Upendo wa kweli ni kumpenda mtu
yule anayekuchukia, siyo kwa sababu ya mali au vitu alivyonavyo bali kwa sababu
moyo umeamua kumpenda.
Jambo hilo
ni gumu sana kwa wengi wetu, kwani tunawapenda wanaotupenda tu na hata kukawa
na msemo unaosema “mpende akupendaye, asiyekupenda achana naye”. Tabia hii
imeingia hadi makanisani, upendo wa wapendwa wengi wa siku hizi ni kupendana
wao kwa wao tu, kusaidiana wao kwa wao tu na hata kutembeleana ni wao kwa wao
tu. Huu siyo upendo aliotufundisha Bwana Wetu Yesu Kristo, ni kosa!
Kama wewe
ni mkristo au siyo mkristo na unampenda mtu kwa sababu ana kitu au mali inayokunufaisha
kwa namna moja au nyingine, bado hauna upendo. Kwa sababu mtu huyo akiondokewa
na hicho kinachokufanya umpende, upendo wako kwake utayeyuka wote.
Upendo ni
nini?
Mathayo
5:44 “lakini Mimi (Yesu Kristo) nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowaudhi”.
Upendo ni
kuwapenda watu wote; rafiki zetu na adui zetu, na kuwaombea pia wapate mema na
siyo mabaya.
Wakristo
wa siku hizi ili wakuombee basi ni lazima yawe maombi ya kanisa kwa ujumla, au
kuwe na jambo zuri umetenda kwa manufaa na faida yao. Ukimpa zawadi ya kitu au
pesa, atakuombea Baraka hata kufunga atafunga. Lakini asipopewa kitu, mkristo
huyu hana muda wa kukuombea. Huo siyo upendo tulioagizwa na Bwana wetu Yesu
Kristo. (Luka 6:27)
Upendo huu
ni kuwapenda watu wote kama nafsi zetu; kama vile tunavyojipenda sisi wenyewe
ndivyo tuwapende na wenzetu.
Mathayo 19:19
“…mpende jirani yako kama nafsi yako”.
Kama wewe
ukilala njaa siyo kwa sababu upo katika maombi ya kufunga, bali kwa sababu
umekosa chakula utakavyoumia ndivyo uumie vile vile ukisikia jirani yako
amelala njaa pasipo kujali kuwa ni mkristo mwenzako au siyo mkristo, ni rafiki
yako au adui yako. Huu ndiyo upendo wa Yesu Kristo, tena ni amri (Marko 12:31).
Nini
faida za upendo?
Sadaka pasipo
upendo haifai kitu. Ukikosa upendo kwa jirani yako yoyote, sadaka unayoitoa
madhabahuni si kitu. Upendo unafaa kuliko sadaka unayoiona ni nono, au
inayogusa moyo wako.
Marko 12:33
“…na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa
na dhabihu zote pia”.
Kutukamilisha.
Kama jinsi Baba yetu wa Mbinguni alivyomkamilifu kwa sababu alimtoa Yesu Kristo
afe ili kutukomboa kwa sababu anatupenda, na sisi tukiwapenda wenzetu wote
tunakamilishwa kama Mungu mwenyewe alivyo mkamilifu.
Mathayo 5:45,48
“ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; Basi ninyi mtakuwa wakamilifu,
kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Pendo litawavuta
wasiomjua Mungu, wamjue Mungu. Tukiwapenda wote; wakristo na wasio wakristo,
frafiki zetu na adui zetu, tunamtambulisha Mungu wetu mwenye upendo kwa watu
wote kwao. Na kwa njia hii ya upendo huu wa dhati, tunawafanya wasiomjua Mungu
nao wamjue Mungu kupitia upendo wetu kwao.
Upendo wa
namna hii hauji ila kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na endapo umekosa
upendo huu siyo kosa kwani unaweza kuupata sasa. Yesu mwenyewe alisema, ombeni
lolote mtakalo kwa jina langu na Baba wa mbinguni atawapa. Kama umekosa upendo
aliotuagiza Yesu, omba na kwa imani Mungu wetu atakupa.
Yohana 14:13
“Nanyi mkiomba lolote (upendo) kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba
atukuzwe ndani ya Mwana”.
Mungu aliyetukuka,
mtakatifu awabariki wote.
No comments:
Post a Comment