Tunaendelea na somo letu lenye kichwa, "HATUA ZA KUUKULIA WOKOVU NA NEEMA YA MUNGU", na sasa tupo sehemu ya pili. ni imani yangu kuwa Roho wa Mungu atakuhudumia. Endelea...
(a). Kumjua Mungu
Yeremia 9:23-24. Bwana
asema hivi, mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye
nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya
utajiri wake; bali ajisifuye na ajisisfu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu
mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki,
katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana.
Unapochukua uamuzi wa
kuokoka au kuamua kuwa mfuasi wa Mungu na Yesu Kristo, ni lazima umjue huyo
Mungu unayemtumikia kwa kina na marefu. Ni lazima uujue uwezo wake, nguvu zake,
neema zake, rehema zake na kila kitu kumuhusu yeye. Kama utakuwa unamuabudu na
kumtumikia Mungu usiyemjua, ni lazima utakuwa mfuasi wa dini na siyo mfuasi wa
Mungu unayedai kumtumikia. Na kwa taarifa yako, ukikubali kuwa mfuasi wa dini
na siyo Mungu aliye hai, Yehova na Yesu Kristo basi unapoteza muda wako.
Kumjua Mungu siyo jambo
jepesi kiasi unachoweza kufikiria, ni kazi ngumu kama kazi ngumu nyingine
unazozijua. Inahitaji uvumilivu na nia thabiti ya moyo katika kumjua Mungu
ipasavyo(Kutoka 33:13). Kwa tabia za waumini wa siku hizi, za kwenda nyumba ya
ibada na kusubiri kusikiliza mahubiri na shuhuda mbali mbali za watu ni vigumu
kumjua Mungu wanayemtumikia.
Kinachohitajika hapa ni
muumini au mfuasi wa Mungu na Yesu Kristo kuchukua hatua thabiti na kuvaa moyo
wenye nia ya kumjua Mungu, wewe mwenyewe unatakiwa kumtafuta Mungu ipasavyo
(Mithali 8:17), Mungu mwenyewe anasema wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
Kumjua Mungu ni lazima
uwe rohoni, kwa sababu Mungu ni Roho na anafunuliwa kwa watu waliopo rohoni tu
kupitia Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ni lazima ukubali kuwa rohoni na ukubali
kuongozwa na Roho Mtakatifu ili umjue Mungu (1 Wakorintho 2:9-12).
Kutokumjua Mungu
unayemtumikia kuna hatari kubwa sana; kwanza hutomwabudu katika roho na kweli,
hutomuamini kwa kiwango kinachotakiwa. Pili utayumbishwa na imani zinazoibuka
kila leo. Na tatu, unaweza kuabudu miungu na siyo Mungu pasipo wewe kujua.
Chukua hatua ya kuamua kumjua Mungu ipasavyo.
(b). Mungu naye akujue
Kuna aina tatu za watu
Mungu anaowajua, jichunguze wewe Mungu anakujua kwa aina ipi? Kisha rekebesha
ikistahili.
Moja; ni wale watu
ambao Mungu anawajua kwa uovu wao uliofika katika kiti chake cha enzi, watu
ambao Mungu amewageuzia kisogo asiuone uovu wao (Ufunuo 3:1)
Pili; ni wale watu
ambao Mungu anawajua kwa kuchanganya mambo, leo wameokoka kesho hawajaoko,
keshokutwa wamerudi, mtondogoo wameanguka tena (Ufunuo 3:15). Watu hawa
wanakiri kumpenda Mungu lakini wanatenda mapenzi ya shetani.
Tatu; ni wale watu
ambao Mungu anawajua kwa matendo mema, wanampendeza Mungu kwa kutii na kutenda
amri na sheria zake (Ufunuo 2:19).
(c). kumjulisha Mungu
kwa wengine
Kumjulisha Mungu na
Yesu Kristo kwa wengine ni jambo la lazima mara tu baada ya kuchukua uwamuzi wa
kuokoka. Kumwambia mwengine siri ya mafanikio ni uwamuzi wako, ukipenda
utamwambia na usipopenda hutamwambia. Lakini kumjulisha Mungu na Yesu Kristo
kwa wengine ni lazima na siyo uamuzi wako, kwa sababu ni agizo la Yesu Kristo
mwenyewe (Marko 16:15).
Kuna njia nyingi za
kumjulisha Mungu kwa wengine; kuhubiri, kufundisha, kuimba. Unaweza kuitumia
njia moja wapo katika hizo ili mradi injili ya Mungu isonge mbele. Cha muhimu
hapa, ni kutengeneza matendo yako kwanza, kwa sababu matendo yana nguvu katika
kuhubiri kuliko kelele za mwaka mzima. Na kumuhubiri Mungu na Yesu Kristo ni
jambo endelevu, halina ukomo au likizo (Yohana 17:26a).
Mungu aishiye milele, Yehova na akubariki sana kwa kushiriki sehemu hii ya somo hili, kwa Jina la Yesu Kristo. Amina.
No comments:
Post a Comment