Thursday, September 27, 2012

NGUVU YA MANENO.


  Katika maneno tunayoyazungumza kuna nguvu ya uumbaji wa kile tunachokizungumza. Kwa mfano mtumishi wa Mungu anapofanya maombezi kwa ajili ya mtu fulani, anatamka maneno ya uponyaji kwa imani, na yule anayeombewa akiyasikia yale maneno ya uponyaji anaamini katika maneno yale na ndipo anapokea uponyaji. Hii inatokea kwa sababu maneno tunayoyasikia yanatufanya tujenge picha ya kile tunachokisikia. Ukisikia maneno ya uponyaji unapata picha ya kupona, ukisikia maneno ya kukutia moyo unapata picha ya kutiwa moyo na ukisikia maneno ya kukukatisha tamaa utapata picha ya kukata tamaa na kushindwa. Na jambo hilo linasababishwa na jinsi tunavyojenga imani katika maneno tunayoyasikia ama kujisemea wenyewe.
Yakobo 1:19 “Basi kila mtu  na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema;”.
Mstari huo wa kitabu kitakatifu cha Biblia, unatufundisha kutokuwa wepesi wa kusema. Kwa sababu katika kusema sana tutasema maneno yenye kuvunja moyo, kukatisha tamaa, kulaani na hata maneno yasiyo na maana ili mradi tuonekane tumesema. Tunatakiwa tuseme au tuongee maneno ya kubariki, kutia moyo na kufariji; maneno ambayo mtu anayekusikia atatamani akusikie tena na kesho na siku inayofuata kwa sababu una kitu cha maana katika maisha yake.
   Baraka, kwa kutumia maneno ya vinywa vyetu tunaweza kubariki. Tukitaka kumbariki mtu au kumfariji tunatumia maneno. Tunatamka maneno yenye baraka au kufariji. Mwanzo 27:27-28 “…akambariki AKASEMA (maneno), Mungu na akupe  ya umande wa mbingu, na ya manono ya nchi, na wingi wa nafaka na mvinyo.”
   Laana, pia kwa kututmia maneno ya vinywa vyetu tunaweza tukatamka maneno ya kulaani. Ambapo tunaweza kujilaani wenyewe au wenzetu kwa kujua ama kutokujua. Tunapoongea jambo baya kwa maisha yetu au ya wenzetu tunakuwa tunatamka laana ambazo ni lazima zitatimia. Zaburi 10:7 “kinywa chake kimejaa laana, na hila na dhuluma, chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu.”
   Ikiwa unatamka laana au baraka, ushindi au kushindwa katika maisha yako au ya mtu mwingine, ni lazima jambo hilo litakuja kutimia. Unaweza ukamwambia mtu fulani kuwa unataka uanze kufanya biashara, na mtu huyo akakwambia, “na wewe unataka kufanya biashara, ameshinwda fulani utaweza wewe?” badala ya kumjibu NITAWEZA, unamjibu ‘najaribu jaribu tu ndugu yangu’. Unaanza biashara alafu miaka inakatika huoni faida yoyote, ni kwa sababu uliyemshirikisha jambo lako aliongea kushindwa na wewe pia ukakiri kushindwa huko. Kwa maana hiyo unaweza ukawa umetamkiwa/umejitamkia laana au baraka katika maisha yako bila wewe kujua. Na falme zote mbili; ufalme wa giza na Ufalme wa Mungu zinafuatilia unayoyakili kwa ajili ya maisha yako au ya wenzako ili kuyatenda au kuhakikisha yanatendeka.
Isaya 59:17(a) “Mimi nayaumba matunda ya midomo;”. Hapa Mungu alimwambia nabii Isaya kuwa yeye (Mungu), anayaumba matunda ya midomo yetu, kwa maana nyingine ni kwamba Mungu anayaumba maneno tunayotamka kwa ajili ya maisha yetu au wenzetu.
Na kwa upande wa ufalme wa giza pia yapo mapepo yanayofuatilia na kutimiza maneno ya vinywa vyetu, hasa maneno ya laana ili kuhakikisha tunaishi maisha yenye mateso na dhiki.
Kwa hiyo ndugu mpendwa katika Kristo Yesu, unatakiwa kufanya maombi ya kufunga ili uvunje laana zote katika maisha yako, laana ulizojitamkia kwa kujua au kutokujua na zile walizokutamkia wengine. Na Mungu yupo atakujibu na kukubariki, muamini tu.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts