Friday, June 14, 2013

NDIPO UJITUNZE USIJE UKAMSAHAU BWANA MUNGU WAKO.



Bwana Yesu asifiwe!

Somo letu la leo ni lenye kichwa “NDIPO UJITUNZE USIJE UKAMSAHAU BWANA MUNGU WAKO”, hapo unaweza ukajiuliza ujitunze nini? Au ujitunzaje?

Cha kujitunza hapa ni moyo wako, kwa sababu tabia ya moyo wa mwanadamu ni kupata kile unachokihitaji kwa njia yoyote na gharama yoyote isipokuwa kitu hicho kiwe ni dhambi kwa Mkristo, lakini wapo Wakristo ambao wametimiza haja za mioyo yao ambazo ni chukizo mbele za Bwana.

Sasa baada ya kutimiza matamanio ya moyo, iwe kwa njia halali au isiyo halali, moyo hurizika. Baada ya moyo kuridhika mwanadamu husahau vyote nje na riziki ya moyo wake. Hiyo ndiyo tabia ya moyo.

Tuangalie neno la Mungu linavyosema;
Kumbukumbu la Torati 6:10-13. Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.

Moyo wa mwanadamu siku zote unawaza mafanikio ya mwili, kumiliki majumba, mashamba, magari, wanyama n.k na kwa juhudi zote mwanadamu huyu atahakikisha anatimiza matamanio ya moyo wake. Katika kipindi cha kutafuta, mwanadamu huyu hujitoa moyo wake wote kumpenda Bwana, Mungu wake na mchana na usiku humlilia Mungu ambariki. 

Inapotokea mwanadamu huyu amefanikiwa, moyo wake hurizika na kumsahau Mungu aliye chanzo cha baraka na mafanikio yake (Zaburi 24:1, 1 Wakorintho 10:26). Na hii ndiyo imekuwa sababu, kuna watu wamelia na kuomba baraka za mwili na mafanikio lakini wamekosa, Mungu anajua siku atakapokufanikisha, moyo wako utamsahau Mungu.

Siyo kwamba Mungu anatufundisha kutotafuta mali, la hasha, Mungu anatuonya kuwa tupatapo mali au utajiri, mioyo yetu isimsahau Mungu na kujaza mali katika nafasi ya Mungu. Yaani Mungu asiwe “substituted” na mali au utajiri ulionao. 

Luka 12:16-19. Akawaambia mithali, kuwa shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akasema, nifanyaje? maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, nitafanya hivi, nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.  Kisha nitajiambia ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe na ufurahi.

Hapa tunapata somo kupitia huyu tajiri, alipofanikiwa alijiambia moyo wake kuwa atajenga ghala kubwa ya kuweka akiba vitu vyake vizuri, na akajiambia tena, ee nafsi yangu kula, unywe na ufulahi. Hapa tunatambua moja kwa moja kuwa tajiri huyu alilidhika nafsini mwake hata akamsahau Mungu. 

Kwanini nasema alimsahau Mungu; hakusema neno lolote la kumshukuru Mungu, nafasi ya Mungu moyoni mwake sasa ilikuwa imejaa utajiri na mali aliyonayo.

Vivyo hivyo na wanadamu wa siku hizi, wakipata mali, mioyo yao inamsahau Mungu na wanaanza kuitumikia mali waliyonayo (Torati 6:14-15). Mungu anasema utapofanikiwa, usisahau kumtumikia Mungu, Bwana wako. Unaweza ukasema mbona bado nampenda Mungu na ninamtumikia pia, ngoja nikwambie, amri kuu ya Mungu inasema umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote.

Sasa wewe unampenda Mungu, Bwana wako kwa akili yako na nguvu zako, lakini moyo wako unapenda na kuitumikia mali uliyonayo. Hujatimiza amri kuu ya Mungu bado. Kwa sababu umejiinulia mungu mwingine mbali na huyo Mungu unayedai unamwabudu. Mungu, Bwana wetu alishatuonya kuwa hatuwezi kutumikia mabwana wawili, hatuwezi kumpenda Mungu na mali (Luka 16:13, Mathayo 6:24). 

Kama kwa akili zetu na nguvu zetu tunampenda na kumtumikia Mungu, lakini mioyo yetu inapenda na kutumikia mali tulizonazo, hatutendi kitu bado.

Kupitia mali zako unatakiwa umtumikie Mungu, ukiunganisha na akili na nguvu zako unakuwa kweli umempenda Mungu. Kwa sababu mali hukaa moyoni, ukiweza kumtumikia Mungu kwa mali zako na kumpenda Mungu kwa moyo wako, hapo unakuwa umetimiza amri kuu ya kwanza ya Mungu (Mathayo 22:37-38). Usimtoe Mungu ndani ya moyo wako na kuweka mali na utajiri ulionao, ukifanya hivyo hutoweza kuikwepa hasira ya Bwana, Mungu wako (Kumbukumbu la Torati 6:15).

Na kama umeamua kumtumikia Mungu kwa mali zako, usifanye kwa mashindano ili uonekane na watu na kupata sifa machoni mwao (Luka 18:9-14), hiyo ni habari ya Farisayo na mtoza ushuru waliokwenda hekaluni kuomba, maombi ya huyu Farisayo yanatuonesha kila alilofanya alifanya ilia pate sifa machoni mwa wanadamu na alifanya kwa mashindano (Filipi 2:3).                                                   
Unapomtumikia Mungu kwa mali zako, usito masalio ya mali/fedha yako au wanyama walemavu katika kundi la wanyama wako na kupeleka madhabahuni mwa Bwana, Mungu wako kwani hapendezwi na dhabihu ya aina hiyo (Mambo ya Walawi 22:21, Marko 12:41-44).

Kama ulikuwa ukiishi maisha ya aina hii; ulimtoa Mungu moyoni mwako na kujaza mali na fedha ulizonazo, ulimtumikia Mungu kwa mali na fedha zako ili uonekane na watu au ulimtolea Mungu masalio au ziada tu katika mali yako na fedh yako na labda ulitoa wanyama wenye ulemavu na magonjwa katika madhabahu ya Bwana, Mungu wako, leo hii Mungu anataka kutengeneza na wewe, nafasi ipo na neema ya Mungu yatosha, amua sasa kubadilika.

Na ikiwa upo kwenye mchakato na hatua za kuelekea mafanikio, usumsahau Bwana, Mungu wako. Usiache nafasi ya Mungu moyoni mwako ijazwe na mali utakayo ipata, ndipo mali yako itakuwa ni ya kudumu.

“Share somo hili kwa marafiki zako, na Mungu wa mbinguni akubariki sana”.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts