Msongo wa mawazo na
ukosefu wa amani moyoni na/au nafsini imekuwa ni tatizo linaloongezeka kwa kasi
na kuwapata watu wengi sana. Na ubaya ama ugumu wa tatizo hili ni kwamba
linagundulika baada ya matokeo ya ukosefu wa amani moyoni au nafsini na msongo
wa mawazo.
Yaani ni hivi; watu
wengi wasio na amani moyoni na nafsini huishi maisha ya kuigiza na huwa vigumu sana kuwatambua watu hao,
unaweza kumtambua mtu mwenye msongo wa mawazo kwa tabia yake ya kujitenga na
kutoshirikiana na watu. Lakini unaweza usimtambue mtu asiye na amani moyoni au
nafsini kwa sababu wengi wa watu hawa huvaa sura zenye tabasamu na furaha
wawapo mbele za watu.
Ni watu wanaoyabeba maumivu
yao wao wenyewe na kujaribu kutafuta suluhisho pasipo kuwashirikisha watu
wengine. Na ndipo utakaposhangaa kuona mtu fulani amefanya jambo usilolitegemea
alifanye, kwa mfano; kuua au kujiua wao wenyewe, kutukana matusi, au kufanya
jambo la hatari ilihali anajua madhara yake pasipo kujihadhari.
Ndiyo, matokeo ya
ukosefu wa amani moyoni au nafsini pamoja na msongo wa mawazo matokeo yake siku
zote huwa ni hasara au maumivu kwa muhusika au watu wanao mzunguka. Wengi
hutafuta njia za kutua mizigo iliyomo mioyoni na nafsini mwao kwa njia za mkato
ambazo wengi hudhani kujiua au kuwaua wale wailowasababishia maumivu hayo ndiyo
jibu sahihi.
Kuna nyakati ukosefu wa
amani ya nafsi au moyo kunaambatana na chuki na visasi, yaani muhusika hubebea
chuki na/au visasi dhidi ya mtu au watu waliomsababishia maumivu hayo. Kubeba
chuki na visasi vya muda mrefu ndani ya mioyo na nafsi zilizokosa amani
hupelekea matatizo ya kiafya kama shinikizo la damu (hypertension), mshituko
(stroke), kupooza (paralysis) na hata kuzeeka mapema (early aging). Hii hutokea
kwa watu ambao wana msongo wa mawazo, wamekosa amani moyoni na nafsini na huku
wamebeba mizigo ya chuki na visasi dhidi ya watu wasioweza kuwalipia hicho
kisasi.
Sisemi inatupasa kubeba
chuki na visasi mioyoni na nafsini mwetu, hiki ni kitu kinachotupata nje ya
uwezo wetu (involuntary action). Na kama jinsi tumekosa amani mioyoni na
nafsini mwetu pasipo kupenda sisi wenyewe, ndivyo ilivyo ni vigumu kuitafuta
amani ya nafsi na mioyo yetu sisi wenyewe pasipo msaada wowote.
Ni lazima utafute
msaada, na msaada pekee na wa kuaminika ni Mungu (Yehova) peke yake. Ndiyo,
kuna wanasaikolojia waliobobea ambao wanaweza wakakusaidia, lakini msaada wa
Mungu kupitia Yesu Kristo ndiyo una uhakika wa asilimia mia moja (100%).