Maana ya swali “unadhani wewe nani?”
Unadhani wewe nani ni aina ya
swali linalokusudiwa kumkejeli ama kumdharau anayeulizwa likiambatana na
kumnyooshea au kutomnyooshea kidole. Swali hili huelekezwa kwa anayekejeliwa
ama dharauliwa kwa minajili ya kumshusha kiuwezo wa ufanisi wa jambo. Mara nyingi
watu wanaoogopa uwezo wa mtu mwingine mfano katika mashindano hututmia swali
hili ili kudhoofisha upande pinzani. Watu wasiojitambua uwezo wao mara nyingi
hubabaishwa na swali hili.
Unadhani wewe nani? Swali hudhamiria
kumchanganya anayeulizwa na kujiona hafai au hana thamani mbele za muulizaji. Kwa
mfano, unaweza kumueleza mtu Fulani malengo yako makubwa unayotegemea
kuyatimiza na hata ukamuomba msaada wa kimawazo ili kukupa nguvu zaidi ya
kutimiza ndoto zako hizo. Badala ya kukuwezesha kimawazo na mtazamo mtu huyo
anakuuliza, “unadhani wewe nani?” utimize mambo makubwa haya, wengi wamejaribu
wameshindwa itakuwa wewe? Ama mtu anaamua kukukatisha tu tamaa kwa sababu
anaamini utakapofanikiwa utafanyika kikwazo katika biashara zake. Kwa hiyo njia
pekee ya kujiepusha na changamoto ya ushindani huo ni kukuwekea vikwazo vya
kutofanikiwa ikiwamo kukufanya ujione hauwezi, haustahili na huna thamani ya
kufanikiwa.
Kwanini watu huchagua kuwa wakatisha tamaa na kuvunja moyo?
Wakatisha tamaa huchagua kuwa hivyo
kwa manufaa yao binafsi, kwa sababu wanatamani wao peke yao ndio wapate mema tu
siku zote wakati wengine wakitaabika. Wakatisha tamaa huamaini wanapowasaidia
wengine kuinuka na kufanikiwa itawafanya wao kushika na kufilisika, ndiyo
sababu hawachagua kumsaidia ama kumtia moyo mtu yoyote ili afanikiwe. Huona raha
kuwaona wengine wakifeli na kutaabika.
Wakatisha tamaa ni sawa na
wachawi. Mara nyingine huamua kumshusha aliyeko juu ama kumfilisi aliyekwisha
fanikiwa. Watu wanapofeli, wanapoanguka na kushindwa kusonga mbele katika mambo
mbali mbali, hiyo ndiyo furaha ya wakatisha tamaa.
Kupambana na wakatisha tamaa
Huna haja ya kupambana na
mkatisha tamaa yoyote katika maisha yako, wameamua kuishi na kuwa hivyo. Unapokatishwa
tamaa usione kama kikwazo cha kukufanya usonge mbele, ona kama fursa ya kukupa
uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya hata uliyoyakusudia kwanza. Mtu anapokukatisha
tamaa siyo kwa sababu nyingine isipokuwa ameona mafanikio na kung’ara zaidi
katika maisha yako. Unapoamua kupambana na wakatisha tamaa wako, unapoteza muda
wako na muelekeo wako kimaisha. Waache wapambane kushindana nawe na kamwe
hawatashinda.
Usipoteze muda kushindana na
mwanadamu anayekukatisha tamaa. Muoneshe uwezo wako kwa vitendo katika
kufanikisha yale anayokukatisha tamaa na ikiwezekana fanikisha na ziada.
Hakuna nguvu itakayosimama kinyume nawe ikashinda
Hakuna nguvu itakayoshindana nawe
ikashinda endapo utajitambua na kuujua uwezo ulioumbiwa. Wewe ni kiumbe wa
ajabu na pekee uliyeumbiwa uwezo wa kufanikisha jambo lolote pasipo kumtegemea
mwanadamu endapo tu utasimama imara katika kumtegemea Mungu. Mungu amekuumba
kwa mfano wake. Kuyatambua haya haitoshi kukupa nguvu za kusimama na kusonga
mbele katika ya vikwazo wa wakatisha tamaa? Kama haitoshi, soma mstari ufuatao,
“Tuseme nini basi? Mungu akiwa upande wetu nani aliyekinyume chetu akashinda?”
tafsiri kutoka Biblia takatifu, Warumi 8:31. Hakuna mwanadamu, hakuna maneno
yoyote ya kulaani, hakuna nguvu zozote zinazoweza kusimama mbele yako na
kukushinda endapo Mungu atakuwa upande wako. Jiamini katika uwezo Mungu
alikuumba nao na umuamini Mungu, hakika hakuna litakaloweza kukuzuia
kufanikisha jambo lolote linalompendeza na kumpa utukufu Mungu.
No comments:
Post a Comment