Mpendwa katika Kristo Yesu, nakusalimu kwa
Jina la Yesu.
Kabla
hatujaangalia neno la Mungu katika kitabu chake kitakatifu Biblia, ningependa
tushirikiane jambo ambalo wewe pia utakuwa shahidi wa jambo hili. Katika jamii
niliyopo au hiyo uliyopo, kuna watu wanafanya kazi kwa bidii na kujituma mchana
na usiku na wengine wanapokea mishahara mikubwa au minono kama inavyojulikana
na wengi lakini ukiyatazama maisha ya watu hawa hayafanani na mategemeo ya
wengi. Ni maisha ya kawaida sana, ambayo hata ukiyafananisha na maisha ya mtu
fulani ambaye anapokea mshahara wa kiwango cha kawaida au kiwango cha chini
huwezi kuamini. Unakuta mtu anapokea mshahara mdogo lakini ana mafanikio
tofauti na mategemeo ya wengi.
Wewe pia
unaweza ukawa miongoni mwa wengi wanaodhani unono au ukubwa wa mshahara ndiyo
mafanikio. Hapana, ipo siri katika mafanikio ya mtu yeyote, hata wewe
ukiigundua siri hiyo ni lazima ufanikiwe na utashuhudia tu matendo makuu ya
Mungu.
Siri ya
mafanikio ni kutoa, unapotoa fedha na mali zako ili kuwasaidia wahitaji, Mungu
anakubariki. Mungu atakubariki kwa sababu unapo msaidia muhitaji, hata kuripa
fedha au mali, yeye atakuombea baraka kwa Mungu, na anaweza akakesha tena kwa
machozi akimsihi Mungu akubariki na akuongezee maisha marefu. Hapo
ninakuhakikishia kuwa ni lazima Mungu atasikia na kujibu maombi hayo, na lazima
baraka za Mungu zikufuate, tena siyo wewe kuzitafuta bali zitakutafuta wewe.
Kuna matajiri wengi wanadhani mafanikio waliyonayo ni jitihada zao binafsi,
hapana kuna mkono wa Mungu kwa sababu wanawasaidia wenye kuhitaji na hawajui
kama wale wenye uhitaji huwaombea baraka pasipo wao kujua.
Matendo
ya Mitume 9:36,39 “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha,
tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema
na sadaka alizozitoa. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika wakampeleka juu
orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumuonyesha zile kanzu
na nguo alizoshona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao”.
Dorkasi
alikuwa ni mwanamke aishiye Yafa, ni mwanamke aliyekuwa akitoa sadaka nyingi
kwa njia ya kuwahudumia wajane wa mji ule kwa kuwashonea kanzu na nguo. Bila
shaka wajane wale walimuombea, na ndiyo sababu alizidi sana katika kuwahudumia,
hata alipokufa wajane wale walilia sana na kumsii Petro amfanyie maombi ya
kufufuliwa. Sadaka tu, ndiyo ilitosha kutenda muujiza.
Kuna
nyakati mtu unapata fedha nzuri na nyingi na inakwisha kabla ya wakati. Kama ni
mshahara unakwisha kabla ya kukutana na mshahara unaofuata, na huwezi kuandika
au kuonesha chochote cha maana ulichofanya kwa mshahara au fedha hiyo. Hapo nataka ujue kuwa kuna
kinachosaidiana na wewe katika kutumia fedha au mali yako, ni nguvu za yule
adui mwovu. Lakini iwapo ungetambua siri, kuwa ukiikabidhi mali au fedha yako
kwa Mungu itakuwa salama na utafanya maendeleo yasiyo elezeka zaidi utakuwa
ukishuhudia kuwa ni matendo makuu ya Mungu na ni neema zake tu.
Unaweza
ukajiuliza, je nitaikabidhi vipi fedha au mali niliyonayo kwa Mungu ili iwe
salama? Jibu ni jepesi sana; toa fungu la kumi katika fedha au mali unayoipata.
Malaki
3:10-11 “Leteni zaka (fungu la kumi) kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika
nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama
sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo
nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala
hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake
kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.”
Katika
fungu la kumi huitaji kuomba baraka, bali unatakiwa kudai baraka zako. Hapo
Mungu mwenyewe amehaidi kukubariki, ni lazima aitimize ahadi yake kwako.
Nitamkemea
yeye alaye; nguvu zozote za adui hazitakuwa na nguvu tena katika kuichezea
fedha na mali yako, kwani Mungu atailinda nayo itakuwa salama.
Mzabibu
hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake; matunda ni sawa na mali,
fedha au mshahara unaoupata, utadumu hata uje ukutane na mshahara unaofuatia.
Kipindi cha mavuno ya kwanza hadi yanayofuata au kipindi cha mshahara mmoja
hadi mwengine ni sawa na kipindi cha mzabibu kutoa matunda uzao mmoja hadi uzao
unaofuata. Katika kipindi hiki ni lazima matunda ya uzao wa kwanza yadumu hadi
uzao unaofuata, hili linawezekana endapo utatoa fungu la kumi kwani Mungu
ameahidi kutopukutisha mazao ya mizabibu yetu kabla ya wakati wake.
Ni zamu
yako sasa, fanya upande wako na umwachie Mungu upande wake. Hakika utayaona
matendo makuu ya miujiza ya Mungu, na ninakuhakikishia kuwa baraka za Mungu
zitakutafuta kokote uliko au uendako.
Amina.
No comments:
Post a Comment