Kutoka 15:26 “…kwa
kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.” Watu wengi wamekuwa wakihangaika kwenda
huku na huko wakitafuta uponyaji wa magonjwa na madhaifu ya namna mbali mbali
yanayowasumbua katika afya za miili yao, inawezekana ukawa wewe au ndugu yako
wa karibu. Na mara nyingine utawakuta watu wa namna hii wamefikia hata hatua ya
kwenda kwa waganga wa kienyeji. Ngoja nikufungue akili utambue kitu; ili mtu
awe daktari ni lazima afundishwe na madaktari masomo yanayohusu udaktari, na
ili mtu awe mganga wa kienyeji ni lazima afundishwe uganga wa kienyeji na
mganga wa kienyeji. Na ukikuta mganga wa kienyeji anasema ngoja tuiulize mizimu
ama kwa lugha nyingine wanawaita waungwana utambue moja kwa moja kuwa uganga
wake una mahusiano na nguvu za giza (uchawi). Ni vema kutumia chakula; mboga za
majani na matunda kwa kujenga na kulinda afya yako na hata kutibu baadhi ya
magonjwa kama masomo yapatikanayo katika ukurasa wa dondoo za afya (Health
Tips) yanavyokuelekeza.
Napenda nikwambie
kama jinsi Mungu anvyosema, “Mimi ndimi Bwana nikuponyaye” anamaanisha
anachokisema na kamwe Mungu hajawahi na hatawahi kusema uongo. Hebu tuangalie
ahadi nyingine za neno la Mungu kuhusu kutuponya na magonjwa na madhaifu
yanayotupata:-
Kutoka 23:25 “…,Nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.”, Zaburi 103:3 “Akuponya magonjwa yako yote.”,
Isaya 33:24 “Wala hapana mwenyeji atakaye sema, Mimi mgonjwa.”, Yeremia 30:17 “Maana
nitakurudishia afya, name nitakuponya jeraha zako, asema Bwana.”, Mathayo 4:23 “na
kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.”, Luka 9:11 “akawaponya
wale wenye haja ya kuponywa.”
Hizo ni chache katika ahadi za Mungu nyingi zinazoahidi
uponyaji wa magonjwa na madhaifu yanayo kusumbua. Na kama Bwana asemavyo, “Mimi
ndimi Bwana nikuponyaye, akuponya magonjwa yako yote(Zaburi 103:3), maana
nitakurudishia afya (Yeremia 30:17)”. Katika mistari hiyo Mungu anatuonesha
kuwa anao uwezo wa kuponya kila namna au aina ya ugonjwa na udhaifu ndani ya
miili yetu. Na katika neno lake amesema “akawaponya wale wenye haja ya kuponywa
(Luka 9:11)”, hapo Mungu anatufundisha kitu kinachoitwa imani na kumtegemea
yeye. Ili uweze kupokea uponyaji unapaswa uwe na imani na umtegemee Mungu
asilimia mia moja, kwa sababu imani hutupatia haki ya kupokea kutoka kwa Bwana
Mungu (soma: Mwanzo 15:6 “Akamwamini Bwana, naye akamuhesabia jambo hili kuwa
haki”). Kwa hiyo imani inakupa haki ya kupokea kile unachokiamini, endelea
kumwamini Bwana na kuomba uponyaji wako uko njiani usikate tama kwani Mungu
yuko karibu akuponye.
Ikiwa umelipokea neno
hili kwa imani, na utaamua kulifanyia kazi nakuhakikishia utapokea uponyaji
wako kwa Jina la Yesu Kristo Bwana wetu, Amina.
No comments:
Post a Comment