Torati 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi
leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua
uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako”
Hilo lilikua ni neno la Mungu mwenyewe akimwambia Musa na
wana wa Israeli, neno hilo ni kwa ajili yako leo. Mungu anaweka mashahidi
wawili, mbingu na nchi, anapoweka njia mbili mbele yako na kukushauri njia ya
kuchagua.
Mungu anakushauri uchague uzima ili uwe hai, haimaanishi
hutakufa, la hasha, bali siku ya ufufuo na hukumu ya haki ya Mungu utapata
ufufuo wa uzima wa milele. Ikiwa utachagua mauti, utapata ufufuo wa hukumu ya
uharibifu pamoja na dunia hii itakayokunjwa kama karatasi na kutupwa jehanamu
kutakako kuwako kilio na kusaga meno.
Yohana 14:6 “Yesu akawaambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na
uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”
Yesu Kristo ndiye njia, kweli na uzima. Kwa maana nyepesi,
Mungu anakushauri kuichagua njia yenye uzima. Kwa maneno mengine, Mungu
anakushauri kumchagua Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Kwa
sababu Yesu Kristo ndiye njia pekee ielekeayo uzimani, kule Mungu anakushauri
uchague.
Kama bado hujamchagua Yesu Kristo hujachelewa, wakati bado
upo, fanya uamuzi sahihi sasa (bonyeza hapa). Kama umemchagua Yesu Kristo
tayari, amekuwa Bwana na Mwokozi wako, umefanya vema.
Kuingia mbinguni (kupata uzima wa milele), kunaambatana na
vitu vikuu viwili; Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako na matendo
yako baada ya kumchagua Yesu Kristo hadi kifo chako cha mwili huu uharibikao.
Kwa sababu siku ya hukumu ya haki ya Mungu, kila nafsi
itahukumiwa kutokana na matendo yake na italipwa kwa haki kulingana na
ilivyotenda hapa duniani (Yohana Mtakatifu 5:28-29 na Mathayo Mtakatifu 16:27).
Matendo yako hapa duniani ndiyo yatachagua njia
utakayoiendea baada ya kifo na hukumu ya haki ya Mungu. Kifo ni fumbo
lililokosa ufumbuzi, huja wakati tusiodhani, wapo waliosema watajiandaa
kutengeneza maisha yao yajayo na wakaendelea kufanya uovu wa kila aina, lakini
wakapatwa na kifo ghafla pasipo kujiandaa.
Ikiwa umempokea Yesu Kristo, hakikisha unajitakasa kila
iitwapo leo ili kujiweka tayari na safari isiyojulikana itakuwa lini. Na ikiwa
bado hujampokea Yesu Kristo, nafasi ndiyo hii, amua sasa.
Hukumu ya jehanamu haitapendelea waliokiri kumpokea Yesu
Kristo na hali matendo yao ni maovu. Anayestahili mapigo, atapata mapigo, hii
ni kulingana na matendo ya kila nafsi hapa duniani (Luka Mtakatifu 12:45-48).