YESU KRISTO ASIFIWE!
Mpendwa msomaji wangu karibu tena katika mwendelezo
wa somo letu lenye kichwa kisemacho “MAOMBI YENYE KIBALI NA NGUVU MBELE ZA
MUNGU”, ikiwa leo ni sehemu ya pili. Nina imani utazidi kubarikiwa zaidi na
somo hili, ikiwa ulikosa sehemu ya kwanza ya somo hili utaipata humu humu ndani
ya blog hii.
Leo tunaangalia aina kuu za maombi na faida zake, na
aina nyinginezo za maombi na faida zake. Ni matumaini yangu kwa msaada wa Roho
Mtakatifu utajifunza vyema na Mungu atakuwa pamoja nawe.
Aina kuu za maombi na faida zake.
Maombi kabla.
Haya ni maombi ambayo muhusika anaomba kabla
hajafikwa na jambo, kwa mfano unapoamua kuombea maisha yako ya badae, familia
(mke au mume na watoto) yako ya badae ilihali haujaoa au kuolewa. Unapofika
wakati huo, unashangaa mambo yanaenda vizuri, ni kwa sababu ulishaomba kabla.
Mathayo 26:41a. “Kesheni mwombe, msije mkaingia
majaribuni”.
Yesu mwenye anasema kesheni mwombe siyo muwapo majaribuni, bali
msije mkaingia majaribuni. Anamaanisha tuombe sasa, ili majaribu yajapo tusije
tukaingia kwayo, kwa hiyo anatuambia tuombe sasa kwa ajili ya maisha yetu ya
badae.
Waebrania 4:16. “Basi na tukikaribie kiti cha neema
kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa
mahitaji”.
Inawezekana kabisa kupata rehema na neema ya maisha na wakati wetu
ujao sasa, ili tunapoyafikia maisha yetu ya baadae au kupata mahitaji katika
wakati ujao tayari tunakuwa tumefunikwa na rehema na neema za Mungu na hivyo
kutufanya tusimame imara.
Faida ya maombi haya ni maombi yenye mafanikio sana,
kwa sababu muombaji huomba kwa ile imani aliyonayo mbele za Mungu kupitia jina
la Yesu Kristo. Hapa muombaji haombi kutokana na nguvu inayomsukuma kutoka nje,
bali huomba kwa sababu anamwamini Mungu na kumfanya Mungu kuwa ndiye tumaini
lake.
Maombi baada.
Haya ni maombi ambayo mwombaji huomba baada ya
kuingia katika jambo analoliombea. Yaani mwombaji anakuwa ameingia katika
shida, ndipo anamkumbuka Mungu tena baada ya njia nyingine zote kushindwa. Ina
maana, anakuwa na imani na vitu vingine tofauti na Mungu, vile vitu vinaposhindwa
ndipo anamtafuta Mungu.
Zaburi 69:1-2. “Ee Mungu uniokoke, maana maji
yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, pasipowezekana
kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi; mkondo wa maji unanigharikisha”.
Maombi haya siyo mazuri sana kama maombi kabla, kwa
sababu muombaji huomba kutokana na msukumo anaoupata kutoka na shida, tatizo au
hitaji alilonalo.
Maombi ya kawaida.
Ninaposema maombi ya kawaida ninamaanisha maombi
yasiyoambatana na kufunga (not fasting prayers). Maombi haya yana majibu pia,
hasa ukiyaambatanisha na imani na utakatifu na ukifuata vitu vya kuzingatia
uwapo katika maombi au kabla ya maombi.
Maombi ya kufunga (fasting prayers).
Haya ni maombi ambayo muombaji huamua kuingia katika
maombi pasipo kula au kunywa kwa kipindi cha muda maalumu. Kwa mfano
inawezekana kufunga kwa muda wa masaa 12, 24, 48 au 72, n.k ikitegemea ukubwa
na umuhimu wa kile unachokiombea.
Kufunga kunakufanya uoneshe ni jinsi gani una nia ya
dhati kuelekea kile unachokiombea, na kunamfanya Mungu akutegee sikio la
umakini zaidi na hivyo kuitimiza haja yako kwa wakati.
1 Wafalme 21:27-29. “Ikawa, Ahabu alipoyasikia
maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga,
akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole (mbele za Mungu). Neno la Bwana
likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu?
basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku
zake”.
Kwa njia ya maombi ya kufunga na ya unyenyekevu
mbele za Mungu, Mungu akaiondoa hasira yake mbele za mfalme Ahabu.
Aina nyingine za maombi.
Aina hizi za maombi zinaweza zikawa ndani ya aina
mojawapo au mbili ya aina za maombi nilizoziongelea hapo juu katika aina kuu za
maombi. Inaweza ikawa ni maombi kabla, au maombi kabla na ya kufunga ukiombea
maisha yako ya baadae au watoto wako Mungu atakaokupa.
Kwa mfano unaweza ukawa unafanya maombi ya kufunga na kufungua vifungo ambayo pia yakawa ni maombi kabla (unaombea maisha ya badae) halafu na ukawa umefunga, kwa hiyo hapo unakuwa umefanya maombi ambayo yamo ndani ya maombi makuu mawili; maombi kabla na maombi ya kufunga.
Kwa mfano unaweza ukawa unafanya maombi ya kufunga na kufungua vifungo ambayo pia yakawa ni maombi kabla (unaombea maisha ya badae) halafu na ukawa umefunga, kwa hiyo hapo unakuwa umefanya maombi ambayo yamo ndani ya maombi makuu mawili; maombi kabla na maombi ya kufunga.
Aina hizo nyingine za maombi ni kama zifuatazo:-
Maombi ya Roho Mtakatifu.
Waefeso 6:18. “kwa sala zote na maombi mkisali kila
wakati katika Roho, mkikesha katika jambo hilo na kudumu katika kuwaombea
watakatifu wote”.
Haya ni maombi ambayo muombaji anaomba akiwa amezama
rohoni, na Roho Mtakatifu ndiye anayehusika kuomba kwa ajili ya muombaji. Kwa
nini basi tuombe katika Roho, tuangalie kifungu cha Biblia hapa chini;
Warumi 8:26-27. “Kadhalika Roho naye hutusaidia
udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe
hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo, aijua nia
ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”.
Kuna sababu kubwa mbili za kutulazimu kuomba kwa
Roho; hatujui kuomba ipasavyo na Roho hutuombea kama apendavyo Mungu. Kwa hiyo
unaweza ukawa unafanya maombi ya Roho ukiombea maisha yako ya badae au familia
yako au upate kazi.
Maombi ya kufunga na kufungua.
Hapa ninaposema maombi ya kufunga na kufungua
simaanishi maombi ya kutokula wala kunywa, ni maombi ambayo mwombaji anatumia
mamlaka aliyopewa na Yesu Kristo kuvifungia au kuvifungua vitu fulani katika
maisha yake.
Mathayo 18:18. “Amini, nawaambieni, yo yote
mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni, na yo yote mtakayoyafungua
duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni”.
Kwa hiyo unaweza ukafunga kabisa magonjwa katika
maisha yako na hutaweza kuugua, ama unaweza ukafungua mifereji ya baraka za
rohoni na mwilini kwa watoto wako hakika watabarikiwa. Kanuni ni moja tu;
imani, kwa sababu Yesu mwenyewe amesema, “amini, nawaambieni”.
Unganisha utakatifu na vitu vingine vya kuzingatia
katika maombi, ukiwa umebeba imani hakika utamuona Mungu katika viwango vya juu
zaidi. Kwa hiyo unaweza ukawa unafanya maombi haya ukiyaambatanisha na maombi
kabla na maombi ya kufunga.
Maombi ya kusukuma.
Haya ni maombi ambayo muombaji hung’ang’ana na
kuomba hadi apokee majibu ya maombi yake, na mara nyingi waombaji wa maombi
haya huwa kuna jibu wanalokuwa wanalitegemea kutoka kwa Mungu, hivyo
hung’ang’ania kuomba hadi watakapolipata jibu hilo.
Luka 11:5-9. “Akawaambia, ni nani kwenu aliye na
rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, rafiki yangu nikopeshe mikate
mitatu kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, name sina kitu
cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, usinitaabishe, mlango
umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka
nikupe? Nawaambia ya kwamba ijapokuwa aondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake,
lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
Nami nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi
mtafunguliwa”.
Kabla hujaingia katika maombi haya ni vema
ukamuuliza Mungu nini makusudi yake, kwani unaweza ukang’ang’ana kuomba majibu
yasiyo yako, Mungu anaweza akawa amekukadilia mahali pa juu sana lakini kwa
kutojua ukaomba maombi haya ukiwa umejikadilia mahali pa chini mno. Siyo kwamba
Mungu hatakupa haki yako, utaopata lakini lazima uanzie kule ulikoomba ndipo
upande juu.
Aina hii ya maombi, nayo unaweza ukaiambatanisha na
mojawapo au zaidi ya aina zile kuu nne za maombi kutegemea na uhitaji wako.
Maombi kwa adui.
Hii ni aina ya maombi ambayo ni ngumu sana, na
Wakristo wengi huwa hawaombi maombi ya aina hii. Haya ni maombi ambapo mwombaji
huwaombea watesi na adui zake, huwaombea baraka, ushindi, mafanikio na
ikiwezekana hata kuomboleza kwa ajili yao ili Mungu awape rehema.
Mathayo 5:43-44 na 48. “Mmesikia kwamba imenenwa,
umpende jirani yako na umchukie adui yako, lakini mimi (Yesu Kristo) nawaambia,
wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama
Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Kuwaombea adui zetu, ni agizo la moja kwa moja
kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe. Lakini ni Wakristo wangapi leo wanaowaombea
adui zao? Na siyo tuwaombee laana, maisha mafupi, kukosa kibali, la hasha,
tumeagizwa kuwaombea Baraka. Hebu tuangalie kifungu cha Biblia kifuatacho:-
Warumi 12:14. “Wabarikini wanaowaudhi; barikini,
wala msilaani”.
Hapa neno la Mungu
halituagizi kubagua kwamba ni nani aliyetuudhi na awe amutuudhi nini, yeyote na
chochote alichotuudhi, tumeagizwa kumbariki.
Maombi ya ushirika.
Haya ni maombi ambayo wanajumuiya, au Wakristo wa
kanisa fulani wanashirikiana kwa umoja katika kuliombea jambo fulani; aidha
linahusu kanisa au linamuhusu mshirika mmoja.
Matendo ya Mitume 1:12-14. “kisha wakarudi kwenda
Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu,
wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia wakapanda orofani, walipokuwa
wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo
na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote
walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu
mama yake Yesu, na ndugu zake”.
Faida ya maombi haya ni kwamba, yanaonesha umoja na
ushirikianao wa kanisa au jumuiya na pia yana nguvu zaidi kuliko maombi ya mtu
mmoja. Siyo lazima ufanye maombi ya ushirika na kanisa zima japo ni vizuri
zaidi, lakini unaweza ukafanya na baadhi ya jamaa wachache.
Mathayo 18:19. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili
wenu (ushirika) watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba,
watafanyiwa na Baba yangu (Yesu) aliye mbinguni”.
Maombi kwa wengine.
Haya ni maombi ambayo muombaji hutenga siku maalumu
au huamua kufanya maombi maalumu kwa ajili ya kuombea wengine, yeye hajihusishi
kabisa katika maombi haya. Anakwenda mbele za Mungu akibubujika na kulia kwa
sababu yaw engine.
Unaweza ukaliombea kanisa lote, Mungu alisimamishe
imara na kulipa kibali, alizidishie upendo, tena ikiwezekana kwa kuwataja
majina washirika wa kanisa hilo. Na siyo lazima liwe kanisa unaloabudia,
unaweza hata kuliombea kanisa la jirani. Au hata kuiombea familia ya jirani
yako, Mungu ailinde, aibariki na mambo mengine mazuru mengi.
Wakolosai 1:9. “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu
siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe
maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni”.
2 Timotheo 1:3. “Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa
dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavya wewe daima,
katika kuomba kwangu, usiku na mchana”.
Kuombea wengine (tofauti na maombi ya kuombea adui),
ni agizo kwa kanisa pia; kwa sababu tusipowaombea wengine, tunaonesha ubinafsi,
na kama tutakuwa wabinafsi basi kumpenda Mungu hakupo ndani yetu. Na kama
hatumpendi Mungu, tunafanya dhambi.
1 Samweli 12:23. “Walakini mimi, hasha! Nisimtende
Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia
iliyo njema, na kunyoka”.
Maombi ya sifa.
Haya ni maombi ambapo mwombaji anayatafakari matendo
makuu ya Mungu aliyomtendea katika maisha yake, sehemu ngumu alizokuvusha
amabzo kwa akili zako ilishindikana, wema wote ambao Mungu amekufanyia,
kukuweka kuwa hai na wakati wapo uliozaliwa nao tarehe moja, mwezi mmoja au
mwaka mmoja hawapo.
Ndipo muombaji hububujika na sifa mbele za Mungu
wake, moyo wake humshangilia Bwana mchana na usiku.
Zaburi 34:1 na 3. “Nitamhimidi Bwana kila wakati,
sifa zake zi kinywani mwangu daima. Mtukuzeni Bwana pamoja name, na
tuliadhimishe jina lake pamoja”.
Sehemu nyingine katika Biblia, maombi haya ya sifa
yamefananishwa na sadaka mbele za Mungu.
Hosea 14:2. “Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie
Bwana; mkamwambie, ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo
tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe”.
Maombi ya shukurani.
Maombi haya kidogo yafanane na maombi ya sifa,
lakini tofauti yake ni kwamba maombi ya sifa unamtolea Mungu sifa za midomo
yako kulingana na matendo yake wakati maombi ya shukrani ni kwamba unampa Mungu
shukrani kwa mema yote aliyotenda kwako na hata kwa wanaokuzunguka.
Waefeso 5:20. “na kumshukuru Mungu Baba siku zote
kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo”.
Wakolosai 3:17. “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye
(Yesu Kristo)”.
Kwa imani niliyonayo na imani uliyonayo, Mungu akutendee sawa sawa na maombi yangu hapa chini,
"Ni maombi yangu, Bwana Mungu; afungue vilivyofungwa,
arejeshe vilivyonyang’anywa, ainue huduma zilizolala, afufue huduma zilizo
kufa, abariki palipo laaniwa, na akuinue mtumishi wake kutoka utukufu uliopo
akupandishe juu zaidi, kwa jina la Yesu Kristo. Amina!".
Unapobarikiwa, fanyika baraka na kwa wengine. Tafadhari shiriki somo hili katika ukurasa wako wa "twitter" na "facebook".
Usikose kamilisho la somo hili siku ya jumapili tarehe 7/7/2013, kuna kitu cha tofauti sana Mungu atakwenda kukutendea na kujibu maombi yako. Amina.