UTANGULIZI
UTATU MTAKATIFU WA MUNGU (THE HOLY TRINITY OF GOD) |
Mungu ni nani?
Mungu ni Roho
takatifu aliyekuwapo milele iliyopita, aliyepo sasa na atakayekuwapo milele
ijayo (Yohana 4:24, 2 Wakorintho 3:17). Mungu hana mwili wa damu na nyama kama
tulivyo viumbe wengine na hana maumbo ya vitu asili visivyo hai kama milima
mikubwa. Mara nyingi Mungu alipojidhihirisha kwa wanadamu, alijidhihirisha kwa
sauti peke (Mwanzo 3, Isaya 6:8, Kutoka 19:9) na mara chache Mungu alijidhihirisha
kwa uwazi kabisa kwa mtumishi wake Musa (Kutoka 33:18-23). Ijapokuwa Musa
hakuwahi kuiona sura ya Mungu (alipata kibari cha kukiona kivuli cha Mungu
katika maumbo ya moto), kwa sababu Mungu ni Roho yenye utukufu mwingi, hakuna
mwanadamu atakayemuona Mungu kwa macho ya damu na nyama akaishi (Kutoka 33:20,
Yohana 1:18).
Sifa kuu tatu
(3) za Mungu
Omniscient
Neno hili
linatokana na neno “omniscience” neno linalomaanisha “ufahamu”. Mungu ni
“omniscient”, ikimaanisha ni mwenye ufahamu wa elimu zote. Mungu ni Roho
anayejua kila elimu na kamwe hakuna jambo jipya kwake ama analohitaji
kujifunza. Ni Mungu anayeujua mwisho wa kitu au jambo (mfano, uhai wa
mwanadamu) kabla ya mwanzo wa kitu au jambo husika (Isaya 46:10, Yeremia
10:12). Maarifa na hekima yote ya wanadamu wote wa dunia hii ni sawa na
upumbavu tu kwa Mungu (1 Wakorintho 1:25) kwa sababu kiwango chake cha ufahamu
ni juu mno.
Omnipotent
Neno “omnipotent”
linatokana na neno “omnipotence” linalomaanisha kuwa na nguvu ama uwezo
uliovuka mipaka ya vipimo ama akili za kibinadamu. Hivyo basi Mungu ni Roho
yenye uwezo usio na mipaka (kizuizi) katika kutenda jambo lolote. Naweza
kusema, “Mungu ni nguvu na nguvu ni Mungu”. Soma Biblia yako vifungu
vifuatavyo, Kumbukumbu la Torati 3:24, Zaburi 62:11, Ayubu 26:14, Ayubu 9:4,
Yeremia 10:12. Hakuna nguvu iliyowahi kuwashinda wanadamu ilimshinda Mungu,
kumbuka mfano mdogo tu, gharika/vimbunga vyote (mvua za vimbunga) zinazotokea
duniani kote hazijawahi kuzuiliwa na wanadamu zisifanye madhara zaidi ya
wanadamu kuzikimbia gharika/vimbunga hivyo. Kwa sababu mvua hizo zina nguvu
inayozidi uwezo wa wanadamu na fahamu zao zote. Lakini Mungu (Yesu Kristo)
alipokutana na dhoruba ya bahari aliikemea nayo ikatii na kukawa na utulivu
mkubwa (Matayo 8:26). Hii inadhihirisha uwezo na nguvu za Mungu namna zilivyo
kuu pasipo na mipaka ama ukomo wa utendaji kama wanadamu.
Omnipresent
Neno hili
linatokana na neno “omnipresence” lenye maana ya uwepo katika sehemu zote kwa
wakati wote/mmoja (ule ule). Mungu ni Roho iliyopo sehemu zote katika wakati
ule ule, yaani wakati huu unaposoma mafundisho haya, Mungu yupo mahali hapo
ulipo, yupo mahali alipo muandishi wa somo hili, yupo nchi zote za dunia hii.
Hivyo ndivyo Mungu alivyo, Mungu asiye na chanzo au asili wala mwisho (Ufunuo
1:8, Zaburi 139:7-12, Yeremia 23:24).
Sifa hizo kuu za
Mungu aliye hai, ambaye jina lake ni Jehova hakuna mungu mwingine yoyote
anayeweza kuwa nazo. Ni ajabu sana kuona baadhi ya watu wanaabudu miungu mfano
wa wanyama ama miti mikubwa ama milima mirefu. Ni ajabu zaidi kuona mwanadamu
anaabudu hata kinyago alichokitengeneza yeye mwenyewe. Nikusihi mpenzi msomaji
wangu, yupo Mungu mmoja tu wa kuabudiwa, anaitwa Yehova na ndiye Mungu
ninayemuhubiri kupitia jina la Yesu Kristo aliye hai.
MUNGU MMOJA,
NAFSI TATU (UTATU MTAKATIFU WA MUNGU)
Nafsi ni nini?
Kabla ya
kuendelea kumjua Mungu katika nafasi tatu anazochukua yaani nafsi tatu ambazo
ni Mungu Baba, Mungu mwana na Roho Mtakatifu, hebu tuangalie nini maana ya
nafsi? Kwa lugha ya kigeni, neno nafsi linajulikana kama “soul’ wakati neno
roho linajulikana kama “spirit”. Mungu ni Roho na wakati huo huo ni Nafsi tatu
ndani ya Roho moja. Tofauti na mwanadamu ambaye ana roho, nafsi na mwili, Mungu
hana mwili wa nyama na damu kama hii tuliyonayo sisi wanadamu au viumbe wengine
mfano wanyama.
Nafsi ni hisia
au matamanio yanayoongoza matendo au tabia za mwili. Kwa maana nyingine, nafsi
ni hisia au matamanio yanayoamua ubinadamu wa mtu. Nafsi za wanadamu zinaishi
kwa kufuata matamanio ya vitu vionekanavyo kwa macho hapa duniani. Na ndio
sababu mwanadamu anayeishi kwa kufuata tamaa za nafsi yake kamwe hawezi
kumpendeza Mungu. Hata hivyo, roho ya mwanadamu inaishi kumpendeza Mungu
ikishindana na nafsi. Hadi pale mwanadamu anapopokea neema ya kuongozwa na Roho
Mtakatifu ndipo roho yake itaweza kuishinda nafsi na hivyo kuisha maisha ya
kumpendeza Mungu.
Kwa hiyo,
matendo ya Mungu yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo yanatufanya
tumuone Mungu mmoja ndani ya nafsi tatu. Matendo hayo ndiyo tabia za Mungu.
Hebu tuangalie tabia au matendo hayo ya Mungu katika nafsi tatu.
Mungu Baba
Roho ya Mungu
inaopochukua tabia ya uumbaji (kuzaliwa jambo jipya kimwili/kimaumbile au
kiroho), inachukua nafsi ijulikanayo kama Mungu Baba. Katika uumbaji wa viumbe
vyote tunavyoweza kuviona kwa macho yetu na hata vile tusivyoweza kuviona
ambavyo vina udogo usioweza kuonekana kwa macho mfano wa vimelea vya bakteria,
hapa Mungu anaitwa Mungu Baba (mzazi). Mzazi ni chanzo au asili ya maisha ya
ina fulani. Soma Bibli yako katika vifungu vifuatavyo; Mwanzo 1:1, Wakolosai
1:16. Mungu katika nafasi ya uumbaji wa ulimwengu wote na kuwa chanzo ama asili
ya aina zote za maisha/uhai anachukua nafsi ya Mungu Baba. Na kwa namna hiyo,
muimbaji mmoja (Don Moen) alipompima Mungu katika nafasi hiyo akamuita Jina la
“Creator King”, hakika jina hili ni tamu ulimini, nafsini na hata rohoni.
Mungu Mwana
Kulitokea
vipindi viwili vya maangamizo makuu, ambavyo Mungu aliamua kuwaangamiza
wanadamu kutokana na kuongezeka kwa maasi katika dunia. Vipindi hivyo ni wakati
wa gharika ya Nuhu (Mwanzo 6, Mwanzo 7) na wakati wa Sodoma na Gomora (Mwanzo
19). Licha ya maangamizo hayo, bado wanadamu waliendelea kutenda dhambi. Siyo
kwa sababu wanadamu wanapenda sana dhambi, la hasha, ni kwa sababu nafsi ya
mwanadamu inavutwa na matamanio ya kuipendeza dunia na siyo Mungu. Kwa sababu
hiyo Mungu akaonelea atafute namna ya kutusaidia wanadamu ili tuweze kuushinda
ulimwengu (dhambi) na tuishi maisha ya kumpendeza (Mwanzo 9:11).
Hivyo basi,
Mungu akachukua mwili wa udhaifu (mwili wa damu na nyama), akazaliwa na bikira
Maria kwa makusudi maalumu ya kuachilia neema ya ukombozi kwa mwanadamu
aliyepotea dhambini (Mathayo 1:18-20). Mateso yote aliyoyapitia Yesu Kristo;
kukamatwa kama mwizi, kupigwa na kuchapwa mijeredi kama muhalifu, dhihaka za
kutemewa mate na kutukanwa, maumivu ya kuubeba msalaba mzito (msalaba
unaokadiriwa kuwa na uzito usiopungua kilogram 135) juu ya mwili uliodhohofu na
kuchakaa kwa mateso ya usiku kucha na asubuhi yote, maumivu ya misumali
iliyoubeba mwili juu ya msalaba na taji ya miiba kichwani….hakika Bwana wetu
Yesu Kristo alivumilia sana pasipo kutoa neno la lawama. Mateso hayo yalipaswa
tuyachukue kila mmoja wetu ili kulipia thamani ya ukombozi wetu kutoka ufalme
wa giza (ufalme wa shetani) na kuandikishwa katika ufalme wa nuru (Ufalme wa
Mungu), soma Biblia yako katika kitabu cha Isaya 53. Huu ni upendo wa ajabu
kabisa, Mungu kuvaa udhaifu na kupokea mateso (kwa nafasi zetu) ili sisi wenye
dhambi tukombolewe kwa neema na siyo kwa mapigo ya gharika ya maji au moto wa
Sodoma na Gomora.
Katika sura hii
ya upendo kwa mwadamu, Mungu anapokea tabia ya nafsi iitwayo Mungu katika nafsi
ya pili yaani Mungu Mwana. Tofauti na wanadamu, Mungu hahesabu maovu
tuliyomtendea ili atusamehe. Anatusamehe wote sawa, dhambi kubwa ama ndogo,
nyingi ama chache (kwa kipimo cha mwanadamu), Mungu aliyehai, Yehova
anatusamehe zote, wote, sawa. Hakuna anayesamehewa dhambi nusu na mwingine
zote, wote tunasamehewa dhambi zote kwa kila mmoja na wingi wa dhambi zake na
ukubwa wa dhambi zake, akiisha tutakasa anatufanya watoto wake na warithi
pamoja naye (Warumi 8:16-17).
Mungu Roho
Mtakatifu
Mungu yule yule
katika nafsi ya tatu, anajulikana kama Mungu Roho Mtakatifu. Kama tulivyoona
hapo juu, mwanadamu ameumbiwa roho (inayotenda kutimiza mapenzi ya Mungu) na
nafsi (inayovutwa na tamaa za dunia ili kutimiza mapenzi ya mwili). Nafsi ya
mwanadamu kamwe haiwezi kushinda tamaa za mwili kuipendeza dunia, kwa namna
yoyote ile mwili wa mwanadamu utatenda dhambi na kumchukiza Mungu. Hiyo ni
nguvu ya nafsi kutimiza matamanio ya mwili yenye dhambi. Na huu ni udhaifu wa
kila mwanadamu. Ndipo Mungu anaamua kutukamilisha ili tuzishinde nafsi zetu na
kuisha maisha ya kumpendeza katika uchaji wa dhati usio na mawaa (Warumi
8:26-28, Wagalatia 4:6-7, na 1 Yohana 3:24).
Vivyo hivyo,
Mungu analihudumia kanisa lake kama ahadi ya Yesu Kristo ya kutotuacha yatima
(Yohana 14:16). Kupitia huduma mbalimbali zinazoongozwa na Roho Mtakatifu ndani
ya kanisa (Warumi 12:1-8, 1 Wakorintho 12:1-11), Mungu anaendelea kutufundisha
kumjua, kumtumikia na kumuishia yeye ili tupate ukamilifu katika imani na
kuweza kusimama imara kama mashahidi wa haki tukiushuhudia ukombozi wa Yesu
Kristo kwa wenye dhambi ulimwenguni kote (Yohana 14:26, Yohana 15:26).
HITIMISHO
Mungu ni Roho
takatifu anayeishi milele na ndiyo chanzo na asili ya ulimwengu wote na aina
zote za maisha (viumbe) ndani ya ulimwengu. Mungu anatenda kazi kupitia nafsi
tatu ambazo ni Mungu Baba, Mungu Mwanza (Yesu Kristo) na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu
anawapenda wenye dhambi, anawakomboa kutoka utumwa wa shetani na kuwarejesha
katika ufalme wake kupitia Mungu Mwana. Kwa sababu ya udhaifu wa nafsi ya
mwanadamu katika kuipenda dunia na anasa zake, Mungu anatutia nguvu za kuushinda
ulimwengu kupitia Roho Mtakatifu.