Nakusalimu mpenzi msomaji wangu, Jina la Yesu Kristo
lisifiwe.
Leo napenda kuanza na hadithi kwa ufupi sana,
Ninaishi katika jamii ya wafugaji ambao hutegemea malisho ya
mifugo yao; ng’ombe, mbuzi na kondoo katika majani yaotayo kondeni na
vichakani. Wengi wa wafugaji hawa wanamiliki idadi kubwa ya mifugo, hivyo
huwalazimu kutoka na mifugo yao kila siku kwenda kutafuta malisho na maji.
Vijana wa kiume wa umri wa kati, huamka mapema asubuhi, hutoa mifugo katika
mazizi yao, huiswaga na kuiongoza mifugo hii sehemu yalipo malisho mazuri na
maji. Kila ifikapo jioni, hufanya kama walivyofanya asubuhi, huiswaga na
kuiongoza mifugo yao kuirudisha mazizini mwao. Wafugaji hawa wanaotembea na mifugo
yao kwa lengo la kutafuta malisho na maji huitwa wachungaji.
Wachungaji hawa hukaa nyuma na kuitanguliza mifugo yao mbele
kwa lengo la kuweza kuiangalia isitawanyike na kufanya uharibifu wa mazao na
mazingira wawapo njiani kuelekea malishoni ama kurudi mazizini. Katika kundi la
mifugo isiyopungua hamsini, mifugo iliyotangulia mbele huchoka kutokana na
safari ya mwendo mrefu kwenda na kurudi kutafuta malisho, hivyo hupunguza
mwendo kasi wa kutembea. Mifugo iliyotangulia mbele ikipunguza mwende kasi wa kutembea,
huilazimu mifugo yote inayofuata pamoja na mchungaji kupunguza mwendo kasi.
Mara tu mwendo kasi wa kutembea unapopungua mchungaji huichapa mifugo iliyo
karibu naye, mifugo ya nyuma, ili iweze kuongeza mwendo pasipo kujali kuwa
mifugo iliyo mbele ndiyo inayopunguza mwendo hivyo basi mifugo ya mbele ndiyo
ilistahili kuchapwa.
Mifugo ya nyuma iliyochapwa huanza kukimbia na kuisukuma mifugo
ya mbele, ambayo hukumbuka, kumbe tumepunguza mwendo, na kuanza kukimbia pia
ili kuongeza mwendo. Mifugo ya mbele inajisahau kutunza mwendo kasi, inaanza
kutembea taratibu, ili kukumbushwa kuongeza mwendo kasi, inachapwa mifugo ya
nyuma ambayo siyo sababu ya kupungua kwa mwendo kasi. Mara baada ya kuchapwa,
huikumbusha mifugo ya mbele kuongeza mwendo kasi, na mara mwendo kasi
unaongezeka. Hayo ndiyo maisha ya kila siku ya mifugo inayobaki nyuma katika
msafara wa kwenda ama kurudi malishoni. Hupokea kipigo kisicho na sababu.
Tujifunze nini katika hadithi ya leo? Hadithi ya leo
inatufundisha mambo makubwa matatu; 1. Changamoto ni lazima 2. Usilalamikie
changamoto 3. Kabiliana na changamoto.