Sadaka ni nini?
Sadaka igusayo moyo hutolewa katika upendo (Picha:clipart-library.com) |
Sadaka ni toleo la thamani (kwako
unayetoa mfano wa fedha, mnyama au mali ya aina nyingine) kwa Mungu kwa
makusudi ya kupata baraka, kibali, toba au kutii agizo la Mungu (Mwanzo 22:2, 1
Wafalme 17:13-16 na Mambo ya Walawi 4). Sadaka inagawanyika katika makundi
mawili makubwa; 1. Sadaka ya kumwaga damu, sadaka hii ilianzishwa na kumalizwa
na Mungu mwenyewe. Baada ya Adam na Eva kumkosea Mungu kwa kula tunda la mti wa
katikati, Mungu aliwavika vazi la ngozi ya mnyama, hii maana yake Mungu
alimwaga damu ya mnyama ili kuwavika vazi la kuficha dhambi yao (Mwanzo 3:21).
Kupitia kumwaga damu kwa Yesu Kristo katika kifo cha msalaba, dhambi za
wanadamu zinasamehewa na kufutwa kabisa (Waebrania 9:22, Mathayo 5:17, Yohana
3:16, Matendo ya Mitume 4:12 na Yohana 1:29). 2. Sadaka isiyomwaga damu, sadaka
hii ni mazao ya ardhi kama nafaka, matunda n.k. Sadaka inaweza kutolewa moja
kwa moja kwenye madhabahu ya Mungu ama ikatolewa kwa mwanadamu mwingine. Mara
zote sadaka inayotolewa kwa mwanadamu inapaswa kutolewa kwa wenye uhitaji mfano
wajane au yatima wasiojiweza (Yakobo 1:27). Sadaka inatakiwa kutolewa kwa moyo
wa kupenda kwa kadiri Roho wa Mungu atakavyosema nawe (kwa kadiri ya sauti ya
utoaji utakayoisikia moyoni au nafsini mwako). Sadaka itolewayo kana kwamba
unamsaidia Mungu ama unatoa ili mradi uonekane machoni pa watu kuwa nawe umetoa
haimbariki Mungu na kamwe usitegemee kuugusa moyo wa Mungu kwa utoaji huo na
pia usitegemee Baraka za Mungu (Marko 12:41-44).
Maana ya sadaka ya ushawishi
Sadaka ya ushawishi ni sadaka
inayotolewa ili kumshawishi Mungu akutatulie changamoto unayoipitia kwa wakati
huo. Aina na kiasi cha sadaka hii hutolewa maelekezo na Mungu mwenyewe, mara
nyingi unapokuwa katika maombi ya kuomba mkono wa Mungu ukuokoe kutoka katika
shida Fulani ndipo utasikia sauti ya Mungu ikikuelekeza kutoa sadaka ya aina na
kiasi fulani katika madhabahu fulani au kumpatia mtu fulani. Siyo kila
anaeingia katika maombi ya kuomba msaada wa Mungu ataelekezwa kutoa sadaka hii.
Mungu alipotaka kufanya agano na Ibrahimu (baba yetu wa Imani), Ibrahimu
alimuuliza Mungu kuhusu uzao na Mungu akamjibu Ibrahimu kuwa atampatia uzao
lakini alitaka kwake (kwanza) amtolee sadaka (Mwanzo 15).
Tofauti ya sadaka ya ushawishi na
nadhiri
Sadaka ya ushawishi ni sadaka
inayotolewa kwanza (muamini akiwa ndani ya kifungo au shida) ili Mungu afungue
milango ya kifungo fulani wakati sadaka ya nadhiri ni sadaka ambayo muamini
anaahidi kumtolea Mungu mara baada ya Mungu kumvusha katika kifungo au shida
fulani. Kwa mfano, katika hali ya udhaifu au ugonjwa, muamini anamtolea Mungu
sadaka inayosukuma maombi yake ili Mungu aachilie uponyaji (hii ni sadaka ya
ushawishi) na ahadi ya sadaka anyotoa muamini kumpatia Mungu mara baada ya
kuponywa (hii ni sadaka ya nadhiri).
Wakati gani ni sahihi kutoa sadaka ya
ushawishi?
Wakati sahihi wa kutoa sadaka ya
ushawishi ni mara baada ya kusikia sauti ya Mungu ikikuelekeza kufanya hivyo.
Faida za sadaka ya ushawishi
Faida kuu ya sadaka ya ushawishi ni
kumuonesha Mungu utii na imani yako kwake na hivyo kumfanya aharakishe katika
kuachilia majibu ya maombi yako.
No comments:
Post a Comment