Monday, December 24, 2012

X-MAS SIYO CHRISTMAS.

Ni jambo la kawaida kwa wa-Kristo wengi kuchukulia mambo katika hali ya kawaida pasipo kuchunguza uwepo na/au makusudi ya jambo au mambo hayo. Mfano mzuri na ndiyo ukweli halisi ni matumizi ya neno ‘X-mas’, ‘X-MAS’ au ‘Xmas’. Hilo ni neno moja isipokuwa ni tofauti ya matumizi ya herufi; herufi kubwa au herufi ndogo, lakini neno hilo linatumika kuwakirisha neno ‘Christmas’.

Mimi pia nilikuwa ni mmoja wa watumiaji wa neno hilo la kifupi (Xmas) kuwakilisha neno Christmas, inawezekana unalitumia neno hilo pasipo kujua unamaanisha nini au unalitumia kwa sababu unafikiri unaokoa wakati kwa kuiandika Christmas kwa neno fupi. Asante kwa dada yangu aliyenifumbua macho na kunifanya nilifuatilie neno hilo haraka sana.

Ukweli ni kwamba, X inawakilisha thamani, namba au kitu kisichojulikana katika hisabati (mathematics), na ukiliangalia neno Christ-mas na X-mas utapata kutambua kuwa herufi X inawakilisha neno Christ. Na kama X ni thamani, namba au kitu kisichojulikana katika hisabati (mathematics) na kwetu wa-Kristo, je ni halali kuitumia herufi isiyojulikana thamani yake kumuwakilisha Kristo? Kwamba hatumjui au hatuijui thamani ya Kristo?

Funguka macho, acha uvivu, hakikisha unaandika neno kamili, “Christmas”, tena linaandikwa kwa kuanza na herufi kubwa ‘C’.

Na jambo la pili nililojifunza ni kumtumia “Santa Claus” katika kipindi hiki cha kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo badala ya kumuadhimisha Yesu Kristo mwenyewe. Labda ni kwa sababu tunahamasisha kupeana zawadi, lakini ukweli ni kwamba tunapaswa tumtamke Yesu Kristo ambaye ni zawadi tosha maishani mwetu.

Na jambo la mwisho kwa leo ni jinsi wa-Kristo wengi tunavyosherehekea msimu huu wa sikukuu ya “Christmas” na mwaka mpya. Tunasherehekea tofauti na inavyotupasa tuisherehekee, tunasherehekea kwa matendo ya anasa na kujisahau, tumekuwa sawa na watoto wanaofurahi kufika kwa kipindi hiki kwa sababu watanunuliwa nguo mpya na kula chakula kizuri. 

Katika kipindi hiki tunapaswa kufanya tafakari ya mwaka mzima katika mambo makuu manne; imani, uchumi, jamii, kurekebisha. 

Imani: je, wewe mKristo umeitunza na kuitetea imani yako pasipo kumtenda Mungu dhambi kwa kipindi chote cha mwaka unaoumaliza?

Uchumi: je, umepiga hatua kiuchumi kama ulivyopanga na/au kutegemea wakati unaanza mwaka unaoumaliza?

Jamii: je, uhusiano wako na jamii unayoishi nayo unakuwa mzuri au unaharibika? Kama una familia, je familia yako inapata mahitaji muhimu na yale ya ziada kutoka kwako?

Rekebisha: hiki ni kipindi cha kutambua makosa, mapungufu na kufanya tathmini kwa ujumla. Jitahidi kutambua ni wapi ulipokwama na tafuta ufumbuzi ili usonge mbele na inapohitajika ushari, tafuta ushauri kwa watu wanaoweza kukusaidia, usimwambie kila mtu mapungufu yako. Zaidi mtegemee Mungu. 

Mwisho kabisa, ni lazima umshukuru Mungu; wewe umefika mwishoni mwa mwaka lakini yupo aliyepoteza uhai mwanzoni mwa mwaka, wewe umejenga nyumba japo ndogo lakini yupo ambaye analala kibarazani mwa duka la mtu, wewe ulilala njaa usiku mmoja lakini yupo aliyelala na kushinda njaa kwa zaidi ya siku tatu, wewe unaishi katika nchi yenye amani lakini yupo anayeishi katikati ya vita, wewe upo huru japokuwa huna kitu lakini yupo asiye na kitu kama wewe amesingiziwa kesi na kufungwa jela. Huna sababu ya kukwepa kumshukuru Mungu.

 "NAWATAKIENI KHERI YA 'CHRISTMAS' NA FURAHA YA MWAKA MPYA, 2013"

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts