YESU KRISTO ASIFIWE!
Ashukuriwe Mungu aliyetupa kibali cha mimi na wewe msomaji
wangu kukutana leo ikiwa ni kwa mara ya kwanza au kwa mara nyingine tena. Leo
tuna somo lenye kichwa kisemacho “UNAWEZA KUWA UNATEMBEA CHINI YA
LAANA PASIPO WEWE MWENYEWE KUJUA”, katika somo hili tutaangalia kwa undani
mambo yafuatayo:-
- Maana ya laana.
- Laana inaletwa/sababishwa na nani?
- Kwa nini ulaaniwe?
- Je, unaweza kuwa umelaaniwa pasipo wewe kujua?
- Ni vitu gani vinaweza kulaaniwa?
- Kuvunja laana na mikosi, kuomba baraka za Mungu (Yehova).
Hili ni somo zuri sana ambalo ukilifuatilia kwa ukaribu
zaidi na ukijenga imani kwa Mungu kuna vitu (laana), Mungu anakwenda kuzivunja,
kuzifuta na kuziharibu (1 Yohana 3:8) na kuyabadilisha maisha yako kabisa.
Unakwenda kuishi maisha ya baraka na ushindi, nakuhakikishia lazima
utazishuhudia baraka za Mungu katika maisha yako baada ya kumaliza somo hili.
Maana ya laana.
Laana ni bahati mbaya au maneno mabaya ya maapizo
yanayotamkwa kumuelekea mtu fulani yeye mwenyewe au kitu fulani kinachomuhusu,
kwa mfano; kazi, shamba, watoto, masomo n.k kwa makusudi ya kumdhuru mtu huyo
au kitu kinachomuhusu. Kwa kifupi laana ni kinyume cha baraka.
Laana inaweza ikasababishwa kwa makusudi maalumu (mfano: laana
ambayo ni matokeo ya dhambi za wanadamu) au pasipo kujua (mfano: laana ya
kujitamkia sisi wenyewe), kwa njia zote hizi mbili laana inafanya kazi iwe kwa
makusudi au pasipo kujua.
Laana, ili itende kazi ni lazima iwe imeunganishwa na nguvu
fulani zisizo za kawaida, nguvu za ziada “supernatural powers”, nguvu hizo ni lazima ziwe zinazidi nguvu za
mtu au kitu kinacholaaniwa. Nachomaanisha hapa ni kwamba, mdogo hawezi kumlaani
mkubwa; shetani hawezi kumlaani Mungu, na mtu aliyesimama katika kweli na haki
ya Mungu hawezi kulaaniwa na shetani kutokana na ile nguvu ya Mungu iliyomo
ndani yake.
Kwa maana hiyo, kwa maneno yetu wenyewe au ya watu wa karibu
nasi na matendo ya maisha yetu ndiyo sababu kubwa ya laana katika maisha yetu
na vizazi vyetu vijavyo. Kwa sababu kila tunachokitamka na tunachokitenda
kinafuatiliwa kutimilizwa na falme mbili tofauti; ufalme wa Mungu na ufalme wa
shetani. Ni hakika na kweli, ufalme wa shetani hufuatilia hasa mambo ambayo ni hasi kuyatimiliza katika maisha yetu,
kuwa mwangalifu sana.