Kutoa sadaka
kama mazoea au desturi ni kupoteza fedha au mali yako pasipo na manufaa yoyote.
Wapo wakristo ambao wamelelewa katika familia za dini na kukua wakijua ni
lazima kwenda na sadaka ibadani lakini hawajui umuhimu na matunda wanayoweza
kuyapata kwa kutoa sadaka. Wakristo wa namna hii ni kama watoto ambao wanapewa
sadaka na wazazi wao, wakitoa au wasipotoa sadaka hiyo hawaoni mapungufu yoyote,
zaidi ni faida kwao kwani watakula barafu.
Na wapo wakristo wanaotoa sadaka kama ajali, wao
huamua ni sadaka ya aina au kiasi gani watatoa muda mfupi baada ya kujianda
kwenda ibadani au hata wakiwa njiani kuelekea ibadani. Wanatoa sadaka za kushtukiza,
sadaka isiyo na maandalio yoyote.
Sadaka inapaswa kuandaliwa, hata siku moja kabla ya
kutolewa. Katika agano la kale utaona kuna siku zinapita tangu Mungu aombe
kutolewa kwa sadaka na siku ya kuitoa hiyo sadaka, aliyeambiwa atoe sadaka
anafanya maandalizi ya kuchagua sadaka nzuri ya kupendeza itakayopata kibali
machoni pa Mungu.
Sadaka utakayoitoa madhabahuni pa Mungu lazima
uitamkie jambo. Kabla sijatoa sadaka yangu huwa namwambia Mungu hivi; “maadam,
sadaka/dhabihu hii itafanya kazi shambani mwako ee Mungu wangu, fanya jambo
(ninalitaja) katika maisha yangu”.
Sadaka au dhabihu ni sawa na mbegu, ukipanda mbegu
unategemea uzune kulingana na mbegu uliyoipanda. Sadaka au dhabihu ni mbegu ya
kuvunia baraka zote za kiroho na kimwili, afya na uzima.
Zaburi 50:5 “Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu (sadaka)”.
Agano ni makubaliano yasiyovunjika, kufanya agano na
Mungu ni kujithibitishia makubaliano yako na Mungu kuwa yatatimia. Sasa unaweza
ukafanya agano na Mungu kwa kutumia dhabihu au sadaka unayoitoa katika ibada
zako, sadaka iliyoandaliwa na siyo sadaka ya kutolewa kama bahati mbaya. Agano hilo
utalifanya pale utakapo itamkia neno sadaka unayoipeleka madhabahuni pa Mungu
wako, ukitoa sadaka ambayo hukuitamkia neno utakuwa unatoa sadaka kama mtoto
asiyejua nini maana ya sadaka na inatolewa kwa sababu gani.
Siyo kila sadaka utakayoitoa na kuitamkia neno
utakuwa umefunga agano na Mungu, ni sadaka utakayoitoa kwa moyo wa kupenda tu. Kwani
sadaka utakayoitoa kwa moyo wa kupenda ndiyo sadaka itakayopata kibali machoni
pa Mungu, na agano lililofunganishwa na sadaka iliyo na kibali machoni pa Mungu
ndiyo agano litakalo timia na kufanikiwa.
Zaburi 54:6 “Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea
dhabihu”, Kutoka 25:1-2 “Bwana akanena na Musa, akamwambia, waambie wana wa
Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda
mtatwaa kwake sadaka yangu”. Kama ukijikuta unatoa sadaka au dhabihu kwa moyo
uliokunjamana tafuta msaada wa maombi haraka iwezekanavyo. Sadaka ni mbegu
unayoweza kuitumia kuvuna baraka ya aina yoyote, ndiyo maana unatakiwa kuitoa
kwa furaha na moyo mkunjufu.
Sasa kama tunakwenda pamoja, utakuwa umenielewa
hivi; unapotoa sadaka itamkie neno ili kuweka agano na Mungu kupitia sadaka
unayoitoa, ili agano lako lipate kibali cha kufanikiwa na kutimia ni lazima
sadaka iliyoambatana na agano hilo ipate kibali mbele za Mungu. Na sadaka
inayotolewa kwa moyo wa kupenda, moyo mkunjufu ndiyo sadaka inayopata kibali
mbele za Mungu.
Lakini hitimisho la hayo yote ni imani inayoambatana
na sadaka iliyotolewa kwa moyo wa kupenda na kufungamanishwa na agano.
1 Wafalme 17:10-16 “Niletee, nakuomba, kipande cha
mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate
ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota
kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia,
usiogope, enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo
ukaniletee, kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana Mungu wa
Israeli asema hivi, lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta
haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda
akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake
wakala siku nyingi”.
Hiyo ni habari ya mama mjane wa Serepta, aliyebakiwa
na unga kipimo cha kujaza mkono na mafuta kidogo katika chupa yake na bajeti
yake ilikuwa wale wamalize wafe yeye na mtoto wake. Na katika kipindi hicho
kigumu, anatakiwa kutoa sadaka ya kumtengenezea mtumishi wa Mungu, Eliya mkate.
Angeweza kukataa, lakini kwa agano (kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli asema hivi;
lile pipa la unga halitapungua, wala ile chupa ya mafuta haitaisha) lililokuwa
nyuma ya utoaji wa sadaka ile na imani aliyoijenga mjane yule kwa sababu alijua
agano lolote pamoja na Mungu ni hakika na kweli, ndiyo majibu ya baraka yake; kutopungua
kwa unga na mafuta kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Nawe mkristo, unatakiwa
ujenge imani ya kupokea kutoka kwa Mungu kupitia utoaji wako wa sadaka ya aina
yoyote.
Mungu ni mwaminifu kwa watu wake, hulitimiza agano
lake na watu wake. AMINA.
well i like it be blessed
ReplyDeleteAmen amem
ReplyDeleteSomo zuri.
ReplyDeleteIla kitu Mungu amenifundisha kuhusu utoaji;
Toa sadaka kwa Upendo na kwa moyo mkunjufu. Period.
Maana yake, Toa kwasababu unampenda Mungu na ukitoa usibebeshe madai sadaka yako, ili usije ukaingia katika jaribu la kutegemea kujibiwa eti kwasababu umetoa sadaka.
Ukitoa kwa upendo na kwa moyo mkunjufu bila kuweka agano lolote kwenye sadaka yako, Mungu hua anatoa thawabu mara zote katika utoaji wa namna hii. Huitaji kutamka chochote.
Amen!!!
ReplyDeleteWell nice preches
ReplyDelete