Nakusalimu mpenzi msomaji wangu, Jina la Yesu Kristo
lisifiwe.
Leo napenda kuanza na hadithi kwa ufupi sana,
Ninaishi katika jamii ya wafugaji ambao hutegemea malisho ya
mifugo yao; ng’ombe, mbuzi na kondoo katika majani yaotayo kondeni na
vichakani. Wengi wa wafugaji hawa wanamiliki idadi kubwa ya mifugo, hivyo
huwalazimu kutoka na mifugo yao kila siku kwenda kutafuta malisho na maji.
Vijana wa kiume wa umri wa kati, huamka mapema asubuhi, hutoa mifugo katika
mazizi yao, huiswaga na kuiongoza mifugo hii sehemu yalipo malisho mazuri na
maji. Kila ifikapo jioni, hufanya kama walivyofanya asubuhi, huiswaga na
kuiongoza mifugo yao kuirudisha mazizini mwao. Wafugaji hawa wanaotembea na mifugo
yao kwa lengo la kutafuta malisho na maji huitwa wachungaji.
Wachungaji hawa hukaa nyuma na kuitanguliza mifugo yao mbele
kwa lengo la kuweza kuiangalia isitawanyike na kufanya uharibifu wa mazao na
mazingira wawapo njiani kuelekea malishoni ama kurudi mazizini. Katika kundi la
mifugo isiyopungua hamsini, mifugo iliyotangulia mbele huchoka kutokana na
safari ya mwendo mrefu kwenda na kurudi kutafuta malisho, hivyo hupunguza
mwendo kasi wa kutembea. Mifugo iliyotangulia mbele ikipunguza mwende kasi wa kutembea,
huilazimu mifugo yote inayofuata pamoja na mchungaji kupunguza mwendo kasi.
Mara tu mwendo kasi wa kutembea unapopungua mchungaji huichapa mifugo iliyo
karibu naye, mifugo ya nyuma, ili iweze kuongeza mwendo pasipo kujali kuwa
mifugo iliyo mbele ndiyo inayopunguza mwendo hivyo basi mifugo ya mbele ndiyo
ilistahili kuchapwa.
Mifugo ya nyuma iliyochapwa huanza kukimbia na kuisukuma mifugo
ya mbele, ambayo hukumbuka, kumbe tumepunguza mwendo, na kuanza kukimbia pia
ili kuongeza mwendo. Mifugo ya mbele inajisahau kutunza mwendo kasi, inaanza
kutembea taratibu, ili kukumbushwa kuongeza mwendo kasi, inachapwa mifugo ya
nyuma ambayo siyo sababu ya kupungua kwa mwendo kasi. Mara baada ya kuchapwa,
huikumbusha mifugo ya mbele kuongeza mwendo kasi, na mara mwendo kasi
unaongezeka. Hayo ndiyo maisha ya kila siku ya mifugo inayobaki nyuma katika
msafara wa kwenda ama kurudi malishoni. Hupokea kipigo kisicho na sababu.
Tujifunze nini katika hadithi ya leo? Hadithi ya leo
inatufundisha mambo makubwa matatu; 1. Changamoto ni lazima 2. Usilalamikie
changamoto 3. Kabiliana na changamoto.
Changamoto ni lazima
Mpenzi msomaji ninapenda kukujulisha kuwa, katika maisha ili
mradi upo hai unaishi, huna budi kukutana na changamoto katika hatua moja ama
nyingine ya maisha yako. Ni lazima ukutane na changamoto, kwa kusababisha
mwenyewe ama kwa kusababishiwa. Ndiyo, zipo changamoto tunazipitia kwa sababu
tu kwa namna moja ama nyingine tumezisababisha wenyewe. Pia zipo changamoto
ambazo zinatupata katika maisha kama matokeo ya makosa ya watu wengine. Katika
hadithi yetu, ng’ombe waliopo nyuma wanachapwa kwa sababu ya kutembea taratibu
lakini wanaosababisha mwendo wa taratibu ni ng’ombe waliopo mbele. Je,
changamoto ni nini? Changamoto ni hali yoyote ya kiuchumi, kijamii, kimahusiano
ama kielimu inayokuwekea kizuizi cha kusonga mbele na mara zote kizuizi hiki
huumiza na huweza kukufanya ukate tamaa na kujiona haustahili.
Usilalamikie changamoto
Unapokumbwa na changamoto ya aina yoyote ile, usilalamike,
kulalamikia changamoto ni sumu kali sana katika maisha. Kumbuka hadithi yetu,
ng’ombe wa nyuma wanapochapwa kwa kosa la ng’ombe wa mbele kutembea taratibu,
hawamgeukii mchungaji na kuanza kumlaumi kwa kuwachapa kwa kosa lisilo lao.
Unaporuhusu kuilalamikia changamoto iliyokukabili kwa sababu imesababishwa na
mtu mwingine (unajiona umeonewa, haukustahili), unapoteza uwezo na nguvu za
kuitatua. Ukiisha kupoteza uwezo na nguvu za kutatua changamoto inayokukabili,
unakuwa si mshindi tenda dhidi ya changamoto hiyo. Hatua inayoufuata ni KUKATA
TAMAA. Ukikata tama, unapoteza muelekeo na mustakabali mzima wa maisha yako.
Kabiliana na changamoto inayokukabili
Dawa ya changamoto yoyote ile inapokukabili, ni kukabiliana
nayo kwa lengo moja kubwa, kuitatua na kuimaliza kabisa. Katika hadithi yetu
tunaona ng’ombe walio nyuma (wasiopungua watatu hadi watano) wanapochapwa
hukimbia kusonga mbele kulikabili kundi kubwa la ng’ombe (kuanzia hamsini)
waliopo mbele yao na kuwafanya waanze kukimbia ili kuongeza mwendo kama
atakavyo mchungaji. Mchungaji ni sawa na maisha, siku zote maisha yanataka
mchaka mchaka, wewe ni sawa na ng’ombe aliyeko nyuma, changamoto za maisha ni
ng’ombe waliopo mbele. Maisha yanapokupa changamoto, kabiliana nazo ili
uzitatue. Jambo la muhimu, usiache changamoto haijamalizika kutatuliwa. Ni kosa
kubwa sana.
Mpango kazi wa kutatua changamoto
Sasa tuangalie mpango kazi wa Kibiblia wa kukabiliana na
kutatua changamoto. Rejea mistari michache ya Biblia katika kitabu cha Luka 9:10-17.
Wafuasi wa Yesu Kristo walipompelekea habari ya kuwaruhusu waondoke wale
makutano, walikuwa wanafanya kitu kifuatacho, kuwasilisha changamoto (watu wanaozidi
5000 nyikani pasipo chakula) inayomkabili Yesu pamoja na ufumbuzi wa hiyo
changamoto (kuwaruhusu waende vijiji vya jirani kutafuta chakula). Ufumbuzi
waliouwasilisha wafuasi wa Yesu haukuwa sahihi, endapo Yesu angewaruhusu
makutano wale kwenda vijiji vya jirani majira ya jioni kuelekea usiku wangeumia
njiani na wengine wangezimia kwa safari ndefu ya kwenda kutafuta chakula wakiwa
na njaa kali.
Katika masimulizi hayo tunajifunza mambo makuu matatu kutoka
kwa Yesu Kristo; 1. Utulivu 2. Kushukuru 3. Kukabili na kutatua changamoto.
Utulivu
Yesu Kristo alipopokea changamoto yake hakuifanya kuwa
habari ya mjini, masimulizi na malalamiko kwa kila aliyekutana naye. Hili ni
kosa ambalo wengi tunalifanya, tunapopatwa na changamoto tuanza kuilalamikia
huku tukiifanya ni habari ya mjini kuitangaza katika kila mbao za matangazo
tunazokutana nazo. Jifunze kwa Yesu, unapopatwa na changamoto tuliza moyo na
akili, endapo utaona huwezi (unahisi kuchanganyikiwa), jipe nafasi ya utulivu
huku ukitafari mambo mengine yasiyohusiana kabisa na changamoto inayokukabili.
Jaribu kufanya mambo yatakayo kufariji na kukupa furaha kwa wakati huo hadi
pale utakapojiona upo tayari kuikabili na kuitatua changamoto iliyopo mbele
yako. Kujipa muda ili upate utulivu wa moyo na akili ili kuikabili changamoto
yako kunakupa nguvu na uwezo wa kufiriki njia sahihi ya utatuzi ili kuimaliza
kabisa changamoto iliyopo mbele yako. Endapo utathubutu kutatua changamoto
yoyote katika hali ya hofu na mashaka (pasipo utulivu), matokeo ya utatuzi huo
hayatakuwa sahihi wala ya kudumu.
Kushukuru
Kuna nyakati tunajipata uwezo wetu wa kutatua changamoto
zetu ni mdogo kuliko ukubwa wa changamoto, nyakati kama hizi tunapaswa
kushukuru Mungu kwa kuachilia changamoto zitupate. Usilaumu, usimlaumu Mungu
kamwe kwa changamoto inayokukabili. Hakuna changamoto inayompata mtu kamwe kwa
lengo la kumuangamiza, changamoto itakuangamiza endapo tu utanzaa kulaumu,
utajiona hufai, utajiona hukustahili na utamua kukata tama. Lengo la changamoto
pasipokujali inatupata kwa namna gani, ni kutufundisha na kutuimarisha. Na
ndiyo maana kuna misemo mingi sana, kwa mfano msemo mmoja wa Kiswahili unasema,
“ukimuona nyani mzee ujue amekwepa mishale mingi sana”, upo msemo mwingine wa
Kiingereza usemao, “experience makes perfection”. Unapomshukuru Mungu,
unamfanya ashughulikie changamoto yako yeye mwenyewe, ama kwa kukupa njia
sahihi au mtu sahihi kwa ufumbuzi wa changamoto hiyo. Kumbuka Biblia haisemi
Yesu Kristo alipowashika wale samaki watano na mikate miwili (ni zaidi ya utani
kuwa na samaki wawili na mikate mitano kama chakula cha watu wanaozidi elfu
tano) mikononi mwake alianza kuombea waongezeke ili watoshe idadi ya watu. La
hasha, Yesu Kristo alishukuru, Mungu akaongeza samaki na mikate ili itosheleze
idadi ya makutano na kusaza.
Kukabili na kutatua changamoto
Yesu Kristo aliamuru wafuasi wake wafanye mambo mawili;
kuwakalisha chini makutano na kuwagawanya makutano katika makundi ya watu wachache
wachache. Kuwakalisha chini makutano maana yake ni kuliweka tatizo au
changamoto (makutano) chini ya mamlaka na uwezo wake. Unapoiweka changamoto
chini ya mamlaka na imaya yako (kwa njia ya maombi na kushukuru), unaifanya
ionekano ndogo kuliko uwezo na nguvu zako, hii itakusaidia katika kuikabili
hiyo changamoto pasipo woga. Ziambie changamoto zako, Mungu wako ni mkubwa
kuliko zenyewe. Yesu Kristo alipowagawanya makutano katika makundi alikuwa
anatatua changamoto kwa hatua. Kamwe huwezi kutatua changamoto yoyote ile
pasipo kuimega kidogo kidogo hadi inaisha. Ukilazimisha kutatua changamoto yako
kwa mara moja, kuna sehemu kutakudai kutatua badae, hutaweza kuimaliza. Kwa
namna nyingine unapopatwa na changamoto angalia palipo rahisi ndipo anza napo
hapo. Kwa mfano, mwanafunzi unamaliza kidato cha sita, hujafanya vizuri katika
mtihani kuweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu kutimiza ndoto yako ya kupata
digrii uipendayo, badala ya kukata tamaa na kukaa nyumbani kuanza tabia
hatarishi zinazoweza kuharibu kabisa maisha yako, unaweza kuamua kusoma kwanza
diploma ya fani ile uipendayo, baada ya kumaliza hiyo diploma unapata sifa ya
kuendelea na masomo ya chuo kikuu kupata digrii ya ndoto yako.
Mwenyezi Mungu akubariki sana msomaji wangu. Ni maombi yangu
kuwa Mungu akuongoze kwa kila changamoto unayopitia ili utoke kwa ushindi.
Amina.
No comments:
Post a Comment