Monday, August 12, 2019

MIPAKA YA AHADI NA BARAKA ZA MUNGU KWAO WAMUAMINIO

Imani yako ni ufunguo unaofungua baraka na wema wa Mungu maishani mwako (picha kwa hisani ya "ChristArt")


Ahadi ni nini?
Ahadi ni tangazo maalumu linalothibitisha kutendewa jambo lililo nje ya uwezo wako na mtu mwingine au uthibitisho maalumu kwamba jambo fulani lisilotegemewa kutoke litakwenda kutokea.
Ahadi za Mungu zipo katika nene lake (Biblia) kwa wamuaminio. Ahadi hizo ni kutuokoa kutoka kila aina ya maumivu na mateso (njaa, ufukara, magonjwa, vita n.k) na kutujaza mema yake yote (kibari, baraka, amani, furaha, utajiri wa kiroho na kimwili).
Soma vifungu vifuatavyo vya Biblia uone ahadi za Mungu zitupazo tumaini la ukombozi dhidi ya dhiki na mateso ya adui shetani (Wagalatia 5:1, Yakobo 4:7, Zaburi 32:7, Zaburi 34:4, Isaya 43:18-19, Yohana wa kwanza 5:4-5) kwa uchache. Kuna vifungu vingi sana katika Biblia takatifu ambavyo Mungu anasema na kila anayemuamini kwa suala la kumkomboa kutoka dhuluma za shetani.
Soma vifungu vifuatavyo vya Biblia unoe ahadi za Mungu ziachiliazo mema ya Mungu kwao wamuaminio (2 Samweli 7:28, Zaburi 5:12, Isaya 43:2, Zaburi 84:11, Mathayo 7:11, Zaburi 23:6, Marko 10:29-30) kwa uchache. Neno la Mungu linabeba ahadi nyinyi sana za wema wa Mungu kwa wanaoamuamini, kazi ya mwanadamu ni ndogo sana, ni kumuamini Mungu tu, kisha mema ya Mungu yanatimizwa katika maisha yako. Kosa kubwa linalofanywa na waamini wengi ni kumfanya Mungu mbadala. Muamini anaamini ahadi ya kupokea mema ya Mungu lakini kwa wakati huo huo anatafuta njia mbadala za kupokea mema hayo tena hata kwa njia zisizompendeza Mungu. Kwa mfano, muamini anaweza kuwa anaomba uponyaji kwa Mungu kupitia neno la Mungu linalobeba ahadi za Mungu za uponyaji na wakati huo huo anahangaika kwa waganga wa nguvu za giza kutafuta msaada. Hata siku moja Mungu hafanyi kazi na watu wanomfanya yeye kama mbadala “alternative” wa njia zao wenyewe.
Soma vizuri mstari wa Biblia wa Marko 10:29-30, kupokea mema ya Mungu kwa kipimo kilichojazwa na kusukwa sukwa hata kinafurika inahitaji kujikana. Ni lazima muamini uachane na kona kona za dunia hii na kuamua kumfanya Mungu ndio msaada na tumaini lako pekee.

Je ahadi za Mungu ni za aina gani?
Ahadi za Mungu zimehakikishwa (ahadi timilifu).
2 Samweli 22:31(b). Mungu, njia yake ni kamilifu; ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao wote wanaomkimbilia.

Mungu hasemi uongo.
Hesabu 23:19(a). Mungu si mtu, aseme uongo.

Mungu ni mwaminifu, hutekeleza alichoahidi.
Kumbukumbu 7:9. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu.

Tukiomba sawasawa na mapenzi (ahadi) yake, atusikia.
1 Yohana 5:14. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake (sawa sawa na neno au ahadi yake), atusikia.

Ni lazima atimize ahadi yake kwanza, kwa sababu ameikuza kuliko jina lake. 
Zaburi 138:2. Nitakusujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, nitalishukuru Jina lako kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana umeikuza ahadi yako kuliko jina lako lote.


Tofauti ya ahadi za Mungu na ahadi za kipepo/kishetani
Ahadi za Mungu zinatimia kwa wanaomtegemea Mungu kwa asilimia mia moja (100%), ambao hawamfanyi Mungu ni mbadala wa njia zao binafsi. Pia, ahadi za Mungu hazitimii pasipo kuwa na muda wa ukomavu kiimani ili kuweza kuzipokea na kuzitunza ahadi hizo. Soma Biblia vizuri kwa msaada wa Roho Mtakaktifu utaelewa, watu wote Mungu aliofanya nao ahadi, kuna muda ulipita kabla ya ahadi zile kutimia. Angalia mifano ifuatayo;

Ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu
Ahadi ya Mungu na Ibrahimu kuhusu uzao wa ahadi “the promised seed”, ilimchukua Ibrahimu miaka isiyopungua 13 kuipokea ahadi hii (Mwanzo 17-32).

Ahadi ya Mungu kwa Daudi
Ilimgharimu takribani miaka 15 Daudi tangu apakwe mafuta na Samweli nabii hadi kuwa mfalme wa Israeli taifa teule la Mungu (1 Samweli 16).

Mungu akifanya ahadi na muamini huachilia muda wa ukomavu “maturity” ambao utaambatana na majaribio kadhaa. Majaribio haya lengo lake ni kumuimarisha muamini na siyo kumuangusha ili aonekane hafai “disqualifying”. Kama tumaini la muamini ni Mungu pekee, kwa hakika atavuka salama na kwa ushindi wenye kumpa sifa na utukufu Mungu kuelekea ukuu, kwa sababu kwa neema ya Mungu tunakuwa kutoka hatua moja hadi nyingine. Muamini yoyte atakaye mfanya Mungu ni mbadala wa njia za kibinadamu, kwa hakika hataweza kuvuka kipindi hiki cha majaribio. Na hapa ndipo wengi wanapofeli na kudhani hakuna mafanikio kwa wamtumainio Mungu. Mafanikio yapo tele, ikiwa wewe umeshindwa usiwakatishe tamaa wengine (hii ni tabia ya adui, ibilisi).
Mafanikio ya kipepo/kishetani/kichawi ni mafanikio yanayopatikana baada ya muda mfupi sana na yanaambatana na sadaka ya umwagaji damu mar azote. Mafanikio ya kishetani yana mateso makubwa ndani yake, wengi waliofanikiwa kwa njia hii huwa na furaha na sura za vicheko mbele za watu lakini wakiwa peke yao usiku ni mateso na majuto. Ahadi hizi zina kitanzi cha umauti na hazidumu. Mwisho wa mafanikio ya kipepo ni mauti na uharibifu.

Ukomo wa ahadi za Mungu
Ahadi za Mungu zinakoma mara tu muamini anapoacha kumtegemea Mungu. Kwa ufafanuzi Zaidi, Mungu akikuahidi jambo, mfano kukupatia mtoto baada ya miaka kadhaa ya kuhangaika huku na huko, katika kipindi cha mpito kuelekea kutimia kwa ahadi ya Mungu, ukahisi Mungu anachelewa sana ukaanza kuingiza mambo ya wanadamu sijui meza miti shamba fulani, sijui twende kwa mtaalamu fulani, sijui twende kwa bibi au babu fulani amewasaidia wengi na wewe utafanikiwa, hapo ndipo Mungu anakuacha uzitumainie akili zako na yeye anakaa pembeni. Ni kweli unaweza fanikiwa kupata mtoto lakini mtoto utakaye mpata anakuwa na asili ya kipepo kwa sababu ni mali ya mapepo na amepatikana kwa nguvu za giza. 

Labda nikupe mfano rahisi, wengi tunajiunganisha katika huduma za maji safi za miji au majiji tunamoishi kwa kutumia mabomba maalumu. Kupitia hilo bomba, maji yanatiririka kuja majumbani mwetu. Ikitokea ukaamua kukata hilo bomba kutoka maji safi na kuliunganisha kwenye bomba la maji taka hakika utegemee kupokea maji taka nyumbani mwako. Na hii ndivyo inavyokuwa pale tunapoamua kuacha kumtegemea Mungu, siyo kwamba Mungu anaamua kukata Baraka na wema wake kwetu, la hasha, bali sisi ndio tunakuwa tumejiondoa katika mfereji wa kupokea baraka na wema wa Mungu. Kwa sababu imani yetu kwa Mungu ndiyo mlango na bomba pekee ya kuachilia baraka na wema wake kwetu. 

Hitimisho
Endapo unadhani ulijiondoa katika mfereji wa baraka na wema wa Mungu na unataka kujiunganisha tene soma vifungu vya Biblia vifuatavyo (2 Mambo ya Nyakati 30:9 na 2 Mambo ya Nyakati 7:14) na uhakikishe unaomba toba na kurejea tena kwa Mungu. Mungu wetu (Yehova) ni mwingi wa rehema, uwe na imani kuwa atakusamehe na kukubariki na kukufunika na wema wake.

“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” 2 Mambo ya Nyakati 7:14. Kuiponya nchi, ni kuachilia baraka na wema wa Mungu katikati ya maisha ya wanaomuamini. Ujue ya kwamba, paripo na baraka au wema wa Mungu laana na mikosi haiwezi ikakaa hapo.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts