YESU KRISTO ASIFIWE!
Karibu tena ndigu msomaji wangu;
sifa, heshima na shukrani ni kwake Mungu Baba wa mbinguni aliyetupa kibali
tuweze kukutana tena katika sehemu ya mwisho ya somo letu lenye kichwa
kisemacho “MAOMBI YENYE KIBALI NA NGUVU MBELE ZA MUNGU”.
Ikiwa leo ndiyo mwisho wa somo
hili, nina imani Mungu atakuwa amekuhudumia kwa namna ya pekee na utakwenda
kupokea kitu kipya katika maisha yako ambacho kitafanyika baraka ya pekee
katika maisha yako. Endelea!
Kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu.
Isaya 55:10-11. “maana kama vile mvua ishukavyo, na
theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na
kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;
ndivyo litakavyokuwa neno langu (Bwana Mungu), litokalo katika kinywa change;
halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika
mambo yale niliyolituma”.
Hayo ni maneno ya Mungu mwenyewe, anasema neno
(ahadi) lake ni kama mvua ishukavyo toka mbinguni kuinyeshea ardhi isivyorudi
mbinguni, ndivyo neno (ahadi) lake lisivyokuja tupu pasipo kutimiza mapenzi
yake yaliyopo ndani ya neno (ahadi) lake.
Unaweza ukajiuliza kama neno la Mungu lazima
litimize mapenzi yake, kwa nini basi tunapaswa kuomba? Ahadi ya Mungu ipo
inatuzunguka wote, kama neno lake linavyosema yeye huwanyeshea mvua wote wenye
haki na wasio haki (Mathayo 5:45). Lakini ili ahadi ya Mungu itimie katika
maisha yako ni lazima uombe. Tuangalie kidogo neno:-
Isaya 43:26. “Unikumbushe (ahadi yangu); na
tuhojiane (uiombe); eleza mambo yako, upate kupewa haki yako (kutimiziwa ahadi
ya neno langu)”.
Hapo juu pia ni maneno ya Mungu mwenyewe, kwa nini
niende mbele za Mungu kuomba anitimizie ahadi ya neno lake? Kwa nini
nimkumbushe, ina maana amesahau? La hasha, Mungu hajawahi kusahau na hatakuja
kusahau, tunapokwenda mbele za Mungu, tunakili na kuthibitisha imani yetu
kwake. Hicho ndicho kitu, Mungu anapenda kutoka kwetu. Ndiyo maana Yesu Kristo
alipokuwa akiwaponya wagonjwa alikuwa akiitazama imani iliyomo ndani ya mioyo
yao.
Mungu hajawahi kudanganya na hatakuja kudanganya,
lakini lazima tuombe ili tuikili na kuithibitisha imani yetu kwake. Tofauti ya
imani kati kati yetu, hufanya tofauti ya kupokea kwetu kutoka kwa Mungu.
Unaweza ukawa hujanielewa, ni hivi; mwenye imani haba hupokea haba na mwenye
imani nyingi hupokea vingi. Kwa sababu Mungu huwatendea wanadamu wote kulingana
na imani ndani ya mioyo yao.
Hebu tuangalie mistari michache ya maombi
yanayounganisha ahadi za Mungu;
Maombi
ya Mfalme Daudi; 2 Samweli 7:27-29. “Kwa kuwa wewe,
Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema,
Nitakujengea nyumba (ahadi); kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni
mwangu nikuombe dua hii. Na sasa, Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno
yako ndiyo kweli (ahadi yako ni hakika), nawe umemwahidia mtumwa wako jambo
hili jema; basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate
kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana Mungu, umelinena (umeahidi);
na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele”.
Zaburi 119:170. “Dua yangu na ifike mbele zako,
uniponye sawasawa na ahadi (ya uponyaji; Kutoka 23:25) yako”.
Kwa nini uombe kwa kuzitaja ahadi za Mungu.
- Ahadi za Mungu zimehakikishwa (ahadi timilifu).
2 Samweli 22:31(b). Mungu, njia yake ni kamilifu; ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye
ndiye ngao yao wote wanaomkimbilia.
- Mungu hasemi uongo.
Hesabu 23:19(a). Mungu si mtu, aseme uongo.
- Mungu ni mwaminifu, hutekeleza alichoahidi.
Kumbukumbu 7:9. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu
wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu,
ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata
vizazi elfu.
- Tukiomba sawasawa na mapenzi (ahadi) yake, atusikia.
1 Yohana 5:14. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake,
ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake (sawa sawa na neno au ahadi yake), atusikia.
- Ni lazima atimize ahadi yake kwanza, kwa sababu ameikuza kuliko jina lake.
Zaburi 138:2. Nitakusujudu nikilikabili hekalu lako
takatifu, nitalishukuru Jina lako kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
kwa maana umeikuza ahadi yako kuliko
jina lako lote.
Ni maombi yangu, Bwana Mungu; afungue vilivyofungwa,
arejeshe vilivyonyang’anywa, ainue huduma zilizolala, afufue huduma zilizo
kufa, abariki palipo laaniwa, na akuinue mtumishi wake kutoka utukufu uliopo
akupandishe juu zaidi, kwa jina la Yesu Kristo. Amina!
Nina imani umebarikiwa sana, na umepokea kitu cha tofauti katika kukuinua kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine mbele, utukufu ni kwa Mungu (Yehova) mwenyewe.
Ili kuweza ku-download PDF ya somo hili lote tangu mwanzo hadi mwisho, bonyeza HAPA.