Wednesday, August 21, 2013

HATUA NNE ZA KUPATA AMANI YA MOYO NA NAFSI (INNER PEACE).
Msongo wa mawazo na ukosefu wa amani moyoni na/au nafsini imekuwa ni tatizo linaloongezeka kwa kasi na kuwapata watu wengi sana. Na ubaya ama ugumu wa tatizo hili ni kwamba linagundulika baada ya matokeo ya ukosefu wa amani moyoni au nafsini na msongo wa mawazo.

Yaani ni hivi; watu wengi wasio na amani moyoni na nafsini huishi maisha ya kuigiza  na huwa vigumu sana kuwatambua watu hao, unaweza kumtambua mtu mwenye msongo wa mawazo kwa tabia yake ya kujitenga na kutoshirikiana na watu. Lakini unaweza usimtambue mtu asiye na amani moyoni au nafsini kwa sababu wengi wa watu hawa huvaa sura zenye tabasamu na furaha wawapo mbele za watu.

Ni watu wanaoyabeba maumivu yao wao wenyewe na kujaribu kutafuta suluhisho pasipo kuwashirikisha watu wengine. Na ndipo utakaposhangaa kuona mtu fulani amefanya jambo usilolitegemea alifanye, kwa mfano; kuua au kujiua wao wenyewe, kutukana matusi, au kufanya jambo la hatari ilihali anajua madhara yake pasipo kujihadhari.

Ndiyo, matokeo ya ukosefu wa amani moyoni au nafsini pamoja na msongo wa mawazo matokeo yake siku zote huwa ni hasara au maumivu kwa muhusika au watu wanao mzunguka. Wengi hutafuta njia za kutua mizigo iliyomo mioyoni na nafsini mwao kwa njia za mkato ambazo wengi hudhani kujiua au kuwaua wale wailowasababishia maumivu hayo ndiyo jibu sahihi.

Kuna nyakati ukosefu wa amani ya nafsi au moyo kunaambatana na chuki na visasi, yaani muhusika hubebea chuki na/au visasi dhidi ya mtu au watu waliomsababishia maumivu hayo. Kubeba chuki na visasi vya muda mrefu ndani ya mioyo na nafsi zilizokosa amani hupelekea matatizo ya kiafya kama shinikizo la damu (hypertension), mshituko (stroke), kupooza (paralysis) na hata kuzeeka mapema (early aging). Hii hutokea kwa watu ambao wana msongo wa mawazo, wamekosa amani moyoni na nafsini na huku wamebeba mizigo ya chuki na visasi dhidi ya watu wasioweza kuwalipia hicho kisasi.

Sisemi inatupasa kubeba chuki na visasi mioyoni na nafsini mwetu, hiki ni kitu kinachotupata nje ya uwezo wetu (involuntary action). Na kama jinsi tumekosa amani mioyoni na nafsini mwetu pasipo kupenda sisi wenyewe, ndivyo ilivyo ni vigumu kuitafuta amani ya nafsi na mioyo yetu sisi wenyewe pasipo msaada wowote.

Ni lazima utafute msaada, na msaada pekee na wa kuaminika ni Mungu (Yehova) peke yake. Ndiyo, kuna wanasaikolojia waliobobea ambao wanaweza wakakusaidia, lakini msaada wa Mungu kupitia Yesu Kristo ndiyo una uhakika wa asilimia mia moja (100%).


Wafilipi 4:7. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

Kuna vitu vya muhimu sana katika mstari wa Biblia hapo juu, amani ya Mungu; hakuna amani nyingine yo yote iwezayo kutuhifadhi mioyo na nia zetu kama jinsi iwezavyo amani atupayo Mungu. Kuna watu wana mali nyingi; magari ya kifahari, majumba makubwa ya kifahari, mashamba makubwa yenye rutuba na mifugo mingi iliyositawi sana lakini wamekosa amani. Hakuna kiwezacho kukuhifadhi moyo wako au nafsi yako katika utulivu wa amani isipokuwa Mungu tu.

Ipitayo akili zote; kuna watu wana elimu ya saikolojia, ni washauri wazuri sana. Watakushauri vyema lakini hawana uwezo wa kuingia ndani ya moyo au nafsi yako kuweka amani. Ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kuingia moyoni mwako na kukupatia amani ya kudumu.

Katika Kristo Yesu; ukitaka kuipata amani ya Mungu ikuhifadhi moyo na nafsi yako, ni kupitia Yesu Kristo au kuomba kwa kupitia Jina la Yesu Kristo, hakika utapokea. Huo mzigo wa uchungu, hasira, chuki na/au visasi ulioubeba moyoni mwako ni Yesu Kristo pekee ndiye anayeweza kukutua mzigo huo, kwani ameahidi kutupa pumziko na raha nafsini mwetu (Mathayo 11:28-30 na Wagalatia 5:1).
Kuna mambo mengi yanayoweza kukufanya ukose amani moyoni au nafsini; inawezekana ni jambo ulilojikosea wewe mwenye ama lilikuwa nje au ndani ya uwezo wako, au ni jambo walilokukosea watu wa karibu nawe. Katika hali zote hizo mbili hupaswi kuendelea kuubeba mzigo ulioubeba hivi sasa ndani ya moyo/nafsi yako na hupaswi kujidhuri au kuwadhuru watu wengine.

1 Petro 3:8-11. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana atakaye kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya, na modomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; atafute amani aifuate sana.

Kinachowaumiza wengi na kuwakosesha amani mioyoni na nafsini mwao ni kwamba wanaowakosea au kuwaumiza ni watu wa karibu yao na ni wale waliowapenda sana. Hivyo hujikuta wanajaza chuki na visasi ndani ya mioyo yao lakini wanashindwa kufanya jambo lolote kwa sababu wanaakuwa katika hali ya kutahamaki na kutoamini waliyotendewa. Na jinsi siku zinavyozidi kwenda ndivyo hali ya muhusika inavyozidi kuwa mbaya. 

Nataka nikwambie hivi; haijarishi aliyekuumiza ni nani, ni mtu wa karibu nawe kiasi gani, ni mtu uliyempenda na kumuamini kiasi gani? Hata kama ni mzazi/wazazi, mke/mume, mchumba au rafiki, hutakiwi kulipa kisasi na kubeba chuki ndani ya moyo/nafsi yako. Tafuta amani ya nafsi/moyo wako kwa faida yako wewe mwenyewe, raha jipe mwenyewe. Achana na habari za kubeba mizigo isiyo na faida nafsini/moyoni mwako.

Na kitu cha muhimu zaidi unachopaswa kuishi huku ukikitambua na kukitegema kila siku ni kuwa hata watu wa karibu yako, unaowapenda sana wanaweza wakakuumiza na kukukwaza. Ukilitambua hilo, halitakupa tabu. Usimwamini mwanadamu mwenzako kama jinsi unavyomwamini Mungu, wanadamu tuna mapungufu ni Mungu pekee ndiye hana mapungufu. Hakuna sababu ya kujidhuru au kujiua kwa sababu ya mwanadamu mwenzako.

Baada ya kuyaelewa hayo machache hapo juu, sasa tuangalie hatua nne muhimu za kukuwezesha upate amani ya moyo/nafsi. Nakuhakikishia kupitia Jina la Yesu Kristo kuwa kupitia hatua hizi nne unakwenda kupata amani ya moyo/nafsi yako na unakwenda kuwa na furaha ya kweli kama wengine na siyo furaha ya maigizo uliyonayo sasa.

Jisamehe wewe mwenyewe.
Wasamehe waliokukosea.
Tua mzigo uliopo moyoni/nafsini mwako.
Omba rehema mbele za Mungu.


Jisamehe wewe mwenyewe.
Kujisamehe wewe mwenyewe ni hatua ya kwanza muhimu katika kupata amani ya moyo na/au nafsi. Kwa sababu gani nasema unatakiwa kujisamehe wewe mwenyewe, kuna watu wamejikosea wenyewe au wamekosewa na watu wengine lakini hujichukia nafsi zao, hujilaumu na kujiona hawastahili kuendelea kuishi. Hufikiria kujitendea mambo mabaya na kujidhuru. 

Hupaswi kuwa katika hali hiyo; pasipo kujali umejikosea wewe mwenyewe au umekosewa na mtu/watu wa karibu yako. Unastahili kujisamehe na kuachilia mzigo ulionao moyoni mwako.
Hupaswi kuangalia ukubwa au wingi wa makosa uliyojikosea au uliyokosewa, hebu jiulize kama Mungu angehesabu wingi na ukubwa wa makosa yetu hasingekuwa radhi kutusamehe kabisa. Lakini Mungu yupo radhi na anasubili tumuombe msamaha atusamehe pasipo wingi au ukubwa wa makosa yetu (Luka 15:7, 2 Petro 3:9).

Mungu atakusaidia kama utamuomba msaada, hupaswi kuhesabu uliyotenda au kutendewa unastahili kujisamehe na kuisamehe nafsi/moyo wako (Zaburi 103:10-12 na Zaburi 130:3).
Kamwe hutaweza kupata furaha na amani nafsini/moyoni mwako au hutaweza kukamilisha hatua tatu zifuatazo ikiwa hutaweza kuitekeleza na kuikamilisha hatua hii ya kwanza muhimu sana.
Ondoa mawazo mabaya sasa ya kutaka kujidhuru au kujitoa uhai, kuwadhuru au kuwatoa uhai wengine. Unaweza kusimama katika mstari mnyofu, jipe nafasi tena na Mungu atakusaidia.

Wasamehe wengine.
Hatua nyingine muhimu katika kupata amani ya moyo na nafsi yako kwa ujumla ni kuwasamehe wengine, hasa wale waliokukosea na kukufanya ubebe mzigo wa chuki, hasira na kisasi ndani ya moyo wako.

Ni jambo jepesi kujisamehe wewe mwenyewe, lakini ni vigumu kumsamehe au kuwasamehe watu waliokukosea hasa ikiwa watu hao wanaishi mazingira ya karibu na wewe na wanafurahia kwa walichokukosea au kukufanyia. Ikiwa unapata ugumu kuachilia msamaha, omba msaada wa Mungu.
Lakini huna budi kuachilia msamaha kwa ajili yao, siyo kwa faida yao bali ni faida yako, ya nafsi yako na moyo wako wewe mwenyewe. Zipo faida kuu mbili; kwa ajili ya afya yako na kiimani ya dini hasa Kikristo.

Kwa ajili ya afya yako; unapojisamehe na kuwasamehe waliokukosea unajipa nafasi kubwa ya kuachilia na kutua mzigo ulioubeba ndani ya moyo wako. Na unapoachilia na kutua mzigo uliomo ndani ya nafsi yako, unajipa nafasi kubwa ya kuepukana na msongo wa mawazo. Na mwili wenye afya na usioweza kupatwa na magonjwa ya tabia hasa ya msongo wa mawazo ni mwili wenye amani na furaha moyoni na nafsini.

Kiimani; unapowasamehe waliokukosea unakuwa unatimiza agizo la Mungu, na kwa kutimiza agizo la Mungu unakuwa unazingatia na kutimiza amri za Yesu Kristo (Luka 17:3-4). Tuwapende adui zetu na kuwaombea mema wanaotuudhi (Warumi 12:14 na Mathayo 5:43-44 na 48).
Kwa kuwasamehe waliokukosea, unajipa nafasi ya wewe kupata msamaha mbele za Mungu kwa makosa/dhambi ulizozitenda (Marko 11:25 na Waefeso 4:32). Hivyo basi huna budi kujisamehe na kuwasamehe waliokuudhi na kukukosea pasipo kuhesa wingi na kuangalia ukubwa wa makosa waliyokutendea.

Achilia na tua mzigo uliopo moyoni mwako.
Hii ni hatua muhimu sana, ikiwa umeweza kutimiza hatua mbili za mwanzo na ukashindwa kutimiza hatua hii, hujafanya kitu bado. Ndiyo sababu nakwambia kwamba hii ni hatua muhimu sana, kuna watu wanaweza kusamehe; kujisamehe au kuwasamehe wengine lakini hawawezi kuwasahau waliowakosea.

Ikiwa umejisamehe au umemsamehe mtu na huwezi kumsahau, maana yake ni kwamba bado hujamsamehe au hujajisamehe. Na kama kweli umemsamehe lakini unashindwa kumsahau, maana yake ni kwamba umembeba ndani ya moyo wako.

Kumbeba mtu aliyekukosea moyoni mwako ni sawa na kubeba mizigo mingine kama chuki, hasira na kisasi. Huwezi kutua mzigo wa chuki, hasira na kisasi halafu ukabaki umembeba aliyekukosea ukidhani unaweza kupata amani moyoni au nafsini mwako. Haiwezekani kamwe!

Ndiyo maana nakwambia kuwa hii ni hatua muhimu sana ya kupata amani moyoni/nafsini, kutua mzigo uliofunga moyo na nafsi yako isiwe na amani ni pamoja na kuwatua na kuwaachilia watu uliowabeba ndani ya moyo wako. Siyo kuachilia na kutua chuki, hasira na kisasi tu, ni pamoja na kuwatoa watu wote waliokuudhi uliowahifadhi ndani ya moyo wako.

Mara nyingi, hatua hii huja yenyewe endapo utaamua kusamehe kwa dhati. Mara tu unapokubali kusamehe, unahisi kuna mzigo mzito unautua na kupata afueni ya moyo/nafsi.

Endapo utashindwa kutua mzigo wa hasira, chuki na kisasi dhidi yako au mtu/watu fualni waliokukosea, Yesu Kristo wa Nazareti yupo kukusaidia, kwani anasema wote walioelemewa na mizigo Yeye (Yesu) huwapa pumziko (Mathayo 11:28-30 na Waefeso 4:31). Hata wewe una haki na nafasi ya kupata pumziko, mwombe Yesu Kristo akusaidie.

Omba rehema kwa Mungu.
Kwa nini uombe rehema kwa Mungu? Ni kwa sababu kuhifadhi chuki, hasira na kisasi ndani ya moyo au nafsi ni dhambi (Wagalatia 5:19-21, Waefeso 4:26, 31-32, Wakolosai 3:8). 

Pia, mtu mwenye hasira, chuki na kisasi moyoni mwake huongea maneno ya kufuru, hutukana, hudhamiria uovu kama kujitoa uhai au kumtoa mtu/watu wengine uhai, hayo yote ni chukizo mbele za Mungu (Yakobo 1:20, Wakolosai 3:8).

Hayo yote unastahili kuyaombea toba, Mungu wetu (Yehova) ni mwaminifu, atakusamehe, anasubiri kuiona nia ya moyo wako na kuisikia sauti yako ikikiri kuomba toba na rehema mbele zake. Mungu ni mwingi wa rehema (Zaburi 111:4 na Zaburi 145:8), tukiziungama dhambi zetu atatusamehe na kutusafisha udhalimu wote (1 Yohana 1:9), maadam tumeomba rehema kutoka ndani ya mioyo yetu kwa nia thabiti (Yoeli 2:12-13).

Kuna aina nyingine ya ukosefu wa amani ya nafsi au moyo, aina hii ni tofauti na hiyo niliyoielezea hapo juu. Aina hii, unakuta mtu unapoteza amani moyoni au nafsini pasipokuwa na sababu maalumu au inayoeleweka. 

Yaani hakuna mtu aliyekuudhi au kukukosea na hata wewe mwenyewe hujafanya jambo lolote la kukukera, lakini ghafla au taratibu unajikuta unapoteza amani moyoni au nafsini na unachukia au unakuwa na hasira dhidi yako au watu wanaokuzunguka.
Na wengi wanaopatwa na aina hii ya ukosefu wa amani ya moyo/nafsi hupenda kujitenga mbali na watu, huwa hawapendi kuwa karibu na watu. Ikiwa unapatwa na hali hii, unapaswa kutafuta msaada wa haraka sana.

Kwa nini utafute msaada wa haraka sana? Ni kwa sababu hali hii husababishwa na nguvu za giza au mapepo ambayo hutumwa kwa makusudi maalumu. Na makusudi hayo huwa ni uharibifu au madhara kwa muhusika au jamii yake ya karibu kama kuharibu kazi za ofisi, kuwasababishia wengine maudhi, kujitoa uhai au kutoa uhai wa mtu/watu wengine. Ni rahisi sana kwa mtu wa aina hii kujidhuru au kuwadhuru watu wengine.

Msaada wa mtu anayepatwa na hali hii ni; maombi, hakikisha unafanya maombi ya kumuomba Mungu akupe amani nafsini/moyoni na akuepushe na kufanya jambo baya, zaidi akuepushe na hali ya kukata tamaa, inapobidi tafuta watu wanaomtumikia Mungu (Yehova) katika roho na kweli washirikishe kimaombi.

Pia, unapopatwa na hali hii ya kupotelewa na amani moyoni au nafsini pasipo sababu, ikiwa kuna kazi ya muhimu ulikuwa unafanya jipe mapumziko hadi pale utakapolejelewa na amani moyoni/nafsini. Na usijitenge mbali na watu, jaribu kuwa karibu na watu wanaokufanya ujisikie furaha.
Mungu ni mwaminifu, ukimtumainia atakusaidia. Amina.

1 comment:

Featured Post

WHO IS JESUS CHRIST?

  Who is Jesus Christ? Jesus Christ is God who wore man’s flesh purposely to die on the cross for compensating humans’ sins ...

Popular Posts