Saturday, October 27, 2012

AHADI YA MUNGU HUTUJENGEA IMANI ITUPAYO HAKI.


Ahadi za Mungu.
   Mungu amefanya ahadi nyingi kwa mwanadamu; ahadi za uponyaji, mafanikio, heshima, hekima, ufaulu katika masomo na nyingine nyingi. Na wengi wetu tunazifahamu vizuri ahadi hizo alizotuahidi Mungu; tunazisoma katika neno lake takatifu, Biblia na pia tunazisikia kupitia watumishi mbalimbali wa Mungu.
Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya, Kwa maana wewe upo pamoja nami”,  na  Zaburi 119:50 “Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imeniuhisha”.
   Kupita kati ya bonde la uvuli wa mauti (Zaburi 23:4) na kuwa katika taabu (Zaburi 119:50) ni kuingia au kupitia katika hali zenye changamoto mbalimbali za kiafya; magonjwa na udhaifu wa mwili, kielimu; kushindwa kutimiza malengo yako, kiuchumi; hali ngumu ya kiuchumi au kukosa ajila licha ya kuwa na elimu stahiki, kijamii; kukosa watoto kwa miaka mingi katika ndoa na hata jamii inakuita tasa, kufiwa na watoto pale tu wanapozaliwa na changamoto za namna nyingine nyingi. Katika neno la Mungu hapo juu tunafundishwa kwamba kuna nyakati tutaingia katika changamoto, taabu au bonde la uvuli wa mauti katika maisha yetu. Jambo la kujiuliza hapa, je tuingiapo katika changamoto au taabu hizo tunachukua hatua gani? Je, tumekuwa ni watu wa kumlaumu Mungu kwanini ameruhusu tuingie katika taabu? Na kama tumekuwa ni watu wa kulaumu na tunasubiri majibu kutoka kwa Mungu hakika Mungu hata tujibu kamwe, kwa sababu Mungu hana majibu ya lawama. Mungu anayo majibu ya maneno au maombi yenye hoja zilizojengwa katika imani ya neno lake tu.
   Na ndiyo maana kupitia mistari ya neno la Mungu hapo juu anatufundisha kuwa na imani kwa ahadi zake kwetu.  Anaposema “sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami”, Mungu kuwa pamoja naye ni kwamba ahadi ya Mungu ya ukombozi imemfunika na ni lazima atatoka katika bonde hilo la uvuli wa mauti, na “ahadi yako imeniuhisha” anamaanisha hawezi kukata tama pasipo kujali anapitia taabu ya namna gani kwa sababu ukombozi wake unakuja tena uko karibu.
   Na sisi tunapopitia katika mahangaiko, taabu, shida na misukosuko ya maisha tusiwe ni watu wa kulaumu na kulalamika mbele za Mungu, bali tuwe ni watu wenye kusimama katika maombi yenye imani ya ukombozi tukiziangalia ahadi za Mungu katika taabu zetu.

Mungu anazithibitisha ahadi zake.
Isaya 55:10-11 “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;  ndivyo litakavyo kuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”.
   Neno litokalo katika kinywa cha Mungu ni ahadi ya Mungu kwa wanadamu; ahadi ambayo Mungu mwenyewe anaifananisha na mvua, jinsi ambavyo haikuwahi kutokea mvua imenyesha kuelekea mbinguni bali kutoka juu kuja chini, ndivyo zilivyo ahadi za Mungu kwetu, kamwe hazitamrudia Mungu hadi zitimize mapenzi ya Mungu kupitia ahadi zile. Ukifika wakati wa masika (mvua kunyesha), mkulima huliandaa shamba na kulipanda mbegu akiwa na imani mvua itanyesha na mbegu alizopanda zitachipua na kuzaa matunda ambayo ni mazao bora. Nasi tunapaswa kuwa na imani kama mkulima huyu, jinsi anavyoamini kuwa mvua itanyesha hata akaandaa shamba nasi pia inatupasa tuwe na imani kuwa ahadi ya neno la Mungu ni lazima itatimia. Hatuamini kwa kubahatisha, tunaamini kwa sababu tunamjua Mungu wetu hajawahi kushindwa, yeye ndiye aliyefanya juzi na jana basi atafanya na leo pia. Na zaidi, Mungu wetu mwenyewe amethibitisha kuitimiza ahadi iliyo katika neno lake (Isaya 55:10-11).
   Hivyo basi napenda kukutia moyo mpendwa, usiangalie ni nyakati za namnna gani ulizopo au ni mazingira ya namna gani yanakuzunguka, wewe iangalie ahadi ya Mungu katika shida na taabu yako na uwe na moyo wa imani kwamba iko siku Mungu mwenyewe anaenda kukushika kwa mkono wake na kukuvusha katika mapito hayo kwani ameithibitisha ahadi yake na amethibitisha kuitimiza ahadi hiyo.
Ahadi ya Mungu huleta imani.
   Tunapoitambua ahadi ya Mungu na kuipokea kwa moyo usio na mashaka au wasiwasi, tunajenga imani ndani yetu mabayo kupitia hiyo Mungu anakwenda kufanya jambo jema katika maisha yetu. Na ndiyo sababu Yesu Kristo alipokuwa akifanya uponyaji kwa watu wenye magonjwa na kuwafungua waliofungwa na nguvu za mapepo aliwaambia “imani yako imekuponya”. Watu hawa walimuamini Yesu kuwa anao uwezo wa uponyaji, na kupitia imani hiyo Yesu Kristo aliwaponya. Nasi tunapaswa kuziamini ahadi zilizopo katika neno la Mungu.
Warumi 4:20 “Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu”, mtu huyu (Ibrahimu) alipewa ahadi ya kuwa baba wa mataifa kipindi ambacho hata mtoto mmoja hakuwa naye, lakini kwa sababu aliyempa ahadi hiyo alikuwa ni Mungu, naye Ibrahimu alipoikumbuka ahadi ya Mungu alijawa na imani moyoni mwake kwani alijua iko siku ahadi hiyo ingetimia na ndipo alipoimba sifa za kumtukuza Mungu. Nasi tunapaswa tuwapo katika uhitaji, shida au taabu tuitazame ahadi ya Mungu kwa imani thabiti huku tukimpa Mungu sifa.
Mwanzo 15:5-6 “Akamleta nje, akasema, tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia ndivyo utakavyokuwa uzao wako.(Ibrahimu) Akamwamini Bwana.”
Imani huleta haki.
Warumi 4:21-25 “huku akijua hakika(pasipo kuwa na shaka, imani) ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi(ahadi ya Mungu). Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki(kutokana na imani). Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi tutakaohesabiwa vivyo hivyo(tunaoamini)”.
Mwanzo 15:6 “Akamwamini Bwana, naye (Bwana) akamhesabia jambo hili kuwa haki”.
Neno la Mungu linatufundisha kuwa iwapo tutaziamini ahadi za Mungu kuwa ni hakika na kweli, Mungu atazihesabu ahadi zake kwetu kuwa ni haki zetu. Haki ni jambo au kitu ambacho ni lazima ukipate tena pasipo jitihada zozote, unazaliwa nacho. Kwa maana hiyo, tunapoziamaini ahadi zilizopo katika neno la Mungu; Mungu mwenyewe anatuhesabia haki ya kuzipata ahadi hizo, hivyo ni lazima atatimiza alichokiahidi.
Haki husababisha matokeo ya imani.
2 Samweli 22:21a,25a “Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu, Basi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu”.
Hapo Mungu anatufundisha kuwa, yeye huwalipa wanadamu kulinga na haki zao; mwenye haki ya kuponywa, humponya; mwenye haki ya heshima, huheshimika; mwenye haki ya kubarikiwa, humbariki; mwenye haki ya kufaulu masomo, humpa kufaulu; mwenye haki ya utajiri, humtajirisha. Kila mmoja hutendewa sawasawa na haki aliyonayo, yaani utendewa sawasawa na imani aliyonayo. Mwenye imani ndogo hutendewa kidogo na mwenye imani kubwa hutendewa makubwa, kwani imani ndogo huleta haki kidogo na imani kubwa huleta haki kubwa. Ndugu mpendwa, kama Mungu amewahi kukufanyia jambo hata kama ni dogo kiasi gani kwa mtazamo wako, mwamini kuwa hata hilo unaloliona ni kubwa analiweza pia.
Ayubu 33:26 “Yeye humwomba Mungu(kwa imani), naye(Mungu) akamtakabalia(akapata kibali machoni pa Mungu, kwa sababu ya imani iliyo ndani yake); hata auone uso wake kwa furaha; Naye(Mungu) humrejezea mtu haki yake(aliyoipata kwa kuiamini ahadi ya Mungu)”.
Katika kuhitimisha, ninapenda nikwambie ndugu mpendwa katika Yesu Kristo; ahadi zilizopo katika neno la Mungu ni hakika na kweli kwa sababu Mungu mwenyewe amezithibitisha. Hatua unayotakiwa kuchukua, ni kuziamini ahadi hizo ili upate haki itakayokupa matokeo ya ahadi zilizopo katika neno la Mungu, na hutakuwa mtu wa kushuhudiwa tena bali utakuwa ni mtu wa kuyashuhudia matendo makuu anayoyafanya Mungu katika maisha yako. Amina.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts