Mwanadamu wa kwanza aliumbwa katika ukamilifu; kiroho na
kimwili, mtakatifu asiyejua dhambi na mwenye mwili usioonja mauti. Baada ya
kuasi agizo la Mungu na kutenda dhambi, akapoteza ukamiliu wa utakatifu, lakini
kwa vile Mungu ni pendo, anatupenda wanadamu akatuandalia ukombozi ili atununue
kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika Ufalme wa Mwana wa pendo
lake, Yesu Kristo.
Lakini kuupokea ukombozi huo, ni hiyari ya mwanadamu
mwenyewe, kwani baada ya kuitambua dhambi mwanadamu huyu alipata utashi wa
kutambua wema na uovu (Mwanzo 3:7).
Kumbukumbu la Torati 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu
yenu hivi leo, kuwa nimeweka mbele yako uzima na mauti… basi chagua uzima ili
uwe hai, wewe na uzao wako”.
Yeremia 21:8 “Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi,
tazama naweka mbele yenu njia ya uzima na njia ya mauti”.
Katika kitabu cha Torati, Mungu anaapa (anazishuhudiza) kwa
mbingu na nchi kuwa ametuwekea wanadamu njia mbili mbele yetu, ambazo ni uzima
na mauti. Na kwa sababu Mungu ni pendo, anatushauri kuichagua njia ya uzima.
Na siyo anatushauri tu, pia anatupa na sababu ya kwanini
anatushauri kuchagua uzima, anasema ili uwe hai. Kuwa hai ni kupokea uzima wa
milele, baada ya hukumu yenye kutisha ya Mungu yenye haki, siku atakapo tuhukumu
wanadamu sawa sawa na matendo yetu.
Na katika kitabu cha Yeremia, Mungu anarithibitisha neno
lake kuwa ameweka njia mbili mbele yetu; moja ni njia itupayo uzima na nyingine
ni njia ya mauti. Ni juu yetu kuamua tunachagua na kuifuata njia ipi.
Kuchagua njia ya uzima ni lazima kwanza uifahamu hiyo njia,
ni ipi na unawezaje kuichagua na kuifuata. Njia ya uzima ni Yesu Kristo,
kuchagua njia ya uzima ni kumchagua na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na
mwokozi wa maisha yako. Na kuifuata njia ya uzima ni kutimiza na kutenda mapenzi
ya neno la Mungu, kufuata na kushika neno la Yesu mwenyewe kwa matendo dhahiri.
Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na
uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi”.
Ile njia ya uzima ambayo Mungu aliziapia mbingu na nchi kuwa
ameiweka mbele yetu na kutushauri kuichagua na kuifuata hiyo, ndiyo hiyo
inafunuliwa katika kitabu cha Yohana Mtakatifu. Yesu mwenyewe anajidhihirisha
kuwa yeye ndiye njia, na siyo njia tu, ina uzima ndani yake amboyo kupitia hiyo
tunaurithi Ufalme wa Mungu.
Kuchagua njia ya uzima kunapaswa kuendane na matendo ya
uzima, tusikiri kwa maneno ya vinywa vyetu kuwa tunao uzima (tumempokea Yesu
Kristo) na wakati huo huo matendo yetu ni kinyume na kukiri kwetu.
Mathayo 3:8 “Basi zaeni matunda yapasayo toba”, matunda ni
matendo na toba ni kuupokea uzima, sasa matendo yetu yanapaswa kuenenda kama
jinsi tulivyoupokea huo uzima.
Cha kushangaza, Wakristo wengi wa siku hizi wanatenda
kinyume na wanavyokiri katika vinywa vyao. Na kusababisha jina la Mungu
litukanwe.
Tito 1:16 “Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa
matendo yao wanamkana”, kukiri kuwa umempokea Yesu Kristo na unahudhuria katika
nyumba za ibada lakini matendo yako ni kinyume na kukiri kwako ni sawa na
kupoteza muda!
Kuchagua njia ya uzima na kutoifuata kwa matendo njia hiyo
kunamadhara yafuatayo;
Kulitukanisha jina la Yesu; watu wanapoyatazama matendo yetu
wanategemea kuona maisha yetu yakiakisi maisha halisi ya Yesu Kristo, na
inapokuwa tofauti ndipo jina la Yesu linapotukanwa (2 Petro 2:2).
Kurithi mauti na kuzimu; kutotembea katika njia ya uzima ni
kutembea katika njia ya mauti, na kutembea katika njia ya mauti ni kuchagua
mauti (Mithali 12:28, 15:24).
Njia utakayopita katika uhai wako ndiyo njia utakayo iendea
baada ya kifo, ikiwa umechagua njia ya uzima lakini unapita katika njia ya uovu
basi baada ya kifo pia utaiendea njia uliyokuwa ukiipitia. Hapa haijarishi ni
dua, swala au maombi mengi kiasi gani utafanyiwa wakati wa mazishi yako.
Unachochagua
kuishi ndicho utakacho tunukiwa.
Mathayo 16:27 “… ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya
matendo yake”, kila mmoja wetu atalipwa kwa kadiri ya alivyotenda alipokuwa hai
na siyo kwa kadiri ya sala za kumuombea awekwe pema peponi (Yohana 5:28-29).
Kama umechagua njia ya uzima, tembea katika njia ya uzima
maisha yako yote kwa uaminifu.