Saturday, June 22, 2013

MAOMBI YENYE KIBALI NA NGUVU MBELE ZA MUNGU. (SEHEMU YA KWANZA).



YESU KRISTO ASIFIWE!

Mpendwa msomaji wangu, siku ya leo tunaanza semina yetu ya mtandaoni ambayo tutatembea nayo kwa muda wa wiki zisizopungua tatu. Tafadhari jitahidi usikose sehemu hata moja ya somo letu lenye kichwa kisemacho “MAOMBI YENYE KIBALI NA NGUVU MBELE ZA MUNGU”.

Katika kipindi hiki cha semina hii tutakuwa tukiangalia maombi kwa jicho la tofauti, na ninakusihi ndugu msomaji wangu tegemea kukuta na Mungu katika kipindi hiki. Mungu mwenyewe atakwenda kukuhudumia, na hakika utapokea kitu kipya.

Kufikia kumalizika kwa somo hili tutakuwa tumejifunza vitu vifuatavyo:-

1. Maana ya maombi. 

2. Faida za maombi.

3. Vitu vya kuzingatia uwapo katika maombi. 

4. Aina kuu za maombi na faida zake.
  •      Maombi kabla.
  •      Maombi baada. 
  •         Maombi ya kawaida.
  •      Maombi ya kufunga.
5. Aina za maombi.


  • Maombi ya Roho Mtakatifu.
  • Maombi ya kufunga na kufungua.
  • Maombi ya kusukuma.
  • Maombi kwa adui.
  •  Maombi ya ushirika.
  •  Maombi kwa wengine.
  •  Maombi ya sifa.
  •  Maombi ya shukrani.

6    6. Kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu na sababu za kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu.



 Maana ya maombi.

Ni hitaji au tamanio la moyo wa mwanadamu ambalo yeye mwenyewe hawezi kujitosheleza, hivyo basi anahitaji msaada kutoka nje. Maombi ni moja ya silaha yenye nguvu sana katika ulimwengu wa roho; silaha inayoweza kuziharibu kazi za shetani, silaha inayoweza kufanya yasiyowezekana yawezekane.

Waefeso 6:11-13. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

Kama neno la Mungu linavyotuambia, hatushindani kwa damu na nyama; bali tunashindana na falme na mamlaka, wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya. Moja kwa moja vita hivi havihitaji mwili kama mwili na silaha zionekanazo kwa macho ziingiie kupambana, kwa sababu vitu hivi haviwezi kuingia katika ulimwengu wa roho. Kwa hiyo inahitajika silaha inayoweza kuingia katika ulimwengu wa roho ilihali mpiganaji amevaa mwili wa damu na nyama. Nielewe, wote tunatambua ya kwamba tuna miili ya damu na nyama na wakati huo tuna roho, miili ya damu na nyama itakapokufa tutaishi katika roho, sasa hauhitaji kufa iliueweze kupigana katika ulimwengu wa roho dhidi ya shetani.

Ukiwa bado unaishi na mwili wa damu na nyama, bado unaweza kupigana vita dhidi ya falme za giza na majeshi yake, sasa silaha pekee unayoweza kuitumia ili kupigana vita hiyo, silaha ambayo inapenya katika ulimwengu wa roho na kuharibu kazi za shetani na kuyasulubu na kuyapa kipigo mapepo ni maombi pekee. Silaha nyingine zinakulinda wewe na uvamizi wa ufalme wa giza na majeshi yake, lakini hazikufanyi wewe upigane na ufalme wa giza na kuushinda. Ni maombi peke yake.

Marko 9:28-29. Hata alipoingia nyumbani (YESU KRISTO), wanafunzi wake wakamuuliza kwa faragha, mbona sisi hatukuweza kumtoa (pepo bubu na kiziwi)? Akawaambia, namna hii haiwezi kutoka (vita hii hamuwezi kuipigana) kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.

Yesu Kristo mwenyewe anatuthibitishia katika mistari ya Biblia hapo juu kwamba, kuna vita nyingine hatuwezi kupigana na kushinda pasipo maombi. Ni lazima tuwe waombaji ili tuweze kuzishinda vita za namna hiyo, vita dhidi ya ulimwengu wa roho.


Vitu vya kuzingatia katika maombi.
  
Kabla hujaingia kufanya maombi na wakati ufanyapo maombi lazima uzingatie mambo yafuatayo;
  • Mahali au sehemu ya kufanyia maombi. Chagua sehemu yenye utulivu, isiyo na kelele na shughuli za wanadamu, ambapo unaweza kumtafakari Mungu na kuongea naye kwa urahisi zaidi. Unapokuwa sehemu yenye kelele na shughuli za wanadamu, ufahamu wako unashindwa kuzama zaidi katika kumtafakari Mungu. Sehemu nzuri unayoweza kufanya maombi kwa utulivu zaidi ni kanisani au mlimani. Ukiangalia mitume wa zamani na watumishi wa Mungu wa sasa wenye nguvu ni wale wanaojitenga na wanadamu wanapotaka kufanya maombi. Mathayo 8:1-2, Mathayo 26:36-39, Luka 6:12, Walawi 25:1, Kutoka 34:1-4.
  •  Muda wa kufanya maombi. Muda mzuri wa kufanya maombi ni wakati wa usiku, kwa sababu ni wakati tulivu na vita vinapiganika kwa ushindi zaidi.
  • Muda wa kudumu katika maombi. Huu ni urefu wa maombi yako; kwa mfano unafanya maombi ya kufunga labda masaa 12 halafu unaomba nusu saa au saa moja kutwa nzima, au unafanya maombi ya masaa 24 halafu unaomba masaa mawili au matatu, hakika hapo huna unachokifanya bali umeamua kushinda njaa, hayo ni maombi ya kawaida. Kama umefunga masaa 12, angalau fanya maombi kwa muda usiopungua masaa manne na kama umefunga masaa 24 angalau ufanye maombi yasiyopungua masaa nane.
  • Utakatifu. Unapoanza kufanya maombi lazima utubu makosa yako yote kwanza ndipo uanze kupeleka hoja zako mbele za madhabahu ya Mungu. Ni lazima utubu kwa sababu Mungu anasema maombi ya wenye dhambi ni kelele mbele zake, na maombi ya mwenye haki ni kama manukato. Kwa hiyo Mungu hawezi kusikiliza kelele (maombi ya mwenye dhambi), bali hupendezwa na harufu nzuri ya manukato (maombi ya mwenye haki). Isaya 59:1-2, Ufunuo 5:8, Mithali 15:8, 29, Zaburi 34:15, Yohana 9:31.
  • Imani. Ni mkono wa kupokelea majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu, huwezi kupokea majibu ya maombi yako kama huna imani. Luka 11:24, Luka 9:2, Mathayo 17:19-20, Yakobo 5:15.
  • Usifanye maombi ya kujiinua au kujisifu.  Siku zote Mungu anapendezwa na mioyo iliyoshuka, mioyo inayonyenyekea. Moyo wa kujiinua ni chukizo mbele za Bwana. Luka 18:11-14.
  • Tunaomba kupitia Jina la Yesu Kristo. Ukiwa umejitakasa na umeambatanisha imani, ukilitumia Jina la Yesu Kristo hakika utayaona matokeo ya maombi yako. Hatuna jina jingine tuliloagizwa kulitumia katika maombi yetu, ni Jina la Yesu Kristo pekee. Yohana 14:13-14, Yohana 15:16.
  • Usilalamike, peleka hoja mbele za Mungu. Kuna baadhi ya watu wanapofika mbele za Mungu kwa ajili ya kuomba, badala ya kuomba wanaishia kulalamika. Kwa mfano umefikwa na ugonjwa, usilalamike bali muulize Mungu nini makusudi ya ugonjwa huo? Na mwambie kuwa unataka kupona, ili uendelee kuifanya kazi yake ambayo inasimama kwa sababu ya ugonjwa uliokupata. Unapopata nafasi ya kusimama mbele za Mungu, hakikisha unaongea hoja zenye nguvu na siyo unatoa lawama tu, Mungu hajawahi kujibu lawama za mtu hata siku moja. Isaya 43:26, Habakuki 2.
  • Kuna maombi hayaendi pasipo sadaka. Hapa ni lazima uwe makini kumsikiliza Mungu, unaweza ukawa umeombea jambo moja kwa muda mrefu halafu hupati majibu, huenda Mungu anasema na wewe kwa habari ya kumtolea sadaka lakini unashindwa kumuelewa. Mungu anaweza akasema na wewe kwa sauti ndani ya moyo wako uwapo katika maombi, ama akasema na wewe kupitia watumishi wake. Yona 2:1 na 9-10, hapa ni maombi ya Yona ndani ya tumbo la samaki, licha ya kuomba maombi marefu yule samaki hakumtapika Yona, lakini katika mstari wa 9, Yona alisema nitatoa sadaka an kuziondoa nadhiri zangu, Biblia inasema, Mungu akasema na yule samaki naye akamtapika Yona. Kwa hivyo, kuna maombi yanasukumwa na sadaka. Ukitaka kubalikiwa kwa habari ya mwili, toa fungu la kumi (zaka). Malaki 3:10-12.
  • Uvumulivu. Uombapo, mngoje Bwana akupe majibu sahihi kwa wakati sahihi. Kuna watu wamepokea majibu yasiyokamilika kwa sababu ya kukosa uvumilivu. Bwana anajua unatakiwa kupewa nini kwa wakati gani, ukiwa umefanya kwa sehemu yako ya kuomba, hapo mngojee Bwana naye afanye kwa sehemu yake, kukujibu. Zaburi 40:1, Warumi 8:25, Waebrania 6:15.



 Faida za maombi.

Njia ya kumjulisha Mungu haja za mioyo yetu. Tunapokuwa na mahitaji ya kiroho na kimwili mbele za Mungu, hatuwezi kumtuma mtu atupelekee hizo haja zetu mbinguni, bali tunazipeleka sisi wenyewe mbele za Mungu kwa njia ya maombi. Isaya 43:26, Isaya 1:18, Wafilipi 4:6.

Kupitia maombi, Mungu huongea nasi kwa njia ya maono au sauti ya wazi mioyoni mwetu. Matendo ya Mitume 10:9-15, hapa ni wakati Mungu anasema na Petro kwa habari ya mtumishi wake Kornelio. Mungu aliongea na Petro kwa njia ya maono wakati Petro alipokuwa katika maombi.

Maombi ni jibu la kila kitu. Maombi yakisindikizwa na vitu kama; utakatifu, imani na sadaka, hutoa jibu la kila jambo. Hufungua vifungo vya shetani, huponya magonjwa, huinua walemavu na hata magonjwa sugu na yasiyo na tiba hupata kupona. Mathayo 21:22.

Maombi hutufanya tukue kiroho. Tunapoongea na Mungu, na anapotufunulia siri za ufalme wake tuwapo katika maombi, na imani yetu inapokuwa kupitia matendo ya Mungu yatokanayo na maombi yetu, tunakuwa kiroho. Mathayo 17:14-21.


Huu ndiyo mwanzo wa somo letu zuri, ambalo nina hakika litakubariki. Wajulishe na wenzako ili nao wabarikiwe. "Share" na "like" somo hili katika ukurasa wako wa facebook na twitter ili uwabariki marafiki zako. Mungu akubariki sana, tukutane tena jumapili, tarehe 30/06/2013.

8 comments:

  1. asante kwa darasa zuri na Mungu azidi kukubariki

    ReplyDelete
  2. nashukuru Mungu kwa ujumbe na mafundisho uliyotoa kwa Sehemu I na II Mungu akubariki sana

    ReplyDelete
  3. Namshuru mungu kwa maombi aya

    ReplyDelete
  4. Asante kwa somo nzuri

    ReplyDelete
  5. Nashukur Kwa somo kuhusu maombi

    ReplyDelete

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts