Yohana Mbatizaji aliuliza swali hilo kana kwamba
hamjui Yesu Kristo na hakuwahi kumuona bali alizisikia habari za ujio wake tu.
Lakini ukisoma maandiko utaona kuwa Yohana mbatizaji
alikuwa akimjua Yesu Kristo na aliwahi kukutana naye;
Mathayo 3:11. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa
ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala
sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na
kwa moto.
Mstari huo wa Biblia unatueleza kuwa Yohana
Mbatizaji aliutambua ujuo wa Yesu Kristo hata kabla hajaonana na Yesu Kristo
mwenyewe.
Mathayo 3:13-14. Wakati huo Yesu akaja kutoka
Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia,
akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
Mstari huo wa Biblia unathibitisha kuwa Yohana Mbatizaji
aliwahi kukutana na kuongea na Yesu Kristo, na alimtambua kuwa ndiye Masihi wa
Mungu kwa sababu alitaka kumzuia asimbatize bali yeye Yohana ndiyo abatizwe na
Yesu. Pia sauti ya uthibitisho ilisikika kutoka mbinguni, na mkutano wote
waliisikia (Mathayo 3:17).
Sasa iwaje Yohana Mbatizaji alipokuwa gerezani na
alipozipata habari za Yesu Kristo na matendo ya miujiza aliyoifanya (alizijua
nguvu zake pia, Mathayo 3:11b), aliwatuma wanafunzi wake wakamuulize Yesu
Kristo swali hili; “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Mathayo 11:3.
Yohana Mbatizaji aliuliza swali hili kwa sababu;
alitegemea Yesu Kristo angeenda kumuona gerezani, na alitegemea kupata
kipaumbele kutoka kwa Yesu katika kipindi alichokuwa kizuizini, lakini Yesu
Kristo aliwapa kipaumbele wenye dhambi na watoza ushuru (Luka 15:2).
Yesu Kristo alitambua makusudi ya Yohana Mbatizaji
kuuliza swali hilo, ndipo alipowajibu wanafunzi wa Yohana Mbatizaji;
(a). “Nendeni mkamueleze Yohana mnayoyasikia na
kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa,
viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.”
Mathayo 11:4, 5.
Hapa Yesu Kristo alikuwa akimthibitishia Yohana
Mbatizaji kuwa yeye ndiye.
(b). baada ya wanafunzi wa Yohana Mbatizaji kuondoka
Yesu Kristo akaongezea, “Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Maana Yohana
alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo. Mwana wa Adamu alikuja akila na
kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye
dhambi!” (Mathayo 11:16-19).
Ukiangalia pia Luka 5:30-32. Ikawa mafarisayo na
waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa
pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, wenye afya
hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki,
bali wenye dhambi, wapate kutubu.
Hapo Yesu Kristo alitaka kutufundisha kuwa
anachokipa kipaumbele zaidi ni kile kilichomleta duniani; kuutangaza ufalme wa
Mungu na kuziokoa roho zinazopotea dhambini. Ndipo aliposema mfano huu, “ni
nani kwenu aliye na kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini
na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?”, “Nawaambia,
vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja
atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya
kutubu”. Luka 15:3-7.
Yesu Kristo anazidi kufafanua kuwa, yeye kuwa karibu
na wenye dhambi ni ili aziokoe roho zao. Hawapi kipaumbele zaidi wenye haki,
bali wenye dhambi.