaya 53. Huu ni upendo wa ajabu kabisa, Mungu kuvaa udhaifu na kupokea mateso (kwa nafasi zetu) ili sisi wenye dhambi tukombolewe kwa neema na siyo kwa mapigo ya gharika ya maji au moto wa Sodoma na Gomora. 

Katika sura hii ya upendo kwa mwadamu, Mungu anapokea tabia ya nafsi iitwayo Mungu katika nafsi ya pili yaani Mungu Mwana. Tofauti na wanadamu, Mungu hahesabu maovu tuliyomtendea ili atusamehe. Anatusamehe wote sawa, dhambi kubwa ama ndogo, nyingi ama chache (kwa kipimo cha mwanadamu), Mungu aliyehai, Yehova anatusamehe zote, wote, sawa. Hakuna anayesamehewa dhambi nusu na mwingine zote, wote tunasamehewa dhambi zote kwa kila mmoja na wingi wa dhambi zake na ukubwa wa dhambi zake, akiisha tutakasa anatufanya watoto wake na warithi pamoja naye (Warumi 8:16-17). 

Mungu Roho Mtakatifu
Mungu yule yule katika nafsi ya tatu, anajulikana kama Mungu Roho Mtakatifu. Kama tulivyoona hapo juu, mwanadamu ameumbiwa roho (inayotenda kutimiza mapenzi ya Mungu) na nafsi (inayovutwa na tamaa za dunia ili kutimiza mapenzi ya mwili). Nafsi ya mwanadamu kamwe haiwezi kushinda tamaa za mwili kuipendeza dunia, kwa namna yoyote ile mwili wa mwanadamu utatenda dhambi na kumchukiza Mungu. Hiyo ni nguvu ya nafsi kutimiza matamanio ya mwili yenye dhambi. Na huu ni udhaifu wa kila mwanadamu. Ndipo Mungu anaamua kutukamilisha ili tuzishinde nafsi zetu na kuisha maisha ya kumpendeza katika uchaji wa dhati usio na mawaa (Warumi 8:26-28, Wagalatia 4:6-7, na 1 Yohana 3:24).

Vivyo hivyo, Mungu analihudumia kanisa lake kama ahadi ya Yesu Kristo ya kutotuacha yatima (Yohana 14:16). Kupitia huduma mbalimbali zinazoongozwa na Roho Mtakatifu ndani ya kanisa (Warumi 12:1-8, 1 Wakorintho 12:1-11), Mungu anaendelea kutufundisha kumjua, kumtumikia na kumuishia yeye ili tupate ukamilifu katika imani na kuweza kusimama imara kama mashahidi wa haki tukiushuhudia ukombozi wa Yesu Kristo kwa wenye dhambi ulimwenguni kote (Yohana 14:26, Yohana 15:26).  

HITIMISHO
Mungu ni Roho takatifu anayeishi milele na ndiyo chanzo na asili ya ulimwengu wote na aina zote za maisha (viumbe) ndani ya ulimwengu. Mungu anatenda kazi kupitia nafsi tatu ambazo ni Mungu Baba, Mungu Mwanza (Yesu Kristo) na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu anawapenda wenye dhambi, anawakomboa kutoka utumwa wa shetani na kuwarejesha katika ufalme wake kupitia Mungu Mwana. Kwa sababu ya udhaifu wa nafsi ya mwanadamu katika kuipenda dunia na anasa zake, Mungu anatutia nguvu za kuushinda ulimwengu kupitia Roho Mtakatifu.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts