Ukiyachunguza maandiko katika vitabu vya Biblia vya
Injili zile nne; Injili ya Mathayo, Marko, Luka na Yohana utakutana na vifungu
vingi vikionesha jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyopenda kuambatana na Petro,
Yohana na Yakobo.
Na alipenda kuambata na wanafunzi wake hao watatu;
Petro, Yohana na Yakobo sehemu muhimu au katika shughuli muhimu. Kwa mfano,
alipotaka kwenda faragha kwa maombi au alipoamua kufanya jambo la uponyaji
lililohitaji imani kubwa.
Kuna sababu nyingi sana zilizomfanya Bwana wetu Yesu
Kristo apende kuambatana na wanafunzi wake hao watatu katika faragha na sehemu
muhimu mbali mbali.
Petro, Yohana na Yakobo richa ya kwamba walikuwa
ndugu (Yakobo na Yohana - Mathayo 4:21) na marafiki (Marko 13:3, Matendo ya
Mitume 3:1) walikuwa wana sifa za pamoja zinazofana na sifa za kila mmoja wao,
ambazo kwa umoja wao walitengeneza timu iliyompendeza Yesu Kristo.
Hebu tuangalie baadhi ya vifungu vinavyo thibitisha
kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alipenda kuongozana zaidi na Petro, Yohana na
Yakobo kwa maombi ya faragha au katika jambo la kipekee na umuhimu zaidi.
Mathayo 17:1. Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa
Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu yam lima mrefu faraghani
(kwa maombi).
Marko 1:29. Na mara walipotoka katika sinagogi,
walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe
Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia (Yesu
Kristo) habari zake. (Yesu Kristo)
Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.
Marko 5:37. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila
Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo.
Luka 22:8. Akawatuma Petro na Yohana, akisema,
Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila.
Marko 14:32-33. Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo
Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa
Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.
Hivyo ni baadhi ya vifungu vya Biblia vinavyo
thibitisha jinsi Yesu Kristo alivyopenda kuwa karibu na Petro, Yakobo na
Yohana.
Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, Petro, Yohana
na Yakobo walikuwa na sifa za ujumla na sifa za pekee kwa kila mmoja. Ukaribu
wao uliosababishwa na undugu na urafiki uliwafanya watengeneze umoja wa pekee
kwani waliunganisha sifa zao na kufanyika kitu kimoja.
Sifa zao kwa ujumla ndizo zilizomfanya Yesu apende
kufanya nao mambo kwa umoja. Hebu tuziangalie sifa za wanafunzi hao kwa umoja
na kwa upekee.
Sifa za pamoja;
Historia moja. Petro, Yohana na Yakobo walikuwa
wanafunzi wa Yesu Kristo wenye historia ya aina moja kuhusu mahali walipoishi,
aina ya kazi waliyofanya (uvuvi) na sehemu au mahali walipofanyia kazi yao
(bahari ya Galilaya). Hii inapatikana katika; Mathayo 4:18-20, Marko 1:16-20 na
Luka 5:4-11.
Wenye imani kubwa na thabiti. Walikuwa ni wanafunzi
wa Yesu wenye imani iliyosimama imara, walioamini uwezo wa Yesu wa Kiungu
pasipo na shaka yoyote. Hawakuwa na swali juu ya utendaji kazi wa Yesu. Na hata
wengine walipotindikiwa imani, wanafunzi hawa waliendelea kuamini kuwa Yesu
Kristo anao uwezo na nguvu za Kiungu. Hii inathibitishwa na Mathayo 14:28-29 na
Matendo ya Mitume 3:3-8.
Na kutokana na imani yao, Yesu Kristo alikwenda nao
kufanya uponyaji wenye kuhitaji imani kubwa pia. Hii inapatikana katika Luka
8:50-51. Katika kifungu hicho cha Biblia, Yesu Kristo alipoingia ndani ya
chumba cha yule binti marehemu aliingia na Petro, Yohana na Yakobo pamoja na
wazazi wa yule binti kutokana na imani yao thabiti isiyokuwa na shaka.
Walipenda kuwa na Yesu kwa faragha. Wanafunzi hawa
wa Yesu walipenda kumdadisi Yesu mambo fulani, na mara nyingi walipoamua
kumdadisi Yesu jambo walilifanya kwa faragha. Walijichukua wao na kumfuata Yesu
na kumuuliza duku duku lao. Soma vifungu vifuatavyo; Marko 10:35, Marko 13:3.
Marafiki. Wanafunzi hawa wa Yesu Kristo walipenda
zaidi wao na walikuwa ni marafiki. Ukisoma katika Biblia utaona walikuwa
wakifuatana sehemu nyingi hata walipokuwa hawako na Yesu, Marko 13:3 na Matendo
ya Mitume 3:1. Na hata neno linasema watu hawawezi kuongozana isipokuwa
wamepatana (Amosi 3:3). Kwa hiyo wanafunzi hawa watatu wa Yesu walikuwa
wanapatana zaidi.
Sifa za mmoja mmoja;
Petro (Simoni Petro).
Historia fupi ya Mtume Petro;
Mtume Petro alizaliwa Betsaida, mjini Galilaya
katika nchi ya Israeli. Yeye na baba yake, Yona walikuwa wavuvi katika bahari
ya Galilaya. Alikuwa na kaka aitwaye Andrea, alikuwa miongoni mwa Mitume wa
Yesu Kristo.
Yesu Kristo alimwita Simon Petro mwamba, na kumfanya
kuwa msingi wa kanisa imara ambalo milango ya kuzimu hailiwezi. Mathayo 16:18.
Na siku ya Pentekoste, wanafunzi wa Yesu Kristo
walipojazwa nguvu za Roho Mtakatifu, Simoni Petro alisimama kwa ujasiri na
kusema na makutano waliokusanyika wakishangaa. Matendo ya Mitume 2:14-21.
Simoni Petro alifungwa gerezani mara kadhaa kwa
kumuhubiri Yesu Kristo baada ya kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Kisha Petro
alihamia mjini Roma ili aihubiri injili ya Yesu Kristo ambapo alifia huko kwa
kusulubishwa kichwa chini miguu juu.
Mdadisi. Katika wanafunzi wote 12 wa Yesu Kristo, ni
Petro peke yake aliyekuwa haachi jambo limpite endapo hakulielewa. Mara nyingi
alipenda kujua maana ya mafumbo/mifano aliyoiongea Yesu, na hata kuna wakati
alitaka kujua faida ya wao kuacha vyote na kumfuata Yesu Kristo. Mathayo 15:15,
Marko 10:28 na Luka 18:28.
Alijiamini. Petro ni mwanafunzi wa Yesu ambaye
hakuteteleka kwa jambo lolote na kwa hali yoyote. Alijiamini na alijua anaweza
hata katika nyakati ambazo wanafunzi wengine wote waliporudi nyuma, Petro
alisimama peke yake na kusonga mbele. Marko 14:27 na 29, Luka 22:54, Yohana
18:10.
Asiyekatishwa tamaa. Kuna nyakati Petro alikutana na
mambo ya kukatisha tamaa na kurudishwa nyuma, lakini alisimama imara,
hakutetereka. Kuna kipindi Yesu Kristo alimtamkia “rudi nyuma shetani” lakini
Petro alitambua haikuwa kauli elekezi kwake, bali ilikuwa ni kauli iliyotumwa
kwa shetani kupitia yeye, Marko 8:33. Wanadamu wengi wakiambiwa kauli hii
watakata tamaa mara moja.
Yohana.
Historia fupi ya Yohana;
Yohana mwana wa Zebedayo, pamoja na ndugu yake
Yakobo walikuwa wavuvi katika bahari ya Galilaya. Walifanya kazi hiyo pamoja na
Simoni Petro na ndugu yake Andrea.
Yohana na ndugu yake Yakobo walipewa jina la
Boanerge na Bwana wetu Yesu Kristo, ikimaanisha wana wa ngurumo. Marko 3:17.
Yohana ni mwanafunzi au mtume wa Yesu Kristo
aliyeshuhudia mateso hadi kifo cha Yesu Kristo, pasipo kujificha wala kuogopa.
Yohana ni mtume pekee aliyependwa sana na Yesu
Kristo, na hata siku ya kifo cha Yesu Kristo msalabani alimkabidhi mama yake
(bikira Mariamu) kwa Yohana. Yohana 19:26-27.
Yohana ni mtume wa Yesu Kristo aliyeandika Injili ya
Yohana na Nyaraka tatu za Yohana wa 1, 2 na 3.
Alipendwa sana na Yesu Kristo. Kuna mistari kadhaa
katika Biblia inasema kuna mwanafunzi alipendwa sana na Yesu, japo haitaji jina
la mwanafunzi huyo. Lakini wana Theologia wanamtaja mwanafunzi huyo kuwa ni
Yohana. Yohana 13:23, Yohana 20:2.
Alidhamiria kumfuata na kumtumikia Yesu Kristo.
Yohana alijitoa mwili na roho kumtumikia Yesu Kristo na alitamani sana kuona
siku moja anaketi pamoja na Yesu Kristo katika ufalme wa Mungu. Na kuna wakati
aliomba kuketi karibu na Yesu katika ufalme ujao wa Mungu, Marko 10:35-36.
Yakobo.
Historia fupi ya Yakobo;
Alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa kwanza
kuchaguliwa na Bwana wetu Yesu Kristo, yeye pamoja na ndugu yake Yohana. Alifanya
kazi ya uvuvi katika bahari ya Galilaya pamoja na ndugu yake na baba yao
Zebedayo.
Yakobo alikuwa ni mzaliwa wa Kapernaum, baada ya
kifo na ufufuo wa Yesu Kristo, Yakobo aliendelea kuihubiri Injili ya Yesu Kristo.
Aliuawa na mfalme Herode kwa kukatwa kichwa kwa upanga. Matendo ya Mitume
12:1-2.
Hitimisho.
Katika jumla ya wanafunzi wote kumi na wawili (12)
wa Yesu Kristo, ni wanafunzi watatu tu waliopata nafasi ya kuwa karibu na Yesu
Kristo na kufanya kitu kinachoitwa “Christ’s inner circle”, wanafunzi hao ni
Petro, Yohana na Yakobo.
Wanafunzi hawa walipata bahati au nafasi ya
kushuhudia matendo makuu ya Yesu Kristo pasipo uwepo wa wanafunzi wengine.
Matendo au nyakati hizo ni; ufufuo wa binti Yairo
(Marko 5:35-42), kubadilika uso na mavazi yake (Mathayo 17:1-3) na maombi ya
mwisho ya Yesu Kristo kabla ya mateso ya msalaba (Mathayo 26:36-38).
Ubarikiwe na Bwana kwa neno zuri.
ReplyDeleteAsante sana mtumishi kwa uchambuzi mzuri ubarikiwe sana
ReplyDelete