Msamaha ni kufuta
au kuachilia mzigo wa makosa unayotendewa na mtu pasipo kuhesabu ni mara ngapi
mtu huyo amekukosea.
Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi ndimi niyafutaye makosa yako
kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako”.
Hapo neno la Mungu linatufundisha kuwa; msamaha ni kuyafuta
makosa (dhambi) na kutoyakumbuka tena.
Luka 6:37b “…achilieni, nanyi mtaachiliwa”.
Hapa tunaona kuwa maana nyingine ya msamaha ni kuachilia; mtu
anaposhindwa kusamehe anabeba mzigo wa hasira ndani ya moyo wake, ambapo mzigo
huu unaweza kumfanya mtu huyu akose raha, amani na hata furaha. Hapo Mungu
anatuambia tuachilie na kutua mizigo iliyo ndani ya mioyo yetu.
AINA ZA MSAMAHA.
Kuna aina mbili za kusamehe, aina hizi ni;
(a). Msamaha wa
kidunia.
Huu ni msamaha wa kusamehe na kutosahau. Msamaha huu
hautokani na Mungu, na haukubaliki mbele za Mungu.
Ni msamaha wa kinafiki, mtu anakwambia amekusamehe lakini
ndani ya moyo wake ana uchungu nawe. Msamaha huu unahesabu makosa, na wengu
wameumia kwa sababu ya kusamehe kwa kutumia msamaha wa aina hii. Unapomwambia mtu
nimekusamehe na kumbe bado una uchungu naye, yeye anapata amani na furaha
lakini wewe unajawa na uchungu na hasira inayokufanya uumie moyo.
Wengi wetu tumekuwa na msamaha wa aina hii, Mungu atusaidie
tuwe na msamaha wa Kimungu kwani msamaha huu una raha na faida. Kuna watu
wamekonda na hawana raha siyo kwa sababu ya maisha magumu, bali ni kwa sababu
wanavinyongo na mizigo mizito ndani ya mioyo yao.
(b). Msamaha wa Kimungu.
Huu ni msamaha wa
kusamehe na kusahau kabisa. Msamaha huu ni wa Mungu na unatokana na Mungu
mwenyewe, kwani Mungu anasema yeye anatusamehe na kusahau kabisa makosa yetu
(Isaya 43:25). Nasi kama watoto wa Mungu tunapaswa kuwa na tabia ya Mungu
katika kusamehe, tunapaswa tusamehe na kusahau yote tunayokosewa na wenzetu.