Kutoa sadaka
kama mazoea au desturi ni kupoteza fedha au mali yako pasipo na manufaa yoyote.
Wapo wakristo ambao wamelelewa katika familia za dini na kukua wakijua ni
lazima kwenda na sadaka ibadani lakini hawajui umuhimu na matunda wanayoweza
kuyapata kwa kutoa sadaka. Wakristo wa namna hii ni kama watoto ambao wanapewa
sadaka na wazazi wao, wakitoa au wasipotoa sadaka hiyo hawaoni mapungufu yoyote,
zaidi ni faida kwao kwani watakula barafu.
Na wapo wakristo wanaotoa sadaka kama ajali, wao
huamua ni sadaka ya aina au kiasi gani watatoa muda mfupi baada ya kujianda
kwenda ibadani au hata wakiwa njiani kuelekea ibadani. Wanatoa sadaka za kushtukiza,
sadaka isiyo na maandalio yoyote.
Sadaka inapaswa kuandaliwa, hata siku moja kabla ya
kutolewa. Katika agano la kale utaona kuna siku zinapita tangu Mungu aombe
kutolewa kwa sadaka na siku ya kuitoa hiyo sadaka, aliyeambiwa atoe sadaka
anafanya maandalizi ya kuchagua sadaka nzuri ya kupendeza itakayopata kibali
machoni pa Mungu.
Sadaka utakayoitoa madhabahuni pa Mungu lazima
uitamkie jambo. Kabla sijatoa sadaka yangu huwa namwambia Mungu hivi; “maadam,
sadaka/dhabihu hii itafanya kazi shambani mwako ee Mungu wangu, fanya jambo
(ninalitaja) katika maisha yangu”.
Sadaka au dhabihu ni sawa na mbegu, ukipanda mbegu
unategemea uzune kulingana na mbegu uliyoipanda. Sadaka au dhabihu ni mbegu ya
kuvunia baraka zote za kiroho na kimwili, afya na uzima.
Zaburi 50:5 “Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu (sadaka)”.
Agano ni makubaliano yasiyovunjika, kufanya agano na
Mungu ni kujithibitishia makubaliano yako na Mungu kuwa yatatimia. Sasa unaweza
ukafanya agano na Mungu kwa kutumia dhabihu au sadaka unayoitoa katika ibada
zako, sadaka iliyoandaliwa na siyo sadaka ya kutolewa kama bahati mbaya. Agano hilo
utalifanya pale utakapo itamkia neno sadaka unayoipeleka madhabahuni pa Mungu
wako, ukitoa sadaka ambayo hukuitamkia neno utakuwa unatoa sadaka kama mtoto
asiyejua nini maana ya sadaka na inatolewa kwa sababu gani.