Bwana Yesu asifiwe!
Somo letu la leo ni lenye kichwa “NDIPO UJITUNZE
USIJE UKAMSAHAU BWANA MUNGU WAKO”, hapo unaweza ukajiuliza ujitunze nini? Au
ujitunzaje?
Cha kujitunza hapa ni moyo wako, kwa sababu tabia ya
moyo wa mwanadamu ni kupata kile unachokihitaji kwa njia yoyote na gharama
yoyote isipokuwa kitu hicho kiwe ni dhambi kwa Mkristo, lakini wapo Wakristo
ambao wametimiza haja za mioyo yao ambazo ni chukizo mbele za Bwana.
Sasa baada ya kutimiza matamanio ya moyo, iwe kwa
njia halali au isiyo halali, moyo hurizika. Baada ya moyo kuridhika mwanadamu
husahau vyote nje na riziki ya moyo wake. Hiyo ndiyo tabia ya moyo.
Tuangalie neno la Mungu linavyosema;
Kumbukumbu la Torati 6:10-13. Tena itakuwa atakapokwisha
Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na
Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na
nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa
usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe
utakula na kushiba; ndipo ujitunze usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya
Misri, nyumba ya utumwa. Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na
kuapa kwa jina lake.
Moyo wa mwanadamu siku zote unawaza mafanikio ya
mwili, kumiliki majumba, mashamba, magari, wanyama n.k na kwa juhudi zote
mwanadamu huyu atahakikisha anatimiza matamanio ya moyo wake. Katika kipindi
cha kutafuta, mwanadamu huyu hujitoa moyo wake wote kumpenda Bwana, Mungu wake
na mchana na usiku humlilia Mungu ambariki.
Inapotokea mwanadamu huyu amefanikiwa, moyo wake
hurizika na kumsahau Mungu aliye chanzo cha baraka na mafanikio yake (Zaburi
24:1, 1 Wakorintho 10:26). Na hii ndiyo imekuwa sababu, kuna watu wamelia na
kuomba baraka za mwili na mafanikio lakini wamekosa, Mungu anajua siku
atakapokufanikisha, moyo wako utamsahau Mungu.
Siyo kwamba Mungu anatufundisha kutotafuta mali, la
hasha, Mungu anatuonya kuwa tupatapo mali au utajiri, mioyo yetu isimsahau
Mungu na kujaza mali katika nafasi ya Mungu. Yaani Mungu asiwe “substituted” na
mali au utajiri ulionao.
Luka 12:16-19. Akawaambia mithali, kuwa shamba la
mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akasema,
nifanyaje? maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, nitafanya hivi,
nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka
yangu yote na vitu vyangu. Kisha
nitajiambia ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka
mingi; pumzika basi, ule, unywe na ufurahi.
Hapa tunapata somo kupitia huyu tajiri,
alipofanikiwa alijiambia moyo wake kuwa atajenga ghala kubwa ya kuweka akiba
vitu vyake vizuri, na akajiambia tena, ee nafsi yangu kula, unywe na ufulahi.
Hapa tunatambua moja kwa moja kuwa tajiri huyu alilidhika nafsini mwake hata
akamsahau Mungu.
Kwanini nasema alimsahau Mungu; hakusema neno lolote la
kumshukuru Mungu, nafasi ya Mungu moyoni mwake sasa ilikuwa imejaa utajiri na
mali aliyonayo.
Vivyo hivyo na wanadamu wa siku hizi, wakipata mali,
mioyo yao inamsahau Mungu na wanaanza kuitumikia mali waliyonayo (Torati
6:14-15). Mungu anasema utapofanikiwa, usisahau kumtumikia Mungu, Bwana wako. Unaweza ukasema mbona bado nampenda Mungu na ninamtumikia pia, ngoja nikwambie,
amri kuu ya Mungu inasema umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa
akili zako zote na kwa nguvu zako zote.
Sasa wewe unampenda Mungu, Bwana wako kwa akili yako
na nguvu zako, lakini moyo wako unapenda na kuitumikia mali uliyonayo.
Hujatimiza amri kuu ya Mungu bado. Kwa sababu umejiinulia mungu mwingine mbali
na huyo Mungu unayedai unamwabudu. Mungu, Bwana wetu alishatuonya kuwa hatuwezi
kutumikia mabwana wawili, hatuwezi kumpenda Mungu na mali (Luka 16:13, Mathayo
6:24).
Kama kwa akili zetu na nguvu zetu tunampenda na kumtumikia Mungu, lakini
mioyo yetu inapenda na kutumikia mali tulizonazo, hatutendi kitu bado.
Kupitia mali zako unatakiwa umtumikie Mungu,
ukiunganisha na akili na nguvu zako unakuwa kweli umempenda Mungu. Kwa sababu
mali hukaa moyoni, ukiweza kumtumikia Mungu kwa mali zako na kumpenda Mungu kwa
moyo wako, hapo unakuwa umetimiza amri kuu ya kwanza ya Mungu (Mathayo
22:37-38). Usimtoe Mungu ndani ya moyo wako na kuweka mali na utajiri ulionao,
ukifanya hivyo hutoweza kuikwepa hasira ya Bwana, Mungu wako (Kumbukumbu la
Torati 6:15).
Na kama umeamua kumtumikia Mungu kwa mali zako,
usifanye kwa mashindano ili uonekane na watu na kupata sifa machoni mwao (Luka
18:9-14), hiyo ni habari ya Farisayo na mtoza ushuru waliokwenda hekaluni
kuomba, maombi ya huyu Farisayo yanatuonesha kila alilofanya alifanya ilia pate
sifa machoni mwa wanadamu na alifanya kwa mashindano (Filipi 2:3).
Unapomtumikia Mungu kwa mali zako, usito masalio ya
mali/fedha yako au wanyama walemavu katika kundi la wanyama wako na kupeleka
madhabahuni mwa Bwana, Mungu wako kwani hapendezwi na dhabihu ya aina hiyo
(Mambo ya Walawi 22:21, Marko 12:41-44).
Kama ulikuwa ukiishi maisha ya aina hii; ulimtoa
Mungu moyoni mwako na kujaza mali na fedha ulizonazo, ulimtumikia Mungu kwa
mali na fedha zako ili uonekane na watu au ulimtolea Mungu masalio au ziada tu
katika mali yako na fedh yako na labda ulitoa wanyama wenye ulemavu na magonjwa
katika madhabahu ya Bwana, Mungu wako, leo hii Mungu anataka kutengeneza na
wewe, nafasi ipo na neema ya Mungu yatosha, amua sasa kubadilika.
Na ikiwa upo kwenye mchakato na hatua za kuelekea
mafanikio, usumsahau Bwana, Mungu wako. Usiache nafasi ya Mungu moyoni mwako
ijazwe na mali utakayo ipata, ndipo mali yako itakuwa ni ya kudumu.
“Share somo hili kwa marafiki zako, na Mungu wa
mbinguni akubariki sana”.