Imani yako ni ufunguo unaofungua baraka na wema wa Mungu maishani mwako (picha kwa hisani ya "ChristArt") |
Ahadi ni nini?
Ahadi ni tangazo maalumu linalothibitisha kutendewa jambo
lililo nje ya uwezo wako na mtu mwingine au uthibitisho maalumu kwamba jambo fulani
lisilotegemewa kutoke litakwenda kutokea.
Ahadi za Mungu zipo katika nene lake (Biblia) kwa
wamuaminio. Ahadi hizo ni kutuokoa kutoka kila aina ya maumivu na mateso (njaa,
ufukara, magonjwa, vita n.k) na kutujaza mema yake yote (kibari, baraka, amani,
furaha, utajiri wa kiroho na kimwili).
Soma vifungu vifuatavyo vya Biblia uone ahadi za Mungu
zitupazo tumaini la ukombozi dhidi ya dhiki na mateso ya adui shetani (Wagalatia
5:1, Yakobo 4:7, Zaburi 32:7, Zaburi 34:4, Isaya 43:18-19, Yohana wa kwanza
5:4-5) kwa uchache. Kuna vifungu vingi sana katika Biblia takatifu ambavyo
Mungu anasema na kila anayemuamini kwa suala la kumkomboa kutoka dhuluma za
shetani.
Soma vifungu vifuatavyo vya Biblia unoe ahadi za Mungu ziachiliazo
mema ya Mungu kwao wamuaminio (2 Samweli 7:28, Zaburi 5:12, Isaya 43:2, Zaburi
84:11, Mathayo 7:11, Zaburi 23:6, Marko 10:29-30) kwa uchache. Neno la Mungu
linabeba ahadi nyinyi sana za wema wa Mungu kwa wanaoamuamini, kazi ya
mwanadamu ni ndogo sana, ni kumuamini Mungu tu, kisha mema ya Mungu yanatimizwa
katika maisha yako. Kosa kubwa linalofanywa na waamini wengi ni kumfanya Mungu
mbadala. Muamini anaamini ahadi ya kupokea mema ya Mungu lakini kwa wakati huo
huo anatafuta njia mbadala za kupokea mema hayo tena hata kwa njia
zisizompendeza Mungu. Kwa mfano, muamini anaweza kuwa anaomba uponyaji kwa
Mungu kupitia neno la Mungu linalobeba ahadi za Mungu za uponyaji na wakati huo
huo anahangaika kwa waganga wa nguvu za giza kutafuta msaada. Hata siku moja
Mungu hafanyi kazi na watu wanomfanya yeye kama mbadala “alternative” wa njia
zao wenyewe.
Soma vizuri mstari wa Biblia wa Marko 10:29-30, kupokea mema
ya Mungu kwa kipimo kilichojazwa na kusukwa sukwa hata kinafurika inahitaji
kujikana. Ni lazima muamini uachane na kona kona za dunia hii na kuamua
kumfanya Mungu ndio msaada na tumaini lako pekee.
Je ahadi za Mungu ni za aina gani?
Ahadi za
Mungu zimehakikishwa (ahadi timilifu).
2 Samweli
22:31(b). Mungu, njia yake ni kamilifu; ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye
ndiye ngao yao wote wanaomkimbilia.
Mungu hasemi
uongo.
Hesabu
23:19(a). Mungu si mtu, aseme uongo.
Mungu ni
mwaminifu, hutekeleza alichoahidi.
Kumbukumbu
7:9. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu,
ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata
vizazi elfu.
Tukiomba
sawasawa na mapenzi (ahadi) yake, atusikia.
1 Yohana
5:14. Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na
mapenzi yake (sawa sawa na neno au ahadi yake), atusikia.
Ni lazima
atimize ahadi yake kwanza, kwa sababu ameikuza kuliko jina lake.
Zaburi
138:2. Nitakusujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, nitalishukuru Jina lako
kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana umeikuza ahadi yako
kuliko jina lako lote.
Tofauti ya
ahadi za Mungu na ahadi za kipepo/kishetani
Ahadi za
Mungu zinatimia kwa wanaomtegemea Mungu kwa asilimia mia moja (100%), ambao
hawamfanyi Mungu ni mbadala wa njia zao binafsi. Pia, ahadi za Mungu hazitimii
pasipo kuwa na muda wa ukomavu kiimani ili kuweza kuzipokea na kuzitunza ahadi
hizo. Soma Biblia vizuri kwa msaada wa Roho Mtakaktifu utaelewa, watu wote
Mungu aliofanya nao ahadi, kuna muda ulipita kabla ya ahadi zile kutimia. Angalia
mifano ifuatayo;
Ahadi ya
Mungu kwa Ibrahimu
Ahadi ya
Mungu na Ibrahimu kuhusu uzao wa ahadi “the promised seed”, ilimchukua Ibrahimu
miaka isiyopungua 13 kuipokea ahadi hii (Mwanzo 17-32).
Ahadi ya
Mungu kwa Daudi
Ilimgharimu takribani
miaka 15 Daudi tangu apakwe mafuta na Samweli nabii hadi kuwa mfalme wa Israeli
taifa teule la Mungu (1 Samweli 16).
Mungu
akifanya ahadi na muamini huachilia muda wa ukomavu “maturity” ambao
utaambatana na majaribio kadhaa. Majaribio haya lengo lake ni kumuimarisha
muamini na siyo kumuangusha ili aonekane hafai “disqualifying”. Kama tumaini la
muamini ni Mungu pekee, kwa hakika atavuka salama na kwa ushindi wenye kumpa
sifa na utukufu Mungu kuelekea ukuu, kwa sababu kwa neema ya Mungu tunakuwa
kutoka hatua moja hadi nyingine. Muamini yoyte atakaye mfanya Mungu ni mbadala
wa njia za kibinadamu, kwa hakika hataweza kuvuka kipindi hiki cha majaribio. Na
hapa ndipo wengi wanapofeli na kudhani hakuna mafanikio kwa wamtumainio Mungu.
Mafanikio yapo tele, ikiwa wewe umeshindwa usiwakatishe tamaa wengine (hii ni
tabia ya adui, ibilisi).
Mafanikio ya
kipepo/kishetani/kichawi ni mafanikio yanayopatikana baada ya muda mfupi sana
na yanaambatana na sadaka ya umwagaji damu mar azote. Mafanikio ya kishetani yana
mateso makubwa ndani yake, wengi waliofanikiwa kwa njia hii huwa na furaha na
sura za vicheko mbele za watu lakini wakiwa peke yao usiku ni mateso na majuto.
Ahadi hizi zina kitanzi cha umauti na hazidumu. Mwisho wa mafanikio ya kipepo
ni mauti na uharibifu.
Ukomo wa
ahadi za Mungu
Ahadi za
Mungu zinakoma mara tu muamini anapoacha kumtegemea Mungu. Kwa ufafanuzi Zaidi,
Mungu akikuahidi jambo, mfano kukupatia mtoto baada ya miaka kadhaa ya
kuhangaika huku na huko, katika kipindi cha mpito kuelekea kutimia kwa ahadi ya
Mungu, ukahisi Mungu anachelewa sana ukaanza kuingiza mambo ya wanadamu sijui
meza miti shamba fulani, sijui twende kwa mtaalamu fulani, sijui twende kwa
bibi au babu fulani amewasaidia wengi na wewe utafanikiwa, hapo ndipo Mungu
anakuacha uzitumainie akili zako na yeye anakaa pembeni. Ni kweli unaweza
fanikiwa kupata mtoto lakini mtoto utakaye mpata anakuwa na asili ya kipepo kwa
sababu ni mali ya mapepo na amepatikana kwa nguvu za giza.
Labda nikupe
mfano rahisi, wengi tunajiunganisha katika huduma za maji safi za miji au
majiji tunamoishi kwa kutumia mabomba maalumu. Kupitia hilo bomba, maji
yanatiririka kuja majumbani mwetu. Ikitokea ukaamua kukata hilo bomba kutoka
maji safi na kuliunganisha kwenye bomba la maji taka hakika utegemee kupokea
maji taka nyumbani mwako. Na hii ndivyo inavyokuwa pale tunapoamua kuacha
kumtegemea Mungu, siyo kwamba Mungu anaamua kukata Baraka na wema wake kwetu,
la hasha, bali sisi ndio tunakuwa tumejiondoa katika mfereji wa kupokea baraka na
wema wa Mungu. Kwa sababu imani yetu kwa Mungu ndiyo mlango na bomba pekee ya
kuachilia baraka na wema wake kwetu.
Hitimisho
Endapo unadhani
ulijiondoa katika mfereji wa baraka na wema wa Mungu na unataka kujiunganisha
tene soma vifungu vya Biblia vifuatavyo (2 Mambo ya Nyakati 30:9 na 2 Mambo ya
Nyakati 7:14) na uhakikishe unaomba toba na kurejea tena kwa Mungu. Mungu wetu
(Yehova) ni mwingi wa rehema, uwe na imani kuwa atakusamehe na kukubariki na
kukufunika na wema wake.
“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu,
watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi,
nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” 2
Mambo ya Nyakati 7:14. Kuiponya nchi, ni kuachilia baraka na wema wa Mungu
katikati ya maisha ya wanaomuamini. Ujue ya kwamba, paripo na baraka au wema wa
Mungu laana na mikosi haiwezi ikakaa hapo.
Bwana akubariki
ReplyDelete