Luka 2:1-5 “… Yusufu naye
aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa
Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbali na jamaa ya Daudi; ili
aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba”.
Ukisoma kwa makini katika mistari ya injili hiyo hapo juu
kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka; neno linatuambia kuwa Yusufu alifunga
safari yeye pamoja na Mariamu mkewe ambaye alikuwa mjamzito (mwenye ujauzito wa
Bwana wetu Yesu Kristo) kutoka mji aliokuwa anaishi wa Nazareti ulioko Galilaya
na kwenda katika mji wa Daudi yaani Bethlehemu ulioko Uyahudi. Kilichomfanya afanye
safari ile ni amri iliyotolewa na Kaisari Augusto, iandikwe orodha ya majina ya
watu wotewa ulimwengu (ambayo ilikuwa ni orodha ya kwanza kuandikwa hapo
Kirenio).
Hiyo ilikuwa ni sensa
inayofanana na hii tunayoifanya wananchi wa Tanzania kwa mujibu wa katiba kila
baada ya miaka kumi, ili kuijua idadi yetu na hivyo kuipa urahisi serikali yetu
katika mipango yake ya maendeleo kwa sekta mbali mbali za kijamii kama afya,
elimu, miundombinu n.k. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wakiihususha shughuli
hii na ushirikina na wapo ambao wamekuwa wakiipinga kwa sababu zao binafsi
aidha za kimaslahi au kisiasa. Kwa mkristo yoyote kukataa kuhesabiwa kwa
kujishawishi yeye mwenyewe au kwa ushawishi wa mtu mwengine yoyote ni kwenda
kinyume na neno la Mungu na hivyo ni kosa kama kuivunja amri yoyote ya Mungu,
kama biblia inatuonesha Yusufu na mkewe Mariamu walihesabiwa na wewe hutaki
kuhesabiwa ni kosa.