YESU KRISTO ASIFIWE!
Ashukuriwe Mungu aliyetupa kibali cha mimi na wewe msomaji
wangu kukutana leo ikiwa ni kwa mara ya kwanza au kwa mara nyingine tena. Leo
tuna somo lenye kichwa kisemacho “UNAWEZA KUWA UNATEMBEA CHINI YA
LAANA PASIPO WEWE MWENYEWE KUJUA”, katika somo hili tutaangalia kwa undani
mambo yafuatayo:-
- Maana ya laana.
- Laana inaletwa/sababishwa na nani?
- Kwa nini ulaaniwe?
- Je, unaweza kuwa umelaaniwa pasipo wewe kujua?
- Ni vitu gani vinaweza kulaaniwa?
- Kuvunja laana na mikosi, kuomba baraka za Mungu (Yehova).
Hili ni somo zuri sana ambalo ukilifuatilia kwa ukaribu
zaidi na ukijenga imani kwa Mungu kuna vitu (laana), Mungu anakwenda kuzivunja,
kuzifuta na kuziharibu (1 Yohana 3:8) na kuyabadilisha maisha yako kabisa.
Unakwenda kuishi maisha ya baraka na ushindi, nakuhakikishia lazima
utazishuhudia baraka za Mungu katika maisha yako baada ya kumaliza somo hili.
Maana ya laana.
Laana ni bahati mbaya au maneno mabaya ya maapizo
yanayotamkwa kumuelekea mtu fulani yeye mwenyewe au kitu fulani kinachomuhusu,
kwa mfano; kazi, shamba, watoto, masomo n.k kwa makusudi ya kumdhuru mtu huyo
au kitu kinachomuhusu. Kwa kifupi laana ni kinyume cha baraka.
Laana inaweza ikasababishwa kwa makusudi maalumu (mfano: laana
ambayo ni matokeo ya dhambi za wanadamu) au pasipo kujua (mfano: laana ya
kujitamkia sisi wenyewe), kwa njia zote hizi mbili laana inafanya kazi iwe kwa
makusudi au pasipo kujua.
Laana, ili itende kazi ni lazima iwe imeunganishwa na nguvu
fulani zisizo za kawaida, nguvu za ziada “supernatural powers”, nguvu hizo ni lazima ziwe zinazidi nguvu za
mtu au kitu kinacholaaniwa. Nachomaanisha hapa ni kwamba, mdogo hawezi kumlaani
mkubwa; shetani hawezi kumlaani Mungu, na mtu aliyesimama katika kweli na haki
ya Mungu hawezi kulaaniwa na shetani kutokana na ile nguvu ya Mungu iliyomo
ndani yake.
Kwa maana hiyo, kwa maneno yetu wenyewe au ya watu wa karibu
nasi na matendo ya maisha yetu ndiyo sababu kubwa ya laana katika maisha yetu
na vizazi vyetu vijavyo. Kwa sababu kila tunachokitamka na tunachokitenda
kinafuatiliwa kutimilizwa na falme mbili tofauti; ufalme wa Mungu na ufalme wa
shetani. Ni hakika na kweli, ufalme wa shetani hufuatilia hasa mambo ambayo ni hasi kuyatimiliza katika maisha yetu,
kuwa mwangalifu sana.
Mwanzo 2:16-17. Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu (Adamu),
akisema, matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa
ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo
utakufa hakika.
Nataka nikuoneshe kitu hapo, wakati Mungu anampa maagizo
Adamu kwa habari ya chakula ambacho ni matunda Biblia haisemi kuwa shetani naye
alikuwepo akiyasikiliza maagizo hayo. Lakini kwa hakika shetani alikuwepo japo
Adamu hakumuo na aliyasikia vizuri sana maagizo hayo. Hili tunalithibitisha
kutokana na kitendo chake (shetani) cha kumfuata Hawa na kumwambia habari ile
ile ihusuyo maagizo waliyopewa na Mungu.
Mwanzo 3:1. Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote
wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo
alivyosema Mungu, msile matunda yote ya miti ya bustani?
Nataka ujue yule alikuwa ni shetani aliyevaa umbo la mnyama
nyoka. Na ndipo ujue kuwa kila unachokitenda ama kukizungumza, shetani anakuona
na kukusikia na kama Biblia inavyosema kuwa shetani ni mshitaki wetu (Ufunuo
12:10), ndivyo ilivyo, anafanya kazi mchana na usiku kuhakikisha matendo na maneno
yetu hasi yanatimia na tunapata
mateso. Hiyo ndiyo furaha yake.
Ikiwa tumetamka au tumetamkiwa maneno ya kuyalaani maisha
yetu, ufalme wa giza unatuma mapepo yatkayo kufuatilia mchana na usiku ili
kuhakikisha ile laana iliyotamkwa juu yako inatimia na kukupata.
Na jinsi ufalme wa Mungu unavyotenda kazi kwa habari ya
laana katika maisha yetu, tutaona katika kipengele cha aina za laana.
Laana
inaletwa/sababishwa na nani?.
Laana huweza kusababishwa na:-
Mungu.
Mungu hatusababishi wanadamu laana kama kitu cha furaha kwake, bali ni matokeo
ya dhambi zetu. Tunapomkosea Mungu huamua kuachilia laana katika maisha yetu
kwa makusudi ya kutufanya tumrudie yeye baada ya kutambua tunataabika kwa
sababu tumemuacha Mungu.
Mwanzo 5:29.
Akamwita jina lake Nuhu, akinena, huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na
kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani
Bwana (Mungu).
Kumbukumbu la Torati
28:15. Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako,
usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo
(ukiamua kutenda dhambi), ndipo
zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
Malaki 2:2. Kama
hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni (amri ya Mungu), ili kulitukuza
jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi
nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani
baraka zenu; naam, nimekwisha
kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni.
Shetani.
Huyu jamaa naye huweza kusababisha laana katika maisha yako, kama tulivyoona
hapo juu. Pili, unapoamua kuishi maisha ya dhambi ni kwamba unakuwa umedanganywa
(umesababishiwa laana) na ibilisi ambaye alishalaaniwa kwanza. Tutaona hapo
mbele vitu vinavyoweza kulaaniwa ndipo utaelewa kwa undani zaidi, labda nikupe
mfano, mtu anapokuwa na mateso yaliyotoka kuzimu kama mapepo, huyo anakuwa
chini ya laana ya shetani.
Ufunuo wa Yohana 20:10.
Na yule ibilisi, mwenye kuwadanganya,
akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa
uwongo. Nao watateswa mchana na usiku milele na milele.
2 Petro 2:14.
Wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho
zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana (wana wa shetani, wana wa ufalme wa giza).
Mwanadamu.
Mwanadamu akisimama yeye kama yeye hana nguvu wala uwezo wa kulaani, lakini
anaposimama upande mmoja wapo aidha kwa Mungu au kwa shetani, huweza
kusababisha laana. Kwa sababu akiwa upande wa Mungu akitamka neno zuri au baya
linatokea (Mathayo 21:18-19, 1 Wafalme 17:1 na 18:1), kutokana na ile nguvu ya
Mungu iliyomo ndani yake. Na mwanadamu huyo huyo akisimama upande wa shetani
laana atakayoitamka itatokea, kwa sababu furaha ya shetani ni kuwaona wanadamu
wanapata shida na mateso, lazima atatuma roho chafu (mapepo) ziifuatilie na
kuitimiza laana hiyo kwa mtamkiwa.
Warumi 12:14.
Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala
msilaani (mwanadamu ana uwezo wa kulaani).
Yakobo 3:9. Kwa
huo (ulimi) twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo (ulimi-maneno ya kinywa) twawalaani wanadamu waliofanywa kwa
mfan wa Mungu.
Kwa maana hiyo unaweza kuwa unatembea chini ya laana katika
maisha yako, au vitu fulani katika maisha yako vinaweza vikawa vimelaaniwa
pasipo wewe kujua. Na laana hiyo inaweza ikawa imesababishwa na Mungu, shetani
au mwanadamu kama jinsi tulivyoona hapo juu.
Kwanini ulaaniwe?
Kuna sababu nyingi tu zinazomfanya mtu au kitu kipokee
laana. Sababu hizo ni kama zifuatazo:-
Nianze na mfano kwanza; unakuta mtu anasema,
“sisi ukoo wetu ni maskini tu hata tufanyaje”, “kwa hii kozi niliyosoma sijui
kama nitapata kazi kwa kweli”, “watoto wa mama fulani hawaolewagi”, “mimi
masomo ya sayansi hata nifanyaje siji kufaulu”, hiyo ni baadhi ya misemo
iliyobeba laana ndani yake.
Na hakika lazima kuna nguvu itafuatilia
kuhakikisha inatimiza makusudi yaliyopo ndani ya misemo hiyo. Na mara nyingi
laana ya namna hii, watu wengi tunajitamkia pasipo kujua kuwa tunachokitamka
kitatimia katika maisha yetu. (Warumi 12:14, Yakobo 3:9).
Laana itokanayo na kuwalaani
watumishi wa Mungu waliobarikiwa.
Kubali ukatae, mtu yoyote au kitu chochote
Mungu alichokibariki mwanadamu hawezi kukilaani. Na ikiwa umemlaani au kutamka
maneno mabaya juu ya mbarikiwa yoyote wa Mungu, laana hiyo inafanyika kuwa
baraka kwa uliyemtamkia lakini inakurudia wewe kama laana (Hesabu 23:11 na
Hesabu 24:10).
Hesabu
22:12. Mungu akamwambia Balaamu, usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.
Mwanzo
12:3. Nami nitawabariki wakubarikio, naye
akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.
Mwanzo
27:29b. Atakayekulaani alaaniwe,
na atakayekubariki abarikiwe.
Laana ya wazazi.
Hii unaweza ukaipata kutokana na jinsi
unavyowatendea wazazi wako. Haijarishi wazazi wako ni watu wa namna gani au
wamewahi kukukosea nini, watabaki kuwa wazazi wako na ni lazima uwape hushima
yao (Kutoka 20:12). Kitu chochote kibaya utakachowafanyia au kuwasemea wazazi
wako, Mungu atajilipishia kisasi katika maisha yako au hata uzao wako (Mathayo
15:4).
Mwanzo
9:24-25. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo
alivyomtendea (alimchungulia na kuuona uchi wake). Akasema, na alaaniwe Kanaani; atakuwa mtumwa
kabisa kwa ndugu zake.
Pasipo kujarisha wazazi wako wanatabia
gani, laana yoyote watakayo itamka juu yako au manung’uniko yoyote utakayo
wasababishia yatafanyika kuwa laana itakayo laani maisha yako.
Kumbukumbu
la Torati 27:16. Na alaaniwe
amdharauliye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina.
Laana hii ni tofauti na nyingine, inahitaji
upate kibali cha wazazi pia ili kuifuta katika maisha yako. Ikiwa hadi hapa,
umetambua uko chini ya laana ya wazazi, huna budi kuwataka radhi kwa uliyowahi
kuwakosea.
Laana ya kuwanyanyasa wageni,
yatima na wajane.
Hii ni laana inayowapata watu kwa sababu ya
tamaa ya mali, mara nyingi; anapofariki mume mwenye uwezo kifedha wa mwanamke
fulani au baba mwenye uwezo kifedha wa watoto fulani ndugu wa marehemu wanaanza
kuwanyanyasa mke na watoto wa marehemu kwa ajili ya kuwadhurumu mali na kuwazushia
mambo kibao.
Kwa kosa hilo Mungu hujilipishia kisasi juu
ya yoyote aliyehusika kufanya hivyo pasipo kujali kuwa unaowanyanyasa wanamjua
au hawamjui Mungu, machozi yao ni kiberiti cha kuwasha hasira ya Mungu kwako. Kwani
Mungu amesema yeye ni mume wa wajane na baba wa yatima (Yakobo 1:27, Zaburi
68:5).
Kutoka
22:21-24. Usimwonee mgeni, wala
kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na
mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa
watu hao katika neno lo lote, nao
wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami
nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu
mayatima.
Kumbukumbu
la Torati 27:19. Na alaaniwe
apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima,
na mjane aliyefiliwa nu mumewe. Na
watu wote waseme, Amina.
Laana itokanayo na kula/kuiba fungu la
kumi la Mungu.
Laana hii imewafunika watu wengi sana
makanisani, unakuta mtu anafanya biashara au ni mfanyakazi katika ofisi au
shirika fulani lakini hana maendeleo yoyote, na wengine wanapokea mishahara
mikubwa lakini fedha inapotea katika mazingira yasiyo na maelezo kamili.
Kama wewe ni mmoja wapo, amabaye huoni
mafanikio licha ya fedha nyingi unayoipata, biashara yako haikui licha ya kuwa
unaitangaza sana, tambua unatembea chini ya laana kwa kutotoa fungu la kumi.
Malaki
3:9. Ninyi mmelaaniwa kwa laana;
maana mnaniibia mimi (zaka-fungu la kumi), naam, taifa hili lote.
Laana itokanayo na kutenda dhambi
au kutotii maagizo ya Mungu.
Mwanadamu anapofanya dhambi, hasira ya Mungu
inawaka juu yake, na Mungu anaagiza laana juu ya mwanadamu huyo kwa makusudi ya
kumkumbusha mwanadamu huyo kuwa anatakiwa kurejea kwa Mungu na kuziacha njia
zake mbaya.
Mwanzo
3:17. Akamwambia Adamu, kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala
matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, usiyale (kutotii); ardhi imelaaniwa
kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako.
Kumbukumbu
la Torati 11:26-28. Angalieni, naweka mbele yenu hivi leo baraka na laana;
baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo hivi
leo; na laana ni hapo msiposikiza
maagiza ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa
kuandama miungu mingine msiyoijua.
Laana itokanayo na kumwaga damu.
Watu wengi sana wanatembea na laana hii
pasipo wao wenyewe kujua, kwa kuwaua watu (ili wapate mali na utajiri) au kwa
kutoa mimba maisha yako yanalaaniwa. Ndiyo maana utawakuta wengine wana mali
nyingi lakini hawana amani na wengine wamehangaika kila sehemu kutafuta watoto
lakini hawapati, ni kwa sababu wamesahau damu waliyoimwaga miaka mingi
iliyopita, damu ambayo bado inadai kisasi juu yao, mbele za Mungu.
Mwanzo
4:10-11. Akasema (Mungu), umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basa sasa umelaaniwa wewe katika ardhi,
iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako.
Laana itokanayo na kufanya uzinzi
na mzazi wako au mzazi wa mke au mume (mkwe) wako au ndugu yako wa damu.
Laana hii huwapata wale wanaotimiza masharti
ya waganga wa kienyeji hasa, ili kujipatia mali za kishirikina.
Kumbukumbu la Torati 27:20,22, na 23. Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake,
kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina. Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya
babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina. Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme,
Amina.
Laana ya kufanya mapenzi na
mnyama.
Ni kwa mtu yo yote aliyewahi kufanya mapenzi
na mnyama kwa kutimiza masharti ya kishirikina na uchawi, kwa taama binafsi au
kwa minajili ya kujipatia fedha, kwa mfano; mbwa, farasi n.k.
Kumbukumbu
la Torati 27:22. Na alaaniwe alalaye
na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina.
Kuna sababu au vitu vingi vinavyoweza kukusababishia laana
katika maisha yako, kazi au biashara yako, ama vitu unavyovimiliki kama shamba
au nyumba.
Na kitu kibaya zaidi ni kwamba laana inarithiwa, kutoka
kizazi kimoja kwenda kinachofuata. Unaweza usione matokea ya laana katika
maisha yako ya sasa na ukaamua kunyamaza ilihali ukijua kuna mambo uliwahi
kufanya yanayofanana na hayo hapo juu. Nakuambia hiyo laana ni lazima
ikufuatilie kama siyo wewe basi ni uzao wako, na kuna watu wanaishi chini ya
laana zilizosababishwa na wazazi wao ambao unaweza ukakuta hawapo hai kwa sasa.
Kumbukumbu la Torati
28:45-46. Na laana hizi zote
zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa
hukusikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake
alizokuagiza; nazo zitakuwa juu yako
kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako
milele.
Je, unaweza kuwa
umelaaniwa pasipo wewe kujua?
Hakika jibu ni ndiyo; unaweza kuwa ulifanya uovu au jambo
lolote kati ya hayo yanayoweza kusababisha laana katika maisha yako, na bado
hujaona matokeo ya hiyo laana katika maisha (labda uwe ulitubu na kuvunja laana
hiyo), kinyume na hapo laana hiyo bado iko juu yako na inakufuatilia kama siyokukupata
wewe basi ni uzao wako, kama tulivyoona kuwa laana inarithiwa (kumbukumbu la
Torati 28:45-46).
Ni vitu gani
vinaweza kulaaniwa?
Kwanza wewe mwenyewe unaweza kupokea laana katika mwili
wako, vitu unavyomiliki kama ardhi, nyumba, mifugo n.k huweza kulaaniwa kwa
ajili yako.
Ardhi. Unailima ardhi lakini hupati mazao kutoka kwake,
unazingatia kilimo cha kisasa lakini mavuno ni haba.
Torati
29:27. Ndipo ikawashwa hasira ya Bwana juu ya nchi (ardhi) hii, kwa kuleta juu yake (ardhi) laana yote
iliyoandikwa katika kitabu hiki.
Uzao wako. Watoto wako wanakuwa wasumbufu haijawahi kutokea;
wana kiburi, wana tabia mbaya, umetumia upole na ukali kuwakanya lakini
hawakusikii, au hata hawana mafanikio kwa kila jambo wanalolifanya.
Torati
28:18. Utalaaniwa uzao wa tumbo
lako.
Mifugo yako. Unajitahidi kufuga mifugo kwa njia za kisasa,
lakini mifugo haiongezeki, ikizaa watoto wanakufa, au kila siku unaibiwa wewe,
mifugo yako inapotea pasipo kuonekana.
Torati
28:18. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa
kondoo zako (mifugo yako).
Kazi za mikono yako na uchumi wako kwa ujumla. Unafanya kazi
au biashara ambayo huoni faida yake, zaidi ya kukupatia fedha ya kujikimu tu.
Umekuwa na uchumi ule ule miaka nenda rudi na ndiyo kwanza unazidi kushuka
chini.
Torati
28:20. Bwana atakuletea laana na
mashaka, na kukemewa katika yote
utakayotia mkono wako kuyafanya (kazi na biashara zako), hata uangamie na
kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniachia kwayo.
Nyumba yako. Unaweza ukawa umejenga nyumba lakini huna
furaha nayo, hutamani kuendelea kuishi ndani yake, unaona ni afadhari ukapange
kuliko kuendelea kuishi ndani ya nyumba yako uliyoijenga au kuinunua kwa fedha
yako mwenyewe.
Mithali
3:33. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, bali huibariki
maskani ya wenye haki.
Mwili wako. Unapata magonjwa yasiyo na sababu, ukifuatilia
chanzo cha magonjwa au wapi ulipata maambukizo hakuna unakoweza kupata jibu. Na
hata ukienda hospitali bado hupati uponyaji.
2
Nyakati 7:13. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula
nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni (magonjwa).
Anga au mbingu. Mvua hainyeshi au hainyeshi kwa wakati.
Maombi yako hayafiki mbele za Mungu, anga imefungwa isipitishe kitu chochote
kwa ajili yako.
2
Nyakati 6:26. Ikiwa mbingu
zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe.
Hadi kufikia mwisho wa somo hili nina imani kuwa umetambua
laana ni nini na ikiwa upo chini ya laana na hukujua, basi leo umefumbuliwa
macho. Sitaki nikuache hivi hivi, nitafanya maombezi kwa ajili yako ili Mungu
akurehemu na kukufungua vifungo vyote vya laana. Kwanza kabisa nataka nikuombe
rehema na kisha nivunje na kufuta laana zote na kutamka baraka katika maisha
yako.
Unachotakiwa kufanya ni kunipa ushirikiano ambao ni;
unatakiwa kuwa na imani thabiti, kwani si mimi ninayetenda hili, bali Yesu
Kristo mwenyewe anakwenda kuhusika na ninakuhakikishia utatoa ushuhuda mzuri wa
ushindi baada ya maombi haya.
Wewe mwenyewe utakwenda kuyasoma maombi haya, ni maombi
yenye nguvu na uwezo wa Mungu (Yehova); kwa imani gusa kioo cha kompyuta yako,
simu yako au kitu chochote unachotumia kufuatilia somo hili:-
Toba: Ee Yesu Kristo nasogea mbele zako mimi na nafsi yangu,
ninaomba unisamehe dhambi zangu zote, unitakase kwa damu yako ya thamani
iliyomwagika pale msalabani kwa ondoleo la dhambi za wanadamu. Ulifute jina
langu katika kitabu cha hukumu na uliandike katika kitabu chako cha uzima.
Amina.
Maombi: Mungu Baba katika jina la Yesu Kristo, ninamleta mtu
huyu asiye na msaada wo wote zaidi yako, na imani iliyomo ndani yake kwako,
msamehe makosa yake yote, umtakase na kumuosha kwa damu ya Yesu Kristo.
Ninafuta kila laana na mikosi katika misha yake, iliyosababishwa na kila namna
ya sababu, ninatamka baraka na ushindi katika maisha yake yote, yeye mwenyewe,
familia yake na uzao wake wote unakwenda kubarikiwa sasa, mifugo yake, kazi za
mikono yake, mashamba yake na nyumba yake, vyote vikabarikiwe sasa, kwa jina la
Yesu Kristo. Amina.
- Kama unataka kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako sasa, bonyeza HAPA.
- Ku-download Full PDF ya somo hili, bonyeza HAPA
No comments:
Post a Comment