Msamaha ni kufuta
au kuachilia mzigo wa makosa unayotendewa na mtu pasipo kuhesabu ni mara ngapi
mtu huyo amekukosea.
Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi ndimi niyafutaye makosa yako
kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako”.
Hapo neno la Mungu linatufundisha kuwa; msamaha ni kuyafuta
makosa (dhambi) na kutoyakumbuka tena.
Luka 6:37b “…achilieni, nanyi mtaachiliwa”.
Hapa tunaona kuwa maana nyingine ya msamaha ni kuachilia; mtu
anaposhindwa kusamehe anabeba mzigo wa hasira ndani ya moyo wake, ambapo mzigo
huu unaweza kumfanya mtu huyu akose raha, amani na hata furaha. Hapo Mungu
anatuambia tuachilie na kutua mizigo iliyo ndani ya mioyo yetu.
AINA ZA MSAMAHA.
Kuna aina mbili za kusamehe, aina hizi ni;
(a). Msamaha wa
kidunia.
Huu ni msamaha wa kusamehe na kutosahau. Msamaha huu
hautokani na Mungu, na haukubaliki mbele za Mungu.
Ni msamaha wa kinafiki, mtu anakwambia amekusamehe lakini
ndani ya moyo wake ana uchungu nawe. Msamaha huu unahesabu makosa, na wengu
wameumia kwa sababu ya kusamehe kwa kutumia msamaha wa aina hii. Unapomwambia mtu
nimekusamehe na kumbe bado una uchungu naye, yeye anapata amani na furaha
lakini wewe unajawa na uchungu na hasira inayokufanya uumie moyo.
Wengi wetu tumekuwa na msamaha wa aina hii, Mungu atusaidie
tuwe na msamaha wa Kimungu kwani msamaha huu una raha na faida. Kuna watu
wamekonda na hawana raha siyo kwa sababu ya maisha magumu, bali ni kwa sababu
wanavinyongo na mizigo mizito ndani ya mioyo yao.
(b). Msamaha wa Kimungu.
Huu ni msamaha wa
kusamehe na kusahau kabisa. Msamaha huu ni wa Mungu na unatokana na Mungu
mwenyewe, kwani Mungu anasema yeye anatusamehe na kusahau kabisa makosa yetu
(Isaya 43:25). Nasi kama watoto wa Mungu tunapaswa kuwa na tabia ya Mungu
katika kusamehe, tunapaswa tusamehe na kusahau yote tunayokosewa na wenzetu.
FAIDA ZA KUSAMEHE.
Unaposamehe wengine unapa faida zifuatazo ambazo hakuna njia
nyingine ya mkato ya kuzipata faida hizi zaidi ya kusamehe kwa dhati (kasamehe
na kusahau, kusamehe na kutohesabu makosa).
(a). Kusamehewa.
Tunapo wasamehe
waliotukosea na kutokumbuka waliyotukosea, Mungu wetu naye anatusamehe sisi
makosa yetu.
Luka 11:4 “Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi
tunamsamehe kila tumwiaye”. Hii sehemu ya sala aliyotufundisha Bwana wetu Yesu
Kristo, kwamba tunapaswa kumuomba Mungu msamaha ikiwa tu, nasi tunawasamehe
wanaotukosea. Kwa maana hiyo Mungu huwasamehe watu makosa yao endapo watu hao
nao wanawasamehe wenzao wanao wakosea.
(b). Kuyapa kibali
maombi yetu mbele za Mungu.
Tunapo wasamehe
wenzetu kwa dhati, naye Mungu wetu anatusamehe sisi na akiisha tusamehe
anayakubali maombi yetu tunayoyapeleka mbele zake. Hivyo tunapata uhakika wa
kujibiwa.
Marko 11:25 “Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni,
mkiwa na neno juu ya mtu”. Hapa pia Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwa
kila tunapoingia katika maombi ni lazima tuwasamehe kwa dhati na kusahau makosa
yao wale wote walio tukosea na ndipo tuendelee na maombi yetu.
HASARA YA KUTOSAMEHE.
Unapokosa msamaha
wa kweli kwa wanaokukosea unjifungia mlango wa kusamehewa na Mungu, unayanyima
kibali maombi yako mwenyewe mbele za Mungu, na unabeba mzigo ambao utakuumiza
na kuutesa moyo wako.
Na pia unapokosa msamaha kwa wakosaji wako, unamfanya Mungu
asipokee sadaka yako hata ingekuwa kubwa kiasi gani au umejitoa kwa moyo wote
kiasi gani. Samehe kwanza na ndipo utoe sadaka yako tena kwa moyo wa kupenda
nayo itapata kibali mbele za Mungu naye ataitakabali na kukubariki kwa hiyo.
Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku
ukikumbuka ya kuwa ndugu yako na neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya
madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kasha urudi uitoe sadaka
yako”. Hayo ni maneno ya Mungu mwenyewe kupitia Mwana wake, Bwana wetu Yesu
Kristo, kwamba endapo tumefarakana au tumekosana na mtu yoyote ni lazima
tupatane naye kabla ya kutoa sadaka zetu. Haipo maana kama tunatoa sadaka nasi
tumeshindwa kuwasamehe wenzetu.
Ndugu yangu mpendwa katika Kristo Yesu, ninakusihi uwe
mwepesi wa kusamehe na kusahau. Na kama unaona huwezi kusamehe na kusahau,
muombe Yesu Kristo akusaidie kwani yeye ndiye Bwana wa yote, name ninakuhakikishia
kuwa kwa Jina la Yesu Kristo wa Nazareti mambo yatakuwa sawa. Amina.
No comments:
Post a Comment