Amani ni hali ya
ukosefu wa inayohusu au kusababishwa na vurugu au mapigano ya aina fulani au
uwepo wa vurugu au mapigano ya namna yoyote ile katika sehemu fulani. Kunapotea
vuguvugu ya uwepo wa vurugu au mapigano baina ya pande mbili, watu wakiingiwa
na hofu kuhusiana na kutegemewa kuwepo kwa vurugu au mapigano hayo, watu hao
husemekana wamekosa amani. Hali kadhalika uwepo wa vurugu au mapigano yenyewe
ndiyo kabisa watu hukosa amani.
Tunaposema mtu au watu
wana amani ni lazima uwepo usawa baina ya watu hao katika nyanja mbali mbali
kama; usawa kwa mambo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kikabila, kiitikadi au
kiimani za dini. Pasiwepo na mwenye kujiona ni bora na anafaa zaidi ya
mwengine. Na pia ni lazima yawepo mahusiano mazuri baina ya mtu mmoja na
mwengine.
Kunapotekea kutokuwepo
kwa usawa na kuvumiliana katika siasa, manufaa ya mgawanyo wa faida zitokanazo
na rasilimali za nchi, ukabila na hata tofauti za dini, amani huvunjika.
Amani inapovunjika
husababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, yajulikanayo kama vita ya wenyewe
kwa wenyewe. Ni tofauti ndogo tu, ambazo huonekana hazina matokeo hasi kwa
jamii ndizo zilizopelekea ukosefu wa amani na vita ya wenyewe kwa wenyewe
katika mataifa mengi tunayoyajua yana vita.
Na ili machafuko
yatokee, ni lazima kuwepo na watu wanaosukuma na kuchochea machafuko hayo. Ni
lazima awepo mtu mwenye kupindisha ukweli wa mambo au kama siyo kupindisha basi
ni kufikisha ujumbe au ombi lake kwa njia yenye uchochezi wa machafuko
yanayopelekea ukosefu wa amani.
Na wachochezi wa
machafuko na uvunjifu wa amani ni watu wenye ushawishi mkubwa kwa kundi kubwa
la watu, na watu wanaotumiwa ni wale ambao mara nyingi huwa hawafikirii matokeo
ya kile wanachokwenda kukifanya.
Kumekuwa na kutokuelewana
na kutovumiliana baina ya dini mbili hapa nchini kwetu, vurugu zinazoweza
kusababisha machafuko na hata vita kama tu hatua za makusudi za kuitafuta amani
na maelewano baina ya pande hizi hazitafanyika. Kwa sababu mataifa yaliyopo
katika vita kutokana na tofauti za dini, yalianza hivi hivi na wahusika
wakazifumbia macho chachu hizo kwa sababu waliziona ni kitu kidogo sana.
MATOKEO YA UVUNJIFU NA
UKOSEFU WA AMANI.
Vifo. Machafuko ya aina
yoyote, huambatanisha uwepo wa chuki baina ya pande mbili. Chuki hiyo hupelekea
mapigano ya kutumia silaha aidha za jadi au silaha za moto. Na kama ilivyo ada,
silaha inapotumika husababisha majera au kifo. Na idadi kubwa ya watu wanaokufa
ni watoto na wanawake.
Hivyo basi, kabla
hatujaingia katika uvunjifu wa amani ni lazima tujue kuwa miongoni mwa watakao
uwawa ni mama zetu, wake zetu, watoto wetu na hata wapendwa wetu.
Uharibifu wa miundo
mbinu. Miundo mbinu tuliyoijenga kwa miaka mingi na fedha za madeni kutoka
mataifa tajiri, tutakwenda kuiharibu ndani ya muda mfupi tu wa mapigano yasiyo
na tija. Na katika kipindi chote cha vita na machafuko, uchumi wa nchi nao
utakuwa unaporomoka.
Njaa. Taifa lolote
linaloingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ni lazima litakumbwa na
njaa, hii ni kutokana na hofu inayowakalia watu wake na kuwafanya wawe
wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe. Na hii husababisha ukosefu wa ujasiri wa
kwenda mashambani, masokoni na hata kufanya shughuli yoyote ya kujiingizia
kipato, hivyo hukaribisha njaa. Na matokeo ya njaa ni kifo, hata wale
walionusurika kufa kwa silaha za mapigano hufa kwa njaa.
Ubakaji. Tumekuwa
tukisikia kutoka katika nchi zenye vita kuwa wanawake, mabinti na hata watoto
walio chini ya umri wa miaka 18 wamekuwa wakibakwa hovyo pasipo msaada wowote.
Na kitu cha kujiambia na ndiyo ukweli wenyewe ni huu; asipobakwa mama yako,
atabakwa dada yako, kama sivyo basi mke wako au hata binti yako. Fikiri kabla
ya kutenda!
Wakimbizi. Tumezoea
kuitwa kisiwa cha amani na kuwapokea wakimbizi wanaozikimbia nchi zao kutokana
na machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe, kwa nini sasa tunajaribu kuivuruga
amani yetu? Tunatamani kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha wakimbizi duniani?
Labda ni fahari!?
Soko la viwanda vya
kutengeneza silaha. Kuna mataifa makubwa yanayomiliki viwanda vya kutengeneza
silaha, silaha za kila aina ambazo hazitumiki na haziuziki sana wakati wa
amani. Taifa lolote linaloingia katika machafuko ya kivita hugeuzwa kuwa soko
la mataifa hayo yanayotengeneza silaha. Ndiyo sababu utasikia wapiganaji wa
serikali wanapata silaha kutoka taifa Fulani na waasi wanapata silaha kutoka
taifa Fulani. Siyo kwamba wanapatiwa silaha hizo bure, wanazinunua iwe serikali
au waasi na kama siyo kuzinunua ni kwa njia ya mabadilishano na rasilimali za
nchi husika mfano mafuta, madini n.k. Tusikubali kuingia katika vita.
NINI CHA KUFANYA.
Dawa ya amani ya
Tanzania ipo! Hatuhitaji kuyaita mataifa au chombo chochote cha kimataifa cha
amani kutupa dawa, dawa tunayo sisi wenyewe. Haya yafuatayo ndiyo dawa ya amani
yetu.
Vyombo vya dini. Hapa
namaanisha dini zote mbili ni lazima zijiulize, miaka yote iliyopita ziliishi
kwa amani na maelewano kuna nini sasa hata maelewano yale na kuvumiliana kule
kukaondoka kirahisi hivyo? Lazima dini zote mbili zisimame imara kuhakikisha
zinaitetea na kuidumisha amani ya Taifa letu kwa kuihubiri amani na upendo
baina ya wafuasi wake na kati ya wafuasi wa dini nyingine.
Wanasiasa na viongozi
wa serikali. Hawa nao ni watu wenye ushawishi mkubwa kwa wafuasi wa vyama vyao
vya siasa na jamii kwa ujumla. Wanasiasa na viongozi wa serikali ni lazima
wachunge ndimi zao, kwani kulopoka maneno yenye uchochezi wa uvunjifu wa amani
haifai na sisi wananchi mwasiasa yoyote au kiongozi yoyote anayechochea
uvunjifu wa amani yetu huyo hatufai leo wala kesho, hapaswi kuchaguliwa kabisa
kuwa kiongozi wetu.
Wananchi na wafuasi wa
dini. Sisi tusikubali kutumika kama chombo cha kutimiza matakwa ya wengine kwa
manufaa yao binafsi, kama tuliweza kuishi kwa amani na upendo kama ndugu na
tuendelee kuishi hivyo. Hatukupungukiwa na chochote na hatutapungukiwa na chochote,
zaidi tutapata hasara na madhara yatokanayo na vita kama tulivyoona hapo juu.
Tuiheshimu na kuitunza amani yetu kwa manufaa yetu binafsi na kizazi kijacho.
WAKRISTO.
“Mwanzo
1:27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume
na mwanamke aliwaumba”. Ikiwa sote tuliumbwa kwa mfano wa
Mungu basi sisi sote tu ndugu pasipo kuzingatia tofauti ya dini zetu.
“Warumi
12:18 mkae katika amani na watu wote “. Tunasisitizwa kuishi
kwa amani na kila mtu pasipo kuzingatia tofauti ya dini yake kwetu, na ili
tuishi kwa amani ni lazima tuitunze na kuilinda amani tuliyonayo na kuidumisha
zaidi.
Kila Mtanzania ni
lazima atafakari athari na matokeo ya uvunjifu wa amani mapema kabla hajakubali
kutumika katika uvunjifu wa amani.
“MUNGU IBARIKI TANZANIA,
MUNGU WABARIKI WATANZANIA, AMINA”.