Thursday, November 15, 2012

SIRI YA MAFANIKIO.


   Mpendwa katika Kristo Yesu, nakusalimu kwa Jina la Yesu.
Kabla hatujaangalia neno la Mungu katika kitabu chake kitakatifu Biblia, ningependa tushirikiane jambo ambalo wewe pia utakuwa shahidi wa jambo hili. Katika jamii niliyopo au hiyo uliyopo, kuna watu wanafanya kazi kwa bidii na kujituma mchana na usiku na wengine wanapokea mishahara mikubwa au minono kama inavyojulikana na wengi lakini ukiyatazama maisha ya watu hawa hayafanani na mategemeo ya wengi. Ni maisha ya kawaida sana, ambayo hata ukiyafananisha na maisha ya mtu fulani ambaye anapokea mshahara wa kiwango cha kawaida au kiwango cha chini huwezi kuamini. Unakuta mtu anapokea mshahara mdogo lakini ana mafanikio tofauti na mategemeo ya wengi.
Wewe pia unaweza ukawa miongoni mwa wengi wanaodhani unono au ukubwa wa mshahara ndiyo mafanikio. Hapana, ipo siri katika mafanikio ya mtu yeyote, hata wewe ukiigundua siri hiyo ni lazima ufanikiwe na utashuhudia tu matendo makuu ya Mungu.
Siri ya mafanikio ni kutoa, unapotoa fedha na mali zako ili kuwasaidia wahitaji, Mungu anakubariki. Mungu atakubariki kwa sababu unapo msaidia muhitaji, hata kuripa fedha au mali, yeye atakuombea baraka kwa Mungu, na anaweza akakesha tena kwa machozi akimsihi Mungu akubariki na akuongezee maisha marefu. Hapo ninakuhakikishia kuwa ni lazima Mungu atasikia na kujibu maombi hayo, na lazima baraka za Mungu zikufuate, tena siyo wewe kuzitafuta bali zitakutafuta wewe. Kuna matajiri wengi wanadhani mafanikio waliyonayo ni jitihada zao binafsi, hapana kuna mkono wa Mungu kwa sababu wanawasaidia wenye kuhitaji na hawajui kama wale wenye uhitaji huwaombea baraka pasipo wao kujua.
Matendo ya Mitume 9:36,39 “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumuonyesha zile kanzu na nguo alizoshona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao”.
Dorkasi alikuwa ni mwanamke aishiye Yafa, ni mwanamke aliyekuwa akitoa sadaka nyingi kwa njia ya kuwahudumia wajane wa mji ule kwa kuwashonea kanzu na nguo. Bila shaka wajane wale walimuombea, na ndiyo sababu alizidi sana katika kuwahudumia, hata alipokufa wajane wale walilia sana na kumsii Petro amfanyie maombi ya kufufuliwa. Sadaka tu, ndiyo ilitosha kutenda muujiza.
Kuna nyakati mtu unapata fedha nzuri na nyingi na inakwisha kabla ya wakati. Kama ni mshahara unakwisha kabla ya kukutana na mshahara unaofuata, na huwezi kuandika au kuonesha chochote cha maana ulichofanya kwa mshahara au fedha  hiyo. Hapo nataka ujue kuwa kuna kinachosaidiana na wewe katika kutumia fedha au mali yako, ni nguvu za yule adui mwovu. Lakini iwapo ungetambua siri, kuwa ukiikabidhi mali au fedha yako kwa Mungu itakuwa salama na utafanya maendeleo yasiyo elezeka zaidi utakuwa ukishuhudia kuwa ni matendo makuu ya Mungu na ni neema zake tu.
Unaweza ukajiuliza, je nitaikabidhi vipi fedha au mali niliyonayo kwa Mungu ili iwe salama? Jibu ni jepesi sana; toa fungu la kumi katika fedha au mali unayoipata.
Malaki 3:10-11 “Leteni zaka (fungu la kumi) kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.”
Katika fungu la kumi huitaji kuomba baraka, bali unatakiwa kudai baraka zako. Hapo Mungu mwenyewe amehaidi kukubariki, ni lazima aitimize ahadi yake kwako.
Nitamkemea yeye alaye; nguvu zozote za adui hazitakuwa na nguvu tena katika kuichezea fedha na mali yako, kwani Mungu atailinda nayo itakuwa salama.
Mzabibu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake; matunda ni sawa na mali, fedha au mshahara unaoupata, utadumu hata uje ukutane na mshahara unaofuatia. Kipindi cha mavuno ya kwanza hadi yanayofuata au kipindi cha mshahara mmoja hadi mwengine ni sawa na kipindi cha mzabibu kutoa matunda uzao mmoja hadi uzao unaofuata. Katika kipindi hiki ni lazima matunda ya uzao wa kwanza yadumu hadi uzao unaofuata, hili linawezekana endapo utatoa fungu la kumi kwani Mungu ameahidi kutopukutisha mazao ya mizabibu yetu kabla ya wakati wake.
Ni zamu yako sasa, fanya upande wako na umwachie Mungu upande wake. Hakika utayaona matendo makuu ya miujiza ya Mungu, na ninakuhakikishia kuwa baraka za Mungu zitakutafuta kokote uliko  au uendako. Amina.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts