Ahadi za Mungu.
Mungu amefanya
ahadi nyingi kwa mwanadamu; ahadi za uponyaji, mafanikio, heshima, hekima,
ufaulu katika masomo na nyingine nyingi. Na wengi wetu tunazifahamu vizuri
ahadi hizo alizotuahidi Mungu; tunazisoma katika neno lake takatifu, Biblia na
pia tunazisikia kupitia watumishi mbalimbali wa Mungu.
Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya, Kwa maana wewe upo pamoja nami”, na
Zaburi 119:50 “Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi
yako imeniuhisha”.
Kupita kati ya
bonde la uvuli wa mauti (Zaburi 23:4) na kuwa katika taabu (Zaburi 119:50) ni
kuingia au kupitia katika hali zenye changamoto mbalimbali za kiafya; magonjwa
na udhaifu wa mwili, kielimu; kushindwa kutimiza malengo yako, kiuchumi; hali
ngumu ya kiuchumi au kukosa ajila licha ya kuwa na elimu stahiki, kijamii;
kukosa watoto kwa miaka mingi katika ndoa na hata jamii inakuita tasa, kufiwa
na watoto pale tu wanapozaliwa na changamoto za namna nyingine nyingi. Katika
neno la Mungu hapo juu tunafundishwa kwamba kuna nyakati tutaingia katika
changamoto, taabu au bonde la uvuli wa mauti katika maisha yetu. Jambo la
kujiuliza hapa, je tuingiapo katika changamoto au taabu hizo tunachukua hatua
gani? Je, tumekuwa ni watu wa kumlaumu Mungu kwanini ameruhusu tuingie katika
taabu? Na kama tumekuwa ni watu wa
kulaumu na tunasubiri majibu kutoka kwa Mungu hakika Mungu hata tujibu kamwe,
kwa sababu Mungu hana majibu ya lawama. Mungu anayo majibu ya maneno au maombi
yenye hoja zilizojengwa katika imani ya neno lake tu.
Na ndiyo maana kupitia
mistari ya neno la Mungu hapo juu anatufundisha kuwa na imani kwa ahadi zake
kwetu. Anaposema “sitaogopa mabaya, kwa
maana wewe upo pamoja nami”, Mungu kuwa pamoja naye ni kwamba ahadi ya Mungu ya
ukombozi imemfunika na ni lazima atatoka katika bonde hilo la uvuli wa mauti,
na “ahadi yako imeniuhisha” anamaanisha hawezi kukata tama pasipo kujali
anapitia taabu ya namna gani kwa sababu ukombozi wake unakuja tena uko karibu.
Na sisi tunapopitia
katika mahangaiko, taabu, shida na misukosuko ya maisha tusiwe ni watu wa
kulaumu na kulalamika mbele za Mungu, bali tuwe ni watu wenye kusimama katika
maombi yenye imani ya ukombozi tukiziangalia ahadi za Mungu katika taabu zetu.