Sunday, November 25, 2012

FANYA AGANO NA MUNGU KUPITIA SADAKA.

   Kutoa sadaka kama mazoea au desturi ni kupoteza fedha au mali yako pasipo na manufaa yoyote. Wapo wakristo ambao wamelelewa katika familia za dini na kukua wakijua ni lazima kwenda na sadaka ibadani lakini hawajui umuhimu na matunda wanayoweza kuyapata kwa kutoa sadaka. Wakristo wa namna hii ni kama watoto ambao wanapewa sadaka na wazazi wao, wakitoa au wasipotoa sadaka hiyo hawaoni mapungufu yoyote, zaidi ni faida kwao kwani watakula barafu.

   Na wapo wakristo wanaotoa sadaka kama ajali, wao huamua ni sadaka ya aina au kiasi gani watatoa muda mfupi baada ya kujianda kwenda ibadani au hata wakiwa njiani kuelekea ibadani. Wanatoa sadaka za kushtukiza, sadaka isiyo na maandalio yoyote.

   Sadaka inapaswa kuandaliwa, hata siku moja kabla ya kutolewa. Katika agano la kale utaona kuna siku zinapita tangu Mungu aombe kutolewa kwa sadaka na siku ya kuitoa hiyo sadaka, aliyeambiwa atoe sadaka anafanya maandalizi ya kuchagua sadaka nzuri ya kupendeza itakayopata kibali machoni pa Mungu.

   Sadaka utakayoitoa madhabahuni pa Mungu lazima uitamkie jambo. Kabla sijatoa sadaka yangu huwa namwambia Mungu hivi; “maadam, sadaka/dhabihu hii itafanya kazi shambani mwako ee Mungu wangu, fanya jambo (ninalitaja) katika maisha yangu”.
   Sadaka au dhabihu ni sawa na mbegu, ukipanda mbegu unategemea uzune kulingana na mbegu uliyoipanda. Sadaka au dhabihu ni mbegu ya kuvunia baraka zote za kiroho na kimwili, afya na uzima.

   Zaburi 50:5 “Nikusanyieni wacha Mungu wangu, Waliofanya agano nami kwa dhabihu (sadaka).
Agano ni makubaliano yasiyovunjika, kufanya agano na Mungu ni kujithibitishia makubaliano yako na Mungu kuwa yatatimia. Sasa unaweza ukafanya agano na Mungu kwa kutumia dhabihu au sadaka unayoitoa katika ibada zako, sadaka iliyoandaliwa na siyo sadaka ya kutolewa kama bahati mbaya. Agano hilo utalifanya pale utakapo itamkia neno sadaka unayoipeleka madhabahuni pa Mungu wako, ukitoa sadaka ambayo hukuitamkia neno utakuwa unatoa sadaka kama mtoto asiyejua nini maana ya sadaka na inatolewa kwa sababu gani.


   Siyo kila sadaka utakayoitoa na kuitamkia neno utakuwa umefunga agano na Mungu, ni sadaka utakayoitoa kwa moyo wa kupenda tu. Kwani sadaka utakayoitoa kwa moyo wa kupenda ndiyo sadaka itakayopata kibali machoni pa Mungu, na agano lililofunganishwa na sadaka iliyo na kibali machoni pa Mungu ndiyo agano litakalo timia na kufanikiwa.

   Zaburi 54:6 “Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu”, Kutoka 25:1-2 “Bwana akanena na Musa, akamwambia, waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu”. Kama ukijikuta unatoa sadaka au dhabihu kwa moyo uliokunjamana tafuta msaada wa maombi haraka iwezekanavyo. Sadaka ni mbegu unayoweza kuitumia kuvuna baraka ya aina yoyote, ndiyo maana unatakiwa kuitoa kwa furaha na moyo mkunjufu.

   Sasa kama tunakwenda pamoja, utakuwa umenielewa hivi; unapotoa sadaka itamkie neno ili kuweka agano na Mungu kupitia sadaka unayoitoa, ili agano lako lipate kibali cha kufanikiwa na kutimia ni lazima sadaka iliyoambatana na agano hilo ipate kibali mbele za Mungu. Na sadaka inayotolewa kwa moyo wa kupenda, moyo mkunjufu ndiyo sadaka inayopata kibali mbele za Mungu.

Lakini hitimisho la hayo yote ni imani inayoambatana na sadaka iliyotolewa kwa moyo wa kupenda na kufungamanishwa na agano.

1 Wafalme 17:10-16 “Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, usiogope, enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee, kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli asema hivi, lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake wakala siku nyingi”.

   Hiyo ni habari ya mama mjane wa Serepta, aliyebakiwa na unga kipimo cha kujaza mkono na mafuta kidogo katika chupa yake na bajeti yake ilikuwa wale wamalize wafe yeye na mtoto wake. Na katika kipindi hicho kigumu, anatakiwa kutoa sadaka ya kumtengenezea mtumishi wa Mungu, Eliya mkate. Angeweza kukataa, lakini kwa agano (kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli asema hivi; lile pipa la unga halitapungua, wala ile chupa ya mafuta haitaisha) lililokuwa nyuma ya utoaji wa sadaka ile na imani aliyoijenga mjane yule kwa sababu alijua agano lolote pamoja na Mungu ni hakika na kweli, ndiyo majibu ya baraka yake; kutopungua kwa unga na mafuta kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Nawe mkristo, unatakiwa ujenge imani ya kupokea kutoka kwa Mungu kupitia utoaji wako wa sadaka ya aina yoyote.

Mungu ni mwaminifu kwa watu wake, hulitimiza agano lake na watu wake. AMINA.

5 comments:

  1. Somo zuri.
    Ila kitu Mungu amenifundisha kuhusu utoaji;
    Toa sadaka kwa Upendo na kwa moyo mkunjufu. Period.
    Maana yake, Toa kwasababu unampenda Mungu na ukitoa usibebeshe madai sadaka yako, ili usije ukaingia katika jaribu la kutegemea kujibiwa eti kwasababu umetoa sadaka.
    Ukitoa kwa upendo na kwa moyo mkunjufu bila kuweka agano lolote kwenye sadaka yako, Mungu hua anatoa thawabu mara zote katika utoaji wa namna hii. Huitaji kutamka chochote.

    ReplyDelete
  2. Well nice preches

    ReplyDelete

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts