Nakusalimu mpendwa katika Bwana
na Mwokozi wetu Yesu Kristo
Utangulizi
Siku ya leo, Mungu anatufundisha
somo lenye kichwa, “Nguvu ya mwanamke aombaye”. Ni maombi yangu Mungu afungue
ufahamu na uelewa wako ili tunapokwenda kumaliza somo letu la leo, kuwe kuna
kitu kipya kimejengeka na kuimarika katika fahamu zetu. Kitu ambacho
hakitatuacha kubaki kama tulivyokuwa mwanzo, wote wanaume kwa wanawake. Wanaume
tutajifunza nguvu walizonazo wanawake katika ulimwengu wa kiroho na namna Mungu
anavyothamini, sikiliza na kujibu maombi yao. Wanawake watajifunza nguvu
waliyonayo ndani ya Yesu Kristo, kupitia nguvu hiyo watavikwa utu mpya wa
kujithamini na kufanya mambo makubwa katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa
macho ya damu na nyama.
Jamii karibu zote ulimwenguni
zimemchukulia mwanamke kama kiumbe duni na dhaifu, kiumbe kinachostahili
kutendewa ubaya wowote. Na hivyo ndivyo mwanamke alivyoaminishwa kuwa na
kujichukulia. Katika kujikomboa kutoka dhana nzima ya mfumo dume, mwanamke
anafanya kampeni za kutafuta haki sawa na mwanaume. Kutafuta haki sawa kati ya
mwanamke na mwanaume siyo suluhu sahihi ya kumkwamua mwanamke. Suluhu sahihi ni
mwanamke kuitambua nafasi yake mbele za Mungu na namna Mungu alivyomthamini mwanamke
tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Pili, mwanamke kutambua wajibu wake sahihi
kwa mwanaume. Tatu, mwanaume atambue nafasi ya mwanamke katika kumuimarisha
maisha yake ya kiroho, kijamii na kiuchumi.
Mwanamke ni nani?
“Bwana analitoa neno lake (na
kusema), wanawake watangazao habari ni
jeshi kubwa”, Zaburi 68:11. Kwa mujibu wa Biblia takatifu, kutangaza habari
ni kulihuburi neno la Mungu au Yesu Kristo. Habari njema za Yesu Kristo
zinatangazwa mahali kote, sehemu yoyote na wakati wowote. Asilimia kubwa ya
wanawake, asiyeko na aliyeko ndani ya ndoa ni mtangaza habari njema za Mungu na
Yesu Kristo, wengine pasipo hata wao wenyewe kujua. Ndiyo, unaweza kuwa
unatangaza habari njema za Mungu na Yesu Kristo pasipo kujijua. Twende pamoja
sasa kumtambua mwanamke ni nani kupitia 4M; msaidizi, mzazi, mlezi na mlinzi. Kupitia
4M utatatmbua namna mwanamke anavyoweza kutangaza habari njema za ufalme wa
Mungu.
Msaidizi
Mwanzo 2:20b na 18, “…..lakini
hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akasema, si vema
huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye”. Mwanamke ni
msaidizi wa mwanaume, siyo msaidizi tu, ni msaidizi wa kufanana na mwanaume.
Kufanana maana yake ni kuwa na viwango vinavyokaribiana katika ubora na nafasi.
Fundi ujenzi wa nyumba hawezi kutafuta msaidizi mwenye ujuzi wa kutengeneza
magari, ni lazima atatafuta msaidizi mwenye uwezo wa ujenzi wa nyumba. Hivyo
basi mwanamke ni sawa na mwanaume mbele za macho ya Mungu. Hakuna aliye bora
zaidi ya mwingine, si mwanume wala si mwanamke. Mbele za macho ya Mungu, sote
tuna nafasi sawa. Mwanamke jithaminishe sawa na mwanaume, ndivyo Mungu
anavyotuona. Mwanaume mthamini mwanamke kwa maana ameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu (Mwanzo 1:26). Ukimuona mwanamke, ona utukufu wa uumbaji wa Mungu sawa na
ule unaouona kwako. Siku zote za maisha yako mwanamke fanya majukumu yako kwa
mwanaume ukimpendeza Mungu, hii ndiyo injili sahihi ikupasayo kuliko hata ile
ya madhabahuni ilihali hautimizi wajibu wako kwa mumeo impendezavyo Mungu.