Nakusalimu kupitia jina la Mwalimu Mkuu,
Yesu Kristo.
Binti wa umri wa miaka 5 alitenda
kosa mara moja, mama yake akamchapa viboko vitatu huku akimkanya kwamba
alichofanya ni kosa asilotakiwa kulirudia tena, yule binti mdogo alilia
akisema, “mama nimekosa, sitarudia tena”. Kwa mara nyingine yule binti mdogo
alikosea tena, siku hii baba alikuwa nyumbani, binti yule kipenzi cha baba alipokosea. Baba akamchapa binti yake kiboko kimoja na kumkanya kutorudia tena
kosa lile. Yule binti mdogo alilia sana, kwa uchungu na hakutaka kubembelezwa
na mtu yoyote yule isipokuwa baba yake aliyemchapa.
Katika simulizi hiyo hapo juu
tunajifunza mambo makuu mawili. Mosi; binti mdogo alilia zaidi alipochapwa
kiboko kimoja na baba kuliko alipochapwa viboko vitatu na mama. Hii ni sababu
yule binti mdogo ni kipenzi cha baba zaidi ya mama. Alipochapwa na mama
hakujali sana, aliona anafundishwa kutokosea. Lakini alipochapwa na baba aliona
ameonewa, kwa upendo mkubwa wa dhati baina yake na baba yake, haikupaswa baba
amuadhibu kwa kukosea kwake. Pili; binti mdogo hakutaka kubembelezwa na mtu
yoyote isipokuwa baba yake aliyemuadhibu kwa sababu, kubembelezwa na baba ni
sawa na baba kuomba msamaha kwa kumuadhibu binti yake, jambo ambalo lingempa
faraja binti mdogo yule.
Wanadamu wote tuna tabia inayofanana
na huyu binti mdogo katika simulizi hii, hivyi ndivyo tulivyoumbwa tangu utoto
wetu. Tukikosewa au kutendwa na tunaowapenda sana, tunaumia sana mioyoni mwetu
na kubeba maumivu ambayo hudumu mioyoni mwetu kwa muda mrefu sana kuliko
tukikosewa na watu wasio karibu nasi au wapendwa kwetu. Uchungu hujaa mioyo
yetu kwa sababu hatutegemei wale tunaowapenda sana kutuumiza, tunajizuia sana
kutowaumiza ili tusiwapoteze, tunategemea nao wafanye sawa na hivyo. Hatuwezi
kutua mzugo wa uchungu uliojaza mioyo yetu hadi pale tutakapo sikia neno la
kuomba msamaha kutoka kwa waliotuumiza. Kila siku unatamani na kusubiri
aliyekuumiza akwambie samahani, pole, sitakuumiza tena. Nafsi yako ipate furaha
na amani.
Kuna watu wamefanya maamuzi magumu,
hata kujiumiza zaidi katika miili yao au kujitoa uhai kwa sababu ya kushindwa
kuvumilia na kuyashinda maumivu yaliyosababishwa na wanaowapenda sana. Katika
somo hili utajifunza kupokea maumivu kutoka mtu yoyote na namna ya kuyakabili
maumivu hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na maumivu hayo
ikiwemo kuchanganyikiwa akili au kujitoa uhai.
Mtu yoyote anaweza kukuumiza nafsi
Tunawaamini sana wanadamu wenzetu,
kiasi kwamba hatudhani kama wanaweza kutusababishia maumivu makubwa na yenye
madhara kwetu. Tunadhani, endapo tutawatendea wema nao wataturudishia wema na
kumbe sivyo, wanaweza kutulipa ubaya wenye kuumiza zaidi. Kuna mtu alisema,
“wewe kutomla simba haimaanishi simba kutokukula wewe” au “not eating a lion doesn’t mean a lion won’t eat you”. Kutowatendea
mabaya tunaowapenda haimaanishi wao pia hawatatutendea sisi mabaya katika hatua
moja au nyingine ya maisha yao. Ukweli huu ndio unaotufanya tuumizwe sana
endapo tunaowapenda watatutenda ubaya, kwa sababu hatutegemei kupokea mabaya
kutoka kwao. Kuna watu wameumizwa hata wakasema hawata samehe kamwe kwa sababu
tu waliowaumiza ni waliowapenda zaidi. Kusamehe ni lazima. Ufundishe moyo wako
kutegemea chochote; ubaya au wema kutoka kwa yoyote. Anayetuwazia na kutupatia
mema siku zote za uhai wetu ni Mungu pekee.
Mara baada ya kuumizwa na uliyempenda
sana, samehe kwa dhati
Hakuna mwanadamu aliyemkamilifu kwa
namna moja au nyingine, sote tuna mapungufu isipokuwa Mungu pekee. Katika
maisha yetu ya kila siku, mtu mmoja anaweza kummumiza mtu mwingine kwa
kutokukusudia au kwa kukusudia. Baada ya kusababisha maumivu anaweza kuomba
msamaha au hata asiombe msamaha tena kwa makusudi hasa kama akitambua
aliyekuumiza huwezi kumuumiza kwa kulipa kisasi (makusudi) au bahati mbaya. Uambie
moyo wako usamehe na kuachilia mzigo wa hasira na maumivu uliyoyabeba.
Tunaposamehe ni kwa faida yetu kwanza, Waefeso 4:31-32 na Mathayo 6:14-15 (tunajiponya
nafsi na kupata kibali cha msahama mbele za Mungu) na faida ya tunaowasamehe.
Ndio, faida ya tunaowasamehe. Wapo wasioweza (wanaokosa ujasiri) kuomba msamaha
kwa sababu wao pia huumia mara baada ya kuona wamewaumiza wanaowapenda sana.
Usitake kujua sababu ya kuumizwa
kwako
Wanadamu wengi tunapenda kujua sababu
ya kuumizwa kwetu tukidhani itasaidia kutoumizwa tena. Lakini nikufahamishe,
wengi wanaotuumiza huwa hawana sababu madhubuti za kutuumiza, na endapo
tutahitaji kujua sababu, hawataweza kutupatia sababu madhubuti vile vile.
Hivyo, siyo muhimu kujua sababu ya kuumizwa zaidi ya kusamehe na kuachilia.
Usilipe kisasi
Usiwe na tabia ya kulipa kisasi kwa
waliokutendea ubaya. Kulipa kisasi ni kuumia zaidi, hasa utakapotambua
aliyekuumiza hakukusudia kufanya hivyo. Nafsi yako itakuwa imeumia mara mbili
kwa kuiumiza nafsi isiyo na hatia. Moyo wako utajaa chuki na hasira dhidi yako
binafsi. Hasira au chuki binafsi “self denial” ina madhara makubwa sana. Idadi
kubwa ya wanadamu wanojitoa uhai wanakuwa chini ya utawala wa hii roho chafu
“self denial”. Mungu anatuagiza tusilipe kisasi, kwa sababu kisasi ni chake (Warumi
12:19 na Mithali 24:29) na siyo chetu.
Waombee na kuwapenda wanaokutenda ubaya
Hili ni agizo la Mungu (1 Petro 3:9),
tuwaombee na kuwapenda wanaotutenda ubaya. Hii ni kwa sabau kubwa mbili, moja;
Mungu hutubariki na kutuinua na pili; huwafanya waliotutenda ubaya kujifunza
wema wa Mungu kupitia maisha yetu. Tunapowaombea waliotuudhi tunainuliwa
kiimani, waombe heri na siyo laana. Pia Mungu huachilia baraka zake kwetu
maradufu zaidi ya tuombavyo, kwa sababu huonesha roho, moyo na nafsi
iliyopondeka na kunyenyekea mbele za Mungu zaidi ya maumivu tuliyonayo mioyoni.
Tunapowalipa mema waliotutenda ubaya, inawapa fundisho la kuuona wema wa Mungu
kupitia maisha yetu. Inakufanya ufanyike baraka kwa wote, wema na waovu kwako,
hii ni tabia halisi ya Mungu, huwanyeshea mvua wema na waovu.
Dumu katika sala na maombi, ni nguzo
madhubuti ya kuishi maisha yenye amani, furaha na upendo. Amina.