Thursday, March 27, 2014

2. KUMJUA MUNGU, MUNGU KUKUJUA NA KUMJULISHA MUNGU KWA WENGINE

Bwana Yesu asifiwe sana mpendwa msomaji wangu!

Tunaendelea na somo letu lenye kichwa, "HATUA ZA KUUKULIA WOKOVU NA NEEMA YA MUNGU", na sasa tupo sehemu ya pili. ni imani yangu kuwa Roho wa Mungu atakuhudumia. Endelea...



(a). Kumjua Mungu
Yeremia 9:23-24. Bwana asema hivi, mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisisfu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana.

Unapochukua uamuzi wa kuokoka au kuamua kuwa mfuasi wa Mungu na Yesu Kristo, ni lazima umjue huyo Mungu unayemtumikia kwa kina na marefu. Ni lazima uujue uwezo wake, nguvu zake, neema zake, rehema zake na kila kitu kumuhusu yeye. Kama utakuwa unamuabudu na kumtumikia Mungu usiyemjua, ni lazima utakuwa mfuasi wa dini na siyo mfuasi wa Mungu unayedai kumtumikia. Na kwa taarifa yako, ukikubali kuwa mfuasi wa dini na siyo Mungu aliye hai, Yehova na Yesu Kristo basi unapoteza muda wako.

Kumjua Mungu siyo jambo jepesi kiasi unachoweza kufikiria, ni kazi ngumu kama kazi ngumu nyingine unazozijua. Inahitaji uvumilivu na nia thabiti ya moyo katika kumjua Mungu ipasavyo(Kutoka 33:13). Kwa tabia za waumini wa siku hizi, za kwenda nyumba ya ibada na kusubiri kusikiliza mahubiri na shuhuda mbali mbali za watu ni vigumu kumjua Mungu wanayemtumikia.

Kinachohitajika hapa ni muumini au mfuasi wa Mungu na Yesu Kristo kuchukua hatua thabiti na kuvaa moyo wenye nia ya kumjua Mungu, wewe mwenyewe unatakiwa kumtafuta Mungu ipasavyo (Mithali 8:17), Mungu mwenyewe anasema wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

Kumjua Mungu ni lazima uwe rohoni, kwa sababu Mungu ni Roho na anafunuliwa kwa watu waliopo rohoni tu kupitia Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ni lazima ukubali kuwa rohoni na ukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu ili umjue Mungu (1 Wakorintho 2:9-12).

Kutokumjua Mungu unayemtumikia kuna hatari kubwa sana; kwanza hutomwabudu katika roho na kweli, hutomuamini kwa kiwango kinachotakiwa. Pili utayumbishwa na imani zinazoibuka kila leo. Na tatu, unaweza kuabudu miungu na siyo Mungu pasipo wewe kujua. Chukua hatua ya kuamua kumjua Mungu ipasavyo.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts