Thursday, February 14, 2013

TOBA YA KWELI.



   Kuna tofauti kubwa kati ya toba na toba ya kweli, toba haimalizi kosa/dhambi lakini toba ya kweli inamaliza kosa/dhambi. Na baada ya toba ya kweli, Mungu huzifuta dhambi zetu zote (Isaya 43:25). Unapoamua kufanya toba, fanya toba ya kweli maana hiyo ndiyo toba yenye msamaha wa dhambi ndani yake.

   Toba na toba ya kweli zina sifa kadhaa zinazofanana; kutambua kosa/dhambi, kulijutia na kuliombea msamaha.
Tofauti ya toba na toba ya kweli ni kuacha kuitenda tena dhambi uliyokwisha kuiombea msamaha, hii ndiyo toba anayoipenda na kuitaka Mungu.

TOBA.
   Mathayo 27:3, 5 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona amekwisha kuhukumiwa, alijuta akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”. 

Toba ni kulitambua kosa, kulijutia na kuliombea msamaha. Muomba toba anaweza akayarudia makosa au anaweza akalitambua kosa na akalijutia lakini asiliombee msamaha. Na jinsi unavyorudia kosa au unafanya kosa, unalijutia lakini hauliombei msamaha ndivyo hofu ya Mungu inavyozidi kuondoka ndani yako na dhamira ya kukufanya uitambue dhambi na kuijutia nayo inatoweka. Mtu wa namna hii anafikia mahali anakufa kiroho, na mfu wa roho ni kazi sana kumrudia Mungu. Mtu huyu anahitaji huduma ya ukombozi yenye neema ya Mungu mwenyewe. (Luka 11:24-26).

Shetani ndiye anayewadanganya watu kwamba wametenda dhambi kubwa sana zisizo na msamaha, na hata kuiua dhamira iliyo ndani ya mtu ili mtu huyo asitafute toba ya kweli. 

TOBA YA KWELI.
   Luka 15:11-19 “. . . nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa naye amefufuka, alikuwa amepotea naye ameonekana.”

Toba ya kweli ni kulitambua kosa, kulijutia, kuliombea msamaha na kutolitenda tena. Toba ya kweli urudisha utukufu na hofu ya Mungu kwako. Ili usirudie tena dhambi uliyokwisha iombea msamaha unapaswa kujikita katika maombi na kuepukana na mazingira yasababishayo dhambi hiyo. (Zaburi 1:1-2 na Waefeso 4:28).

Hakuna dhambi isiyo na msamaha kwa Mungu, dhambi zote zinasamehewa kwa sababu neema na rehema za Mungu ni juu ya wanadamu wote, wote tunaweza kusamehewa ikiwa tutafanya toba ya kweli. (Zaburi 103:11-13 na 2 Wakorintho 5:17).

Unataka kumpokea Yesu Kristo leo? Bonyeza hapa.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts