Thursday, May 24, 2018

NGUVU YA MWANAMKE AOMBAYE


Nakusalimu mpendwa katika Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo

Utangulizi
Siku ya leo, Mungu anatufundisha somo lenye kichwa, “Nguvu ya mwanamke aombaye”. Ni maombi yangu Mungu afungue ufahamu na uelewa wako ili tunapokwenda kumaliza somo letu la leo, kuwe kuna kitu kipya kimejengeka na kuimarika katika fahamu zetu. Kitu ambacho hakitatuacha kubaki kama tulivyokuwa mwanzo, wote wanaume kwa wanawake. Wanaume tutajifunza nguvu walizonazo wanawake katika ulimwengu wa kiroho na namna Mungu anavyothamini, sikiliza na kujibu maombi yao. Wanawake watajifunza nguvu waliyonayo ndani ya Yesu Kristo, kupitia nguvu hiyo watavikwa utu mpya wa kujithamini na kufanya mambo makubwa katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa macho ya damu na nyama. 

Jamii karibu zote ulimwenguni zimemchukulia mwanamke kama kiumbe duni na dhaifu, kiumbe kinachostahili kutendewa ubaya wowote. Na hivyo ndivyo mwanamke alivyoaminishwa kuwa na kujichukulia. Katika kujikomboa kutoka dhana nzima ya mfumo dume, mwanamke anafanya kampeni za kutafuta haki sawa na mwanaume. Kutafuta haki sawa kati ya mwanamke na mwanaume siyo suluhu sahihi ya kumkwamua mwanamke. Suluhu sahihi ni mwanamke kuitambua nafasi yake mbele za Mungu na namna Mungu alivyomthamini mwanamke tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Pili, mwanamke kutambua wajibu wake sahihi kwa mwanaume. Tatu, mwanaume atambue nafasi ya mwanamke katika kumuimarisha maisha yake ya kiroho, kijamii na kiuchumi. 

Mwanamke ni nani?
“Bwana analitoa neno lake (na kusema), wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa”, Zaburi 68:11. Kwa mujibu wa Biblia takatifu, kutangaza habari ni kulihuburi neno la Mungu au Yesu Kristo. Habari njema za Yesu Kristo zinatangazwa mahali kote, sehemu yoyote na wakati wowote. Asilimia kubwa ya wanawake, asiyeko na aliyeko ndani ya ndoa ni mtangaza habari njema za Mungu na Yesu Kristo, wengine pasipo hata wao wenyewe kujua. Ndiyo, unaweza kuwa unatangaza habari njema za Mungu na Yesu Kristo pasipo kujijua. Twende pamoja sasa kumtambua mwanamke ni nani kupitia 4M; msaidizi, mzazi, mlezi na mlinzi. Kupitia 4M utatatmbua namna mwanamke anavyoweza kutangaza habari njema za ufalme wa Mungu. 

Msaidizi
Mwanzo 2:20b na 18, “…..lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye”. Mwanamke ni msaidizi wa mwanaume, siyo msaidizi tu, ni msaidizi wa kufanana na mwanaume. Kufanana maana yake ni kuwa na viwango vinavyokaribiana katika ubora na nafasi. Fundi ujenzi wa nyumba hawezi kutafuta msaidizi mwenye ujuzi wa kutengeneza magari, ni lazima atatafuta msaidizi mwenye uwezo wa ujenzi wa nyumba. Hivyo basi mwanamke ni sawa na mwanaume mbele za macho ya Mungu. Hakuna aliye bora zaidi ya mwingine, si mwanume wala si mwanamke. Mbele za macho ya Mungu, sote tuna nafasi sawa. Mwanamke jithaminishe sawa na mwanaume, ndivyo Mungu anavyotuona. Mwanaume mthamini mwanamke kwa maana ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26). Ukimuona mwanamke, ona utukufu wa uumbaji wa Mungu sawa na ule unaouona kwako. Siku zote za maisha yako mwanamke fanya majukumu yako kwa mwanaume ukimpendeza Mungu, hii ndiyo injili sahihi ikupasayo kuliko hata ile ya madhabahuni ilihali hautimizi wajibu wako kwa mumeo impendezavyo Mungu. 


Mzazi
Hakuna mwanaume yoyote, awe mwanadamu au awe mnyama mume mwenye kuweza kuendeleza kizazi chake pasipo nafasi ya mwanamke. Sayansi na teknolojia imekuwa kiasi kwamba kuna uwezekano wa kutungisha mimba pasipo kukutana kwa mwanaume na mwanamke, lakini ni lazima mimba hiyo ikiishakutunga, atahitajika mwanamke wa kubeba mimba hiyo. Dunia itaendelea kisayansi na kiteknolojia, kamwe haitaweza kuchukua nafasi ya mwanamke ya kubeba mimba. Na endapo itakuwa, mtoto atakayezaliwa lazima awe na mapungufu yatakomfanya asiishi maisha marefu. Hivyo basi kila mwanaume anayehitaji kuendeleza uzao wake ni lazima awe na ushirika wa ndoa na mwanamke. Kuzaa siyo tu kuendeleza kizazi, bali ni baraka ambayo Mungu alitubariki wanadamu ili kushiriki uumbaji pamoja naye (Mwanzo 1:28). Jinsi vile mwanaume ana nafasi katika kushiriki uumbaji na Mungu, vivyo hivyo mwanamke ana nafasi sawa. Nadhani zaidi, kwa sababu mwanamke anapata masumbufu yote ya kulea mimba na uchungu wa kujifungua. Kushiriki uumbaji wa Mungu (kupitia uzazi) ni sawa na kuitangaza injili kupitia malezi bora ya uzao wa mwanamke husika. 

Mlezi
Mwanamke ndio nguzo kuu ya malezi ya familia. Watoto wakiwa na tabia mbaya, lawama zinabebwa na mwanamke na watoto wakiwa na tabia njema pongezi apewe mwanamke. Mjumuisho wa familia moja na familia nyingine huzaa jamii. Malezi bora ya mwanamke kwa watoto wake ni kujenga familia bora yenye kufuata maadili mema ya Mungu. Ili kuwa na jamii yenye kufuata maadili, ni lazima mwanamke ashiriki ipasavyo katika kutimiza jukumu lake hili muhimu la malezi bora. Ingawa, wanaume nao hushiriki katika malezi ya familia na jamii, mchango wao hauwezi kamwe kulinganishwa na mchango wa mwanamke. Kwa sababu, mume kwa mke ni sawa na mtoto pia. Ndiyo sababu kuna usemi unaosema, “mwanaume akioa hupata mama wa pili wakati mwanamke akipata mume hupata mtoto wa kwanza”. Kuna wanaume walishindikana kwa kuwa na mienendo mibaya, lakini walipokutana na mlezi mwema (mke) wakabadili tabia kumuelekea Mungu (1 Petro 3:1). Hii ni injili njema iliyotangazwa na mwanamke kwa mume wake. 

Mlinzi
“Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani: mwanamke atamlinda mwanaume”, Yeremia 31:22. Ulinzi unaozungumziwa hapa siyo ulinzi wa kimwili kama askari wakaao lindo masaa ya usiku. Ni ulinzi wa kiroho cha mwanaume katika ukuaji na ustawi wa kumjua Mungu. Pia ni ulinzi wa familia na watoto kwa ujumla katika uchaji wa Mungu. Ee mwanamke simama imara kuomba nafasi ya Mungu katika ndoa yako na watoto wako. Kuna mambo maovu yanafanywa na wanaume au watoto kwa sababu wanawake hawajatambua nafasi na nguvu zao endapo watashuka magotini na kumuomba Mungu ipasavyo. Mwanamke ni mlinzi wa maisha ya kiroho ya mume wake na watoto wake. Usilalamike kwa jambo lolote, ingia magotini mwa Mungu, mambo yatakuwa safi. 

Mwanamke anapotimiza nafasi zake zilizotajwa hapo juu, anachukua nafasi kamili ya kuihubiri habari njema ya Mungu na Yesu Kristo. Haihitaji mkusanyiko wa watu kuanzia 100 hadi 1000 ili tuseme mwanamke anatangaza habari njema. Kwa namna na mwenendo mwema wa maisha yake unaompendeza mume na kuwafundisha njia njema watoto wake ili kujenga familia bora yenye maadili mema, hutangaza habari njema za Mungu (1 Petro 3:1). Kwa hiyo mwanamke ni jeshi kubwa mbele za Mungu. Hii ni haki ambayo wanawake wengi wanaipata kwa kule tu kulea familia zao katika mwenendo wa kumpendeza Mungu. Lakini ipo nguvu zaidi wanayovikwa wanawake wanaodumu katika kumuomba Mungu. Kuitambua nguvu ya mwanamke  aombaye au anayedumu katika sala na maombi mbele za Mungu, twende tufuatane nami sasa. 

Nguvu ya mwanamke aombaye kwa bidii
Maombi ya mwanamke yana ushawishi mkubwa sana mbele za Mungu kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa kumimina moyo na kueleza hoja mbele za Mungu tofauti na mwanaume. Mwanamke anjua kushuka, kububujika na kupondeka moyo aelezapo hoja zake mbele za Mungu. Pia, mwanamke ana maombi ya kusukuma, haachi kuomba hadi apokee majibu “persistent praying”. Kwa sababu hiyo maombi ya mwanamke yanapata kibari na majibu mbele za Mungu kwa urahisi zaidi endapo ataomba katika roho na kweli akizingatia misingi na namna ya maombi. Soma masomo yaliyopita; sehemu ya kwanza, pili na tatu ili kujifunza zaidi kwa habari ya maombi yenye nguvu na kibali mbele za Mungu. Tuangalie mambo makubwa yaliyofanywa na wanawake kupitia maombi ambayo wanaume hawakuthubutu kuyafanya.

Kupenya ngome ya kifalme (nguvu ya utawala)
Hamani alipata kukubalika ndani ya moyo wa mfalme Ahasuero kiasi kwamba mfamle alimpandisha cheo na kumfanya nafasi ya pili mara baada ya mfalme. Hamani akaanda waraka aliougonga muhuri wa mfalme akiagiza Wayahudi wote kuuawa. Mordekai mlezi wa malkia Esta na mkwe wa mfalme alipopata habari alilia na kuomboleza (maombi kwa Mungu) akiwa amevaa magunia na kujipaka majivu mwilini. Hakuna jambo lililobadilika hadi pale malkia Esta alipoingia katika maombi. Biblia inasema malkia Esta alipata kibali mbele za mfalme kinyume na utaratibu, ilipaswa Esta auawe kwa kuingilia mlango wa nyuma. Nguvu ya maombi aliyoyatanguliza kabla hajaingia malangoni mwa mfalme na kibali cha Mungu vilimvika kibali malkia mbele za mfalme ambaye baadaye aliagiza rafiki yake na kiongozi wake wa juu Hamani auawe. Laiti kama mkwe wa mfalme, Mordekai angeomba na kwenda mbele za mfalme asingepata kibali kama alivyopata malkia Esta. Unadhani ni kwa nini malkia Esta hakutumia nafasi yake ya umalkia kwenda mbele za mfalme? Kwa sababu asingepata kibali cha kusikilizwa na angepaswa kuuawa. Malkia hakupata kibali kwa sababu ya nafasi yake moyoni mwa mfalme, bali kwa sababu ya nguvu ya maombi aliyoomba kabla hajkwenda mbele za mfalme. Soma Biblia takatifu kitabu cha Esta. 

Mwanamke anapodumu katika maombi kwa nia ya dhati mbele za Mungu, anapata kibali kinachoweza kubadili mfumo wowote wa utawala na kuwa vile atakavyo kwa utukufu wa Mungu. Hata ndani ya ndoa au familia, mwanamke ana nguvu kubwa ya kuitiisha (kuiadabisha, kuimaadilisha) ndoa na familia yake kama tu ataamua kudumu magotini akiomba kwa Mungu. Mwanamke akisimama imara kumwabudu Mungu, ndoa yake, familia yake na nyumba yake kwa ujumla itasimama pamoja naye kumwabudu Mungu. 

Nguvu ya kufunga na kufungua
Palikuwa na mtu ajulikanaye kama Elkana, mwenye wake wawili, Penina na Hana. Penina alimzalia Elkana watoto waume na wake lakini Hana alikuwa mgumba asiweze kumzalia watoto mumewe Elkana. Maonezi na masimango ya Penina kwa Hana kwa sababu ya ugumba wake yalimpa Hana uchungu uliompa nguvu ya kumwendea Mungu kwa maombi. Lazima Elkana na mkewe Hana pamoja na kuhani wa hekalu la Mungu, Eli, walimuomba Mungu kwa habari ya Hana kutopata watoto na ndipo walipopata majibu ya kuwa Hana ni mgumba. Na wakaishi maisha yao yote wakijua na kuamini kuwa Hana ni mgumba hataweza kupata watoto. Uchungu wa mateso ya mke mwenza ulipoujaa moyo wa Hana, akaamua wenda mbele za Mungu kumimina moyo wake uliopondeka na kueleza hoja za ombi la moyo wake. Biblia inasema pale pale, Mungu akalifungua tumbo la Hana na kumpatia mtoto wa kiume, aliyemuita Samweli. Soma Biblia, kitabu cha Samweli sura ya 1 na 2. 

Jambo lolote gumu, kifungo chochote cha kiroho na hata mwili, mwanamke anapoamua kupiga goti na kumuomba Mungu kwa kuumimina moyo wake mbele za Bwana, Mungu huachilia kibali cha kufunga au kufungua. Maombi ya kufunga na kufungua, soma Mathayo 18:18, aina hii ya maombi ndiyo maombi aliyoomba Hana. Aliomba kufunguliwa tumbo (alivunja nguvu ya ugumba tumboni mwake), aliomba kufunguliwa uzazi apate watoto wake mwenyewe. 

Nguvu ya kufanya amani
Nabali alikuwa mtu mashuuri wakati wake, mwenye mali nyingi, mtu huyu alimuoa mwanamke aitwaye Abigaili, mwanamke mwenye hekima na busara. Wajakazi wa Nabali walipokuwa nyikani wakichunga kondoo na mbuzi wa bwana wao, wajakazi wa Daudi (aliyeapishwa kuwa mfalme) waliwalinda wasipatwe na mabaya. Ilipokuwa Daudi na watu wake wametindikiwa (wamepungukiwa chakula), wakamwendea Nabali ili wapate msaada kwake. Nabali akawatukana wajumbe waliotumwa na Daudi na kuamsha hasira ya Daudi hata akanuia kumtenda ubaya Nabali. Daudi alipokuwa njiani kwenda kufanya vita na Nabali, tazama, mkewe Nabali, Abigaili akawahi kumlaki Daudi ili kufanya naye amani. Biblia inasema, Abigaili aliwaambia vijana wake, “tangulieni mimi nakuja nyuma yenu”, 1 Samweli 25:19. Japo Biblia haiweki wazi kwa nini Abigaili aliwatanguliza vijana wake asiende pamoja nao, ni dhahiri Abigaili aliwatanguliza vijana wake ili apate nafasi ya kumuomba Mungu ampe kibali cha kufanya mazungumzo ya amani na Daudi. Abigaili alipokutana na Daudi walizungumza na kufanya amani iliyoepusha kumwaga damu alikodhamiria Daudi. Soma Biblia kitabu cha 1 Samweli sura ya 25. 

Hili lipo wazi hata katika jamii zetu, unakuta mwanaume ana majivuno, mkorofi, asiyependa amani na majirani zake lakini mke wake ndiye nguzo na kiungo kikubwa cha familia na jamii. Kunapotokea mafarakano yoyote ndani ya familia au jamii, mwanamke akichukua nafasi ya kuomba kwa dhati ili amani ipatikane, ni hakika hakuna nguvu itakayosimama kinyume na maombi hayo. 

Ufunguo wa kibali cha maombi ya mwanaume kwa Mungu
Inaajabisha? Unaweza usiamini, lakini hii ni kweli asilimia 100. Mwanamke ni ufunguo wa maombi ya mwanaume mbele za Mungu. Hii ni kwa wanaume na wanawake walioopo ndani ya ndoa tu. Kukitokea mafarakano yoyote ndani ya ndoa kati ya mume na mke na wasipofanya suluhu mapema, unakuta mambo ya mwanaume (kibali cha biashara au kazi kinafungwa) yanaanza kwenda ndivyo sivyo. Hii ni kwa sababu nyumba ikiwa na amani, mke anaomba milango ya baraka za Mungu ifunguke ili wapate riziki na maisha bora. Nyumba ikikosa amani, mwanamke ananung’unika mbele za Mungu kwa uchungu, manung’uniko hayo hufunga milango yote ya baraka kwa mwanaume. Na endapo mwanaume huyu ataamua kwenda mbele za Mungu kuomba baraka, katu hapati majibu ya maombi yake hadi atakapofanya amani na mke wake (Wakolosai 3:19).
“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke hishima, kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”, 1 Petro 3:7
Udhaifu wa mwanamke upo moyoni, siyo nguvu za mwili. Moyo wa mwanamke ni rahisi kupata upweke, anaweza kuwa ndani ya ndoa lakini akawa mpweke kwa sababu haoni ukamilifu wa pendo la mumewe. Ndiyo maana Biblia ikamuamuru mume kumpenda mke (Waefeso 5:25). Kwa hiyo, kuishi na mwanamke kama chombo dhaifu, ni kuishi kwa upendo na mwanamke. Ukimpa mke wako upendo wa dhati na ukamuonesha kwa vitendo (umemchukulia kwa akili katika udhaifu wake), hakika atakunjua moyo wake kwako na kukuombea baraka kwa Mungu na hii itafungua milango yote ya mafanikio kwako na majibu ya maombi yako. 

Kwa somo hili fupi, ni imani yangu, mwanamke utakuwa umetambua nafasi yako na nguvu uliyoibeba endapo utaamua kudumu katika maombi mbele za Mungu. Nawe mwanaume utakuwa umetambua nafasi na sehemu ya mwanamke katika baraka na ustawi wako kiroho na kimwili. Baada ya somo hili, ni wajibu wako mwanamke kuomba kwa ajili yako binafsi, mumeo (walio katika ndoa na wanaotegemea kuingia katika ndoa), watoto wako (walio na watoto na wanaotarajia kupata watoto), wazazi wako na taifa kwa ujumla. 

Shiriki baraka ya somo hili pamoja na uwapendao katika Bwana kwa kubonyeza kitufe cha mtandao wa kijamii unaoutumia hapo chini. Baraka za Mungu aliye hai zidumu pamoja nawe kwa jina la Yesu Kristo. Amina.1 comment:

Featured Post

WHO IS JESUS CHRIST?

  Who is Jesus Christ? Jesus Christ is God who wore man’s flesh purposely to die on the cross for compensating humans’ sins ...

Popular Posts