Maana
na makusudi ya kujaribiwa
Jaribu linasemekana kuwa ni mtaji wa kuinua imani ya
mtu anayejaribiwa, lakini binafsi ninapenda kuirekebisha sentensi hii. Jaribu
ni mtaji wa kuinua imani ya anayeshinda jaribu; kama umejaribiwa na jaribu
likakuangusha, siyo sahihi kusema jaribu hilo lililokuangusha lilikuwa mtaji wa
kuinua imani yako. Imani ipi? Kama umeshindwa kuitetea imani yako na
kuangushwa, jaribu halikuwa mtaji kwako.
Jaribu huja na makusudi mawili; moja, ni
kumuimarisha kiroho na kuinua imani ya anayejaribiwa na kushinda jaribu. Pili,
ni kumuangusha mtakatifu na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Na mara nyingine
jaribu au teso huwa ni kiboko cha Mungu cha kulirudi kanisa lake. Ninaposema
kanisa ninamaanisha Mkristo.
Kuinua imani ya Mkristo. Nikupe mfano kwanza, kuna
hekima ya Kimungu na hekima ya kibinadamu.
Hekima ya Kimungu hupewa mtu yoyote pasipo kujari umri, na hii huletwa
na Yesu Kristo mwenyewe. Na hekima ya kibinadamu huja kutokana na uzoefu wa
muda mrefu alionao mtu katika jambo fulani, na hekima hii wanayo wazee. Na
imani ndivyo ilivyo, ili ikue ni lazima ipitishwe katika kujaribiwa, ipitishwe
katika vitu ambavyo sayansi na akili ya kibinadamu haviwezekani. Ukiisha pita
hapo kwa msaada wa Mungu kwa jina la Yesu Kristo ndipo imani yako inapokuwa.
Ndipo unapozidisha imani na uhusiano wako na Mungu kupitia Yesu Kristo (Yohana
11:3-4, 14-15 na 1 Petro 1:6-7)
Kumuangusha mtakatifu. Hili ni jaribu linalosababishwa
na shetani moja kwa moja, na makusudi yake huwa ni kumuangusha mtakatifu ili
kuharibu na kufuta kabisa uhusiano wake na Mungu. Kwa mfano, Ayubu hakujaribiwa
ili kuinua imani yake au kurudiwa na Mungu, alijaribiwa ili amkufuru Mungu, kwa
Kiswahili chepesi ni ili avunje uhusiano wake na Mungu. Kwa hiyo kuna wakati
shetani huwajaribu Wakristo ili awafarakanishe na Mungu (Yohana 2:10, Ayubu
2:4-5)
Kurudiwa na Mungu. Hapa naomba nieleweke, hili kwa
upande mmoja siyo jaribu na kwa upande mwingine ni jaribu. Nina maana gani; kwa
upande wa Mungu ni kiboko cha kulirudi kanisa lake kama ilivyo kwa mzazi
anapomuadhibu mtoto aliyekosea. Kwa upande wa Mkristo, analiona kama jaribu. Na
hili hutupata ikiwa tumekengeuka na kuiacha njia ya haki, tumemkosea Mungu. Na
tukitubu na kuirudia njia ya haki, utaona mateso yote yanaondoka pia (Mithali
3:11-12, Ayubu 5:17)
Nini
cha kufanya uwapo katika jaribu
Kuna makosa makubwa mawili ambayo Wakristo wengi
tunayafanya tuwapo katika majaribu. Na makosa haya ndiyo yanayogharimu uhusiano
wetu na kutufarakanisha na Mungu. Makosa hayo ndiyo yanayofanya tunaangushwa na
majaribu.
Kosa la kwanza; tunatumia akili zetu kutafuta
ufumbuzi wa jinsi gani tutavuka jaribu tunalopitia kwa ushindi na kumuacha
Mungu kando ambayo ndiye msaada wetu. Hapa ni lazima uelewe, Mungu pekee ndiye
anayetushindia majaribu, kwa akili zetu na nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi
kamwe kujinasua katika majaribu. Uwapo katika jaribu ni lazima umkabidhi Mungu
njia zako na jaribu lako, Yeye ndiye ushindi wako kwa Jina la Yesu Kristo (2
Petro 2:9, Zaburi 37:5)
Kosa la pili; kuwaangalia wanadamu wanafanya nini na
wanasema nini tunapopita katika jaribu hasa wapendwa au wakristo wenzetu. Kitu
tunachojisahau hapa ni kwamba tunategemea wingi wa marafiki tunaokuwa nao
wakati wa furaha ndio hao hao tutakao kuwa nao wakati wa majaribu, sivyo! Uwapo
katika shida au jaribu kama kuna mkristo mwenzako atabaki na wewe hiyo ni neema
tu ya Mungu, lakini wengi kama siyo wote watakuacha peke yako.
Unajua kwa nini watakuacha peke yako? Jaribu siyo
lao ni lako, anayepaswa kushinda siyo weo ni wewe. Kwa hiyo ni lazima upite
peke yako ili ushinde peke yako na tuzo ya ushindi utapata peke yako. Hupaswi
kuwaangalia wapendwa na hupaswi kulalamika iwapo watakuacha upite katika jaribu
peke yako.